• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:26 PM
Davis Chirchir: Huenda lita moja ya petroli ikagonga Sh300

Davis Chirchir: Huenda lita moja ya petroli ikagonga Sh300

NA SAMMY WAWERU

Huku wananchi wa Tanzania wakipumua baada ya serikali kupunguza bei ya mafuta, nchini Kenya Waziri wa Kawi, Davis Chirchir amebashiri kwamba bei ya petroli huenda ikaongezeka zaidi kutokana na mfumko anaosema serikali haina uwezo kuudhibiti.

Kulingana na tangazo lililotolewa na Wizara ya Kawi ya Tanzania kwa ajili ya mwezi wa Novemba, bei ya mafuta ya petroli imeshuka  hadi Sh197.91, nayo dizeli ikishuka hadi Sh203.93 huku mafuta-taa yakifika Sh206.9. Hii ni kinyume na Kenya kwa sasa ambapo petroli inauzwa Sh217, dizeli Sh205 na mafuta-taa Sh205 huku bei mpya zikitarajiwa kutangazwa Novemba 14.

Akizungumza Jumatatu, Novemba 6, 2023 alipofika mbele ya Kamati ya Kitaifa Kuhusu Maridhiano, Bw Chirchir alisema ongezeko la bei ya bidhaa za petroli limechangiwa na vita kati ya Urusi na Ukraine, na chocheo lingine la hivi karibuni likiwa mzozo unaoendelea baina ya Israel na Hamas.

Mwezi Oktoba 2023, Israel na Hamas – Palestina vita vilizuka, Waziri Davis akisema mgogoro kati ya mataifa hayo mawili umechangia zaidi nyongeza ya petroli, dizeli na mafuta ya taa.

“Siku kadha zilizopita, nilisoma taarifa kwenye Gazeti la Financial Times kwa sababu ya vita vinavyoendelea kati ya Hamas na Israel bei ya bareli moja (kipimo cha mafuta) kimataifa huenda ikagonga Dola 150 (USD) – (sawa na Sh22, 717.50 thamani ya pesa za Kenya). Na hiyo inamaanisha lita moja ya mafuta ya petroli itafika Sh300. Tunatumai haitafika hapo,” Bw Chirchir akasema.

Oktoba 14, 2023, Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Bidhaa za Petroli (EPRA) ilitangaza nyongeza ya bei ya petroli ya Sh5.72, dizeli Sh4.48 na mafuta taa Sh2.45, kwa kila lita.

Nyongeza hiyo ilianza kutekelezwa Oktoba 15, petroli, dizeli na mafuta taa yakiuzwa Sh217.36, Sh205.47 na 205.06 kwa lita, mtawalia.

Mnamo Jumatatu, Novemba 6, Waziri Chirchir alisema mfumko huo unatokana na kuendelea kuongezeka kwa bei ya bareli kwa sababu ya vita vinavyoendelea katika mataifa ambayo yana mchango mkubwa zaidi duniani kuzalisha mafuta (Urusi, Ukraine, Israel na Palestina – Hamas).

“Changamoto tunazopitia ni za kimataifa na hatuna mamlaka yoyote kuzuia hali, ikizingatiwa kuwa bareli imepanda kutoka Dola 70 (USD) – Sh10, 591, ikawa Dola 80 (USD) – Sh12, 1014 na sasa ni Dola 90 (USD) – Sh13, 617,” Bw Chirchir akaambia Kamati ya Kitaifa Kuhusu Maridhiano.

Mfumko huo umesababisha Dola kuwa ghali, hivyo basi kufifisha nguvu ya Shilingi ya Kenya.

Hata hivyo, Waziri huyo wa Kawi anasema kufuatia hatua ya serikali ya Kenya kuagiza mafuta ya petroli moja kwa moja kutoka Milki ya Kiarabu (UAE), imesaidia kwa kiwango kikubwa kudhibiti mfumko mkali.

“Kenya inaagiza bareli ya dizeli kwa Dola 88 (USD) – Sh13, 314 kwa sasa, na petroli Dola 95 (USD) – Sh14, 373.50, kinyume na mataifa mengine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kama vile Tanzania inayoagiza bareli moja kwa Dola 160 (USD) Sh24, 208,” akaelezea.

EPRA inatarajiwa kutangaza bei mpya ya mafuta mnamo Novemba 14 au 15, na haijabainika ikiwa yataongezeka bei.

Nyongeza ya bidhaa za petroli na kufifia kwa Shilingi ya Kenya kunazidi kusababisha gharama ya maisha kupanda.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Makanisa 20 yaandaa maombi ‘kutakasa’ eneo la Turkwel...

Raila amwambia Ruto aache kutangatanga, achape kazi

T L