• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
DCI aliyekataa hongo ya Sh200, 000 na kukamata matapeli 2 wa mashamba   

DCI aliyekataa hongo ya Sh200, 000 na kukamata matapeli 2 wa mashamba  

NA MWANGI MUIRURI

WASHUKIWA wawili wa utapeli wa mashamba na ufisadi walipoingiwa na ujasiri wa ajabu na wakaingia katika makao makuu ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) wakisaka wa kuhongana Sh200, 000 walijipata taabani Desemba 7, 2023 walipotiwa mbaroni.

Bila ufahamu kwamba makao hayo yamejaa kamera za siri, walitandaza mabunda ya manoti juu ya meza wakiyahesabu polepole ili maafisa hao wamezee mate lakini wakajipata wamezingirwa na kukamatwa huku pesa hizo zikiwekwa kama ushahidi.

Bw Jackson Mwangi Wambui 44, na Bw Elijah Macharia 49 ambao DCI imewataja kama washukiwa sugu wa kutapeli mashamba yanayomilikiwa na wakongwe wa kigeni wanaoishi hapa nchini walijiingiza kwa moto kwa miguu yao wenyewe.

“Wawili hao walijitokeza katika kitengo cha uchunguzi wa jinai kuhusu utapeli wa ardhi wakitafuta afisa wa kuhonga ili awasaidie kufisadi umiliki wa kipande cha ardhi chenye upana wa hekari 0.2026 katika mtaa wa Thome V,” ripoti ya DCI yasema.

Bw Mwangi anasemwa kwamba alikuwa akisaka ndani ya DCI afisa ambaye angemsaidia kuchelewesha uchunguzi dhidi ya umiliki wa kipande hicho cha ardhi kwa angalau miezi miwili ili awe amefanikiwa kupata stakabadhi ghushi za umiliki.

“Kile hawakujua ni kwamba tumekuwa tukifuatilia mienendo yao katika sarakasi za umiliki wa shamba hilo na bila ya kutoka katika makao makuu kwenda kuwasaka, wao walijileta kwa miguu yao hadi ndani ya makao makuu ya DCI, bila mwaliko wowote wala ilani yoyote na wakajitambulisha kama washukiwa hao,” DCI ikasema.

Ripoti zaidi za DCI zilionyesha kuwa Bw Mwangi alikuwa ameweka ua katika shamba hilo lililo nyuma ya Mkahawa wa Roosters na ndipo ripoti ilipigwa kuhusu njama hiyo ya utapeli.

“Walipojua ripoti imepigwa kwetu, waliingia mitini na tumekuwa tukiwasaka. Lakini wameturahisishia kazi kwa kuwa wameamua kujileta hata bila ya kutupa ilani ya mapema tuwangojee, wakajitambulisha na kazi yetu ikawa rahisi kuwaweka pingu,” DCI ikaongeza.

Uchunguzi zaidi sasa umebaini kwamba kipande hicho cha ardhi kilikuwa chini ya umiliki halali wa raia wa kigeni aliyekuwa ameaga dunia na kukiachia kama urithi wa mke na watoto wake wawili na ambao walikuwa wanalengwa na washukiwa hao kupokonywa urithi wao.

Bw Mwangi anaelezewa kuwa ana kesi zingine zinazohusu utapeli wa mashamba.

“Huyu Bw Mwangi alikuwa amejaribu kunyakua shamba la Bw Richard Hooper katika mtaa wa Karen mnamo Januari 18, 2023 na ambapo alijitambulisha kama kamanda wa polisi wa kituo cha Karen,” DCI yasema.

 

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Mganga aliyedai ana uwezo kuponya kifafa asukumwa jela kula...

Mmiliki tapeli wa shule  

T L