• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Chanjo ya corona ilivyo changamoto kwa wazee

Chanjo ya corona ilivyo changamoto kwa wazee

NA PAULINE ONGAJI

Alipopata dozi ya kwanza ya chanjo ya virusi vya corona mnamo Aprili 23, 2021, Anne Musanga, 70, mkazi wa eneo la Makina katika kitongoji duni cha Kibera, Kaunti ya Nairobi, alidhani kwamba baada ya majuma manane kama ilivyo matarajio, angepokea chanjo yake ya mwisho na hivyo kujihakikishia usalama dhidi ya maradhi haya.

Lakini hilo halikutendeka. Kulingana naye, pindi baada ya kuchanjwa, alikumbwa na tatizo la shinikizo la damu na kuagizwa na daktari kuanza kutumia dawa mara moja.

Ripoti yake ya matibabu inaonyesha kwamba presha ya damu ilikuwa 171 dhidi ya 83 (171/83 mmhg), ishara kwamba alikuwa katika awamu ya pili ya tatizo la shinikizo la damu.Hali hii ilichelewesha dozi ya pili ambayo alifaa kupokea Juni 26, na tangu wakati huo, bado hajapata idhini ya daktari.

“Nilishauriwa kwamba nikamilishe dawa na kufanyiwa uchunguzi wa kila mara wa kimatibabu kabla ya kupata dozi ya ya pili,” aongeza.

Kwa upande mwingine, Molly Aluoch Oloo, 73, kutoka eneo la Katwekera, Kibera, asema kwamba mwanzoni alihofia kudungwa sindano hiyo kutokana na taarifa za kupotosha sio tu kuhusiana na chanjo hiyo, bali maradhi hayo kwa ujumla.

“Nusura nisipokee chanjo kabisa lakini nikabadili msimamo baada ya kushiriki katika vikao kadhaa vya uhamasisho,” aongeza.

Kwa bahati nzuri, asema, hakushuhudia athari zozote za kiafya kutokana chanjo, suala lililomfanya kujitwika jukumu la kuhimiza wazee wenzake pia kuchanjwa.

Wallace Gachau, 71, kutoka Lang’ata, Kaunti ya Nairobi, asema, kilichomsukuma zaidi kuchanjwa ni kufahamu umuhimu wake, hasa ikizingatiwa kwamba, kabla ya kustaafu mwaka wa 2006, alikuwa mfanyakazi msaidizi hospitalini.

“Aidha, nilikuwa nimejifunza mengi kuhusiana na maradhi haya, ambapo nilielewa hatari zake hasa kwa watu walio na umri kama wangu,” asema.

Naye Macfidensio Mureithi, 69, mfanyabiashara kutoka eneo la Makina, mtaani Kibera, asema ngano kibao kuhusu matatizo ya kiafya, vilevile vifo kutokana na maradhi haya, vilimhimiza kupokea chanjo.

Yeye pia alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuchanjwa nchini mwezi Machi. Hata hivyo, ari yake ya kupokea dozi ya pili mwezi Juni ilisitishwa baada ya serikali kutangaza kwamba kulikuwa na upungufu.

“Wakati wa dozi ya pili ulipokaribia, nilipokea ujumbe kutoka Wizara ya Afya nchini ukiniarifu kwamba chanjo hazikuwepo,” aeleza.

Hata hivyo, mwezi Julai serikali ilipotangaza kwamba bidhaa hii inapatikana, alienda hospitalini na akachanjwa.Kulingana na Wizara ya Afya, kufikia Septemba 1, 2021, dozi 2,807,945 za chanjo zilikuwa zimetolea nchini kote, ambapo jumla ya dozi za kwanza zilizotolewa ilikuwa 2,000,285, huku jumla ya dozi za pili zilizokuwa zimetolea ikiwa 807,660.

Dozi ya kwanza ya chanjo kwa watu waliozidi umri wa miaka 58 ilikuwa 424, 919 ambayo ni sawa na zaidi ya 21% ya jumla ya dozi za kwanza za chanjo zilizotolewa.Kwa upande mwingine, watu walio katika mabano haya ya umri waliokuwa wamepokea dozi ya pili walikuwa 240, 293, takriban 30% ya jumla ya dozi zote za pili zilizotolewa.

Aidha, kufikia wakati huo, takwimu zinaonyesha kwamba 56.6% ya walio na umri wa zaidi ya 58 waliokuwa wamepokea dozi ya kwanza, walipokea pia ya pili.Lakini japo takwimu hizi ni za kutia moyo, ni 9.3% pekee ya watu wenye umri huu waliokuwa wamepokea chanjo kamili dhidi ya maradhi haya.

Ni suala linaloibua swali kwa nini asilimia hii ni ya chini hivi? Wataalamu wanahoji kwamba kuna masuala kadha wa kadha ambayo yamesababisha watu wa umri wa zaidi ya miaka 58 kususia chanjo.Kulingana na Jude Otogo, mwakilishi shirika la HelpAge International nchini, shirika linalopigania haki za wazee, mojawapo ya sababu kuu ni umaskini.

Takwimu za shirika la HelpAge zinaonyesha kwamba ni watu wanne pekee miongoni mwa 100, wanaopokea malipo ya uzeeni hapa nchini. Hii inawaacha wengi bila mbinu yoyote ya mapato katika umri wa uzeeni.

Kulingana na Dkt Stephanie Hauck, mshauri katika kitengo cha kuzuia maambukizi hatari katika Shirika la Afya Duniani, eneo la Afrika Mashariki na Mediterania, wazee wamo katika hatari kubwa wakati huu wa janga la corona, kutokana na sababu kwamba wanawategemea wengine kimaisha.

“Hasa hali ni mbaya zaidi kwa mukadha wa Afrika ambapo wengi wao wanawategemea watoto na wajukuu zao ili kupata mahitaji ya kila siku, huku suala la marufuku ya usafiri na kujitenga yakitatiza mambo hata zaidi,” aeleza.

Bw Otogo asema kwamba hali si hali hasa kwa wanaoishi katika mitaa ya mabanda. Kwanza kabisa asema, kwa wanaoishi mbali na vituo vya kiafya, changamoto ni kupata nauli ya kusafiri ili kwenda kupokea chanjo.

“Lakini pia, wanaokumbwa na changamoto ya kiuchumi hawana muda wa kupanga foleni katika vituo vya afya kwani wakati mwingi wako katika harakati za kujitafutia mapato,” aeleza.

Hili ni tatizo ambalo limemkumba Edward Nyundo, 75, kutoka eneo la Kibera 42. Bw Nyundo ambaye ni mlinzi wa usiku hajapokea chanjo yoyote akidai anachokipa kipaumbele kwa sasa ni kufanya kazi ili kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

“Mimi hufanya kazi kama mlinzi wa usiku ambapo wakati wa mchana inanibidi nilale ili kujiandaa kuingia kazini jioni. Endapo nitachukua nafasi kwenda kupanga foleni na pengine ichukue muda mrefu, nitashindwa kwenda kazini jioni. Nitakula nini?” ahoji.

Kulingana na Dkt Willis Akhwale, Mwenyekiti wa jopokazi la usambazaji wa chanjo nchini, mwanzoni wazee hawakuwa miongoni mwa makundi yaliyopewa kipaumbele katika upokeaji chanjo, hadi wimbi la tatu lilipojiri. Lakini aongeza kwamba hili ni suala dogo.

“Tatizo kuu ni kwamba wazee hawaji hospitalini kwa sababu wanahofia wataambukizwa maradhi haya. Kumbuka kwamba hiki ni kikundi cha watu walio na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na matatizo mengine ya kiafya kama vile kisukari. Hali inakuwa mbaya hata zaidi kutokana na dhana potovu kwamba kupokea chanjo kutafanya hali yao ya kiafya kuwa mbaya hata zaidi,” aongeza.

Ni changamoto ambayo Yasmin Abdulrahman Aboyo, msimamizi msaidizi katika kituo cha wazee cha Kibera Day Care Center For The Elderly, asema, imetatiza kampeni zao za kuhimiza watu kuchanjwa.

“Tumeshuhudia visa vingi vya kuenezwa kwa hofu miongoni mwa baadhi ya watu ambao baada ya kupokea dozi ya kwanza au zote, pengine walishuhudia athari kidogo, na wametumia matatizo hayo kama visingizio vya kuwatahadharisha wenzao dhidi ya kudungwa sindano hii,” aeleza.

Dkt Hauck, asema huenda hii ikawa na athari baadaye. “Huenda mambo yakawa mabaya hata zaidi ikiwa pia vijana watasusia chanjo hii kwani wanaweza wakawaambukiza, na hivyo kuwaweka kwenye hatari ya kiafya,” aongeza.

Dkt Akhwale asema hii ni changamoto ambayo itakabiliwa vilivyo kupitia elimu. “Watu wanapaswa kuelewa kwamba mara nyingi chanjo huwa na athari zake.

Lakini je, hii inamaanisha kwamba tunapaswa kususia? La hasha,” asema.Hata hivyo, kuna matumaini kwani takwimu zaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la watu zaidi ya umri wa miaka 58, wanaoendea dozi ya kwanza ya chanjo. Kwa nini?

“Mwezi Mei tulikuwa tumesitisha shughuli za kuwapa watu dozi ya kwanza, hadi waliopokea awali kukamilisha dozi zote mbili. Lakini baada ya kupokea chanjo za kutosha, shughuli hii iliendelea na imechangia ongezeko hili. Aidha, awali tulikuwa na vituo vichache vya kutoa chanjo ikilinganishwa na sasa,” aongeza Dkt Akhwale.

Pia asema kwamba hii ni kutokana na ongezeko la kampeni za uhamasishaji, suala ambalo limefanya iwe rahisi kufikia taarifa kuhusiana na corona vilevile chanjo.Bw Otogo asema pia ukosefu wa shughuli za uhamasishaji na kampeni kuwalenga wazee vimekuwa kizingiti.

“Shughuli za kiafya na kampeni kuwasaidia wazee hazipo, ikilinganishwa na makundi mengine kama vile akina mama wajawazito, watoto na walemavu. Hii ni licha ya kwamba wanajumuisha asilimia kubwa ya idadi ya watu,” asema.

Dkt Akhwale asema kwamba ili kufikia watu katika mabano ya umri huu, jopokazi la chanjo limetoa mapendekezo fulani.

“Tumependekeza matumizi ya wahudumu wa kiafya. Aidha, tumelenga shughuli za uhamasishaji miongoni mwa kikundi hiki kupitia wahudumu wa kijamii. Aidha, wanapaswa kupokea chanjo katika kliniki maalum wanapoenda kufanyiwa ukaguzi wa kawaida wa kiafaya,” aongeza.

 

|Makala haya yamefadhiliwa na mradi wa Code for Africa’s WanaData kama sehemu ya the Data4COVID19 Africa Challenge chini ya l’Agence française de développement (AFD), Expertise France, na The GovLab|

You can share this post!

Jaji alipanga njama za kumuua bwanyenye Tob Cohen, korti...

DKT FLO: Chunusi sehemu ya siri ni tatizo la kiafya?