• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Del Monte yamulikwa walinzi wake wakihusishwa na mauaji ya kikatili  

Del Monte yamulikwa walinzi wake wakihusishwa na mauaji ya kikatili  

NA MWANGI MUIRURI 

FAMILIA nne kutoka Kaunti ya Machakos zinaomboleza mauti ya wapendwa wao wenye umri wa ujana wanaokisiwa kupigwa na walinzi wa kampuni ya Kimarekani ya Del Monte hadi kufa.

Miili yao ilitolewa siku ya Krisimasi, Desemba 25, 2023 kutoka Mto Chania ikiwa imeelea.

Walionekana mara ya mwisho wikendi wakiwa hai.

“Wote wanne walionekana wakiwa hai na inajulikana wazi kwamba walikuwa wanaenda shamba la Del Monte,” akasema msemaji wa familia hizo, James Kasee.

Alisema kwamba “wakati jamaa zao walitarajia wafike nyumbani kujumuika nao Krismasi, waliitiwa miili yao ikiwa imeoza”.

Bw Kasee alisema kwamba “vijana wengi wasio na ajira hapa huwa wanahangaishana na walinzi wa kampuni hiyo kwa madai ya wizi wa mananasi”.

Ripoti ya polisi ambayo imeandaliwa na kamati ya kiusalama eneo hilo inasema kwamba wanne hao walionekana na wapitanjia katika kingo za mto huo.

“Walikuwa na majeraha mabaya mwilini ya kupigwa, kukatakatwa na kuvunjwa. Miili yenyewe ilikuwa imeanza kuoza na baada ya maafisa wa uchunguzi wa makosa ya jinai (DCI) kutekeleza uchunguzi wa hali na mazingara, waliwasilishwa hadi mochari ya General Kago,” ripoti hiyo inasema.

Aidha, ripoti hiyo inasema kwamba “tumepata habari kwamba walinzi wa kampuni ya Del Monte wanashukiwa kuhusika katika mauaji hayo na hatimaye kuitupa ndani ya mto huo”.

Ripoti hiyo inaongeza kwamba kinachochunguzwa sasa na DCI ni tukio la mauaji na pia uharibifu wa kimazingira kufuatia kutupa miili kwenye maji.

Kampuni ya Del Monte kupitia taarifa ilisema kwamba uchunguzi umeanzishwa ili kubaini ukweli.

Licha ya kwamba ilijitenga na mauti hayo kwa msingi kwamba miili haikupatikana ndani ya shamba lao, kampuni hiyo ilisema itaendeleza uchunguzi.
[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Watoto 12 wazaliwa hospitali tofauti Kirinyaga sikukuu ya...

Sudi adai yeye ndiye ‘mpishi’ katika serikali...

T L