• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
Dhuluma za kisaikolojia zinavyawatesa wanandoa kipindi cha corona

Dhuluma za kisaikolojia zinavyawatesa wanandoa kipindi cha corona

NA WANGU KANURI

AGIZO la serikali la kudhibiti mkurupuko wa ugonjwa wa corona mwaka jana limewashurutisha Wakenya wengi kufanyia kazi majumbani huku idadi kubwa ya watu wakipoteza kazi zao na waliosalia kupunguziwa mishahara.

Kulingana na Shirikisho la Wafanyikazi nchini Kenya (FKE), watu milioni 1.7 waliathiriwa baada ya Covid-19 kubisha nchini.

Ni hali hii ambayo imesababisha ongezeko la visa vya magonjwa ya kiakili na dhuluma za kisaikolojia na za kihisia.

Hatua ya serikali kuagiza kampuni zipunguze watu wanaofanyia kazi ofisini kumewafanya wanandoa wengi kuvurugana sana kwani wamelazimika kufanyia kazi nyumbani. Dhuluma za kihisia na kisaikolojia zilielekezwa mwanandoa asiyechuma hela au aliyesimamishwa kazi.

Mercy ambalo si jina lake halisi, ni mkazi wa Nairobi. Amegonga umri wa miaka 26. Amejaaliwa mtoto mmoja.

Ni mmoja kati ya maelfu ya wanandoa walioathriwa na ugonjwa wa Covid-19. “Nilikuwa nafanya kazi na japo tulikuwa na vurugu hapa kule na mume wangu vurugu hizi zilipigwa jeki wakati ambapo nilipigwa kalamu pindi tu baada ya kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Covid-19 kutangazwa nchini.

“Kutokuwa na kazi kulinifanya nimtegemee mume wangu huku maneno kama ulikuwa unadhani unaweza jidumu kivyako? Mimi ndiye mwanamume kwenye uhusiano huu, yakisheheni.”

Kwa wingi wa machungu, Mercy anakumbuka wakati ambapo mtoto wake ambaye anaugua ugonjwa wa pumu (Asthma), alikuwa anashindwa kupumua na alihitaji matibabu ya dharura.

Mercy alimweleza mumewe hali ya mwanao lakini mumewe akamjibu, “ni heri mtoto afe sina pesa. Dhuluma za kihisia na kisaikolojia ziliendelea na kuwa vita huku nikitaka kujiua,” anaendelea kunisimulia, “nilijaribu kujiua mara kama kumi.”

Mercy anasema kuwa angemwomba mumewe pesa angalau aweze kununua chakula lakini mumewe alikuwa akimweleza ni heri aende akafanye ukahaba.

Kila mara alimkumbusha kuwa wakati alipokuwa na pesa alijidai sasa wakati umefika amtegemee kwa hivyo angempa pesa kwa hiari yake. Mercy, alijitenga sana na kufikiria tu namna ya kujitoa uhai kwani maisha yalikosa maana, wakati huo.

Mvutano kati ya mumewe naye, uliacha athari hasi kwa mwanawe. Mercy anakumbuka akimtolea mwanawe kuwa chanzo cha matatizo yake.

Alichopitia Mercy kinafanana sana na kile alichopitia Mary japo si jina lake halisi, mama mwenye umri wa miaka 28 na mama wa mtoto mmoja.

Mary ananieleza kuwa alijiuzulu kazini baada ya mimba yake kuwa ngumu. Kuondoka kwake kazini kulimlazimu kumtegemea mumewe ambaye alimdhuru si kihisia pekee bali kimwili.

Bidii za kuwaeleza wakwe wake ili waweze kuokoa ndoa ziligonga mwamba huku akiambiwa kuwa ‘Ndoa ni kuvumilia na boma hujengwa na mwanamke.’

Mary alipata ugonjwa wa msongo wa mawazo (Depression) na alikuwa akimwadhibu mwanawe wa miezi minne vikali sana. Isitoshe, alijihisi mpweke huku akijilaumu kwa ndoa yake kusambaratika.

Mary anavuta kumbukizi kana kwamba ni tukio la jana. Alijiwa na wazo la kumdunga mumewe kwa kisu lakini akazidhibiti hasira zake ila kihisia na kisaikolojia alikuwa amesononeka.

Huishi siku moja baada ya nyingine, kwani hana uhakika na maamuzi ambayo mumewe huenda akayafanya kesho. Kwake, licha ya Mungu kutopenda talaka, kuna mahali ndoa hufika inakosa maana.

Mtaalamu wa masuala ya kijinsia, Wangu Kanja kupitia wakfu wake wa Wangu Kanja anakiri kuwa mwaka wa 2020, wakfu wake ulishuhudia ongezeko la visa hivi vya dhuluma za kisaikolojia na za kihisia.

Hata hivyo, ongezeko hili lilisababishwa na watu kuwa nyumbani haswa wanaume ambao wengi wao hufika majumbani saa nane asubuhi na kutoka kunapokucha.

Kuwa katika mazingara haya mapya ya kukaa nyumbani mchana kutwa, usiku kucha kuliwafanya wengi kuvurugana huku wanandoa hawa kukosa kuzungumza na pia wao kutojua jinsi watakavyokabiliana na mazingara haya mapya kukisababisha ongezeko hili, anaongeza kusema Wangu

Hata hivyo, Wangu Kanja anaungama kuwa mahusiano mengi haswa ya kimapenzi yamejengwa kwenye misingi ya changarawe.

Mtaalamu wa masuala ya kijinsia Wangu Kanja. Picha/ Hisani

“Mwanamke kwa mfano anaolewa ili tu kuliondoa jicho la kuhukumiwa na jamii katika maisha yake au hata ili wanafamilia wake wasimlaumu. Hivi si vigezo vya ndoa ndiposa wakati ambapo janga la Corona lilikita kambi nchini, wanandoa wa aina hii walipaswa sasa kuzungumza mara kwa mara jambo ambalo lilisababisha dhuluma za aina hii.”

Isitoshe, Wangu Kanja anaamini kuwa njia ya kujiondoa katika mitego ya dhuluma yoyote ile inayofanyika kwa mwanadamu kwanza nikujijua. Anasema unapojijua, utaelewa fika mipaka yako na hutajihusisha na mambo yanayovuka mipaka hiyo.

Hata hivyo, anaelewa kuwa watu wengi hukaa kwenye ndoa zinazowadhuru kwa kuogopa kile jamii itasema na hata namna ya kuanzia upya. Lakini anauliza, je utakaa kwa ndoa hiyo ujiumize na hata uwaumize watoto wako ili tu jamii isiongee na kesho jamii iyo hiyo itakuwa na mada ya familia nyingine?

“Huduma za afya za kiakili si za watu walioruka vichwa pekee,” anasisitiza Bi Kanja. Utapata mtu aliyefutwa kazi akiwatolewa jamaa zake hasira ila wanafamilia hawa si vigezo vya kupata kazi nyingine.

Ni nini mtu anapaswa kufanya? Je mtu huyu anaweza kuenda kumwona mwanasaikolojia ili kupata suluhisho la kazi bila ya kuwatolea hasira jamaa zake?

Pili, watu wanapaswa kubadilisha maisha yao pindi tu mambo yamebadilika. Iwapo, umepigwa kalamu na ulikuwa unaishi kwa nyumba ya kifahari, inakubalika kuondoka katika nyumba hiyo na kutafuta nyumba yenye kodi ya chini, anasema Bi Kanja.

Mtaalamu wa masuala ya kiakili katika Chuo Kikuu cha Aga Khan, Profesa Lukoye Atwoli anasema kuwa hajui uratibu wa uenezi wa ongezeko la visa vya msongo wa mawazo haswa baina ya wanandoa sababu hakuna utafiti umefanywa ili kubaini.

Hata hivyo, anaeleza kuwa ukizuru hospitali kadhaa jijini Nairobi, utapata nusu ya idadi ya wagonjwa waliofika pale wanaugua msongo wa mawazo ila hawajui na asilimia 90% ya wanaojua hawajui jinsi ya kupata matibabu yatakayowafaa.

“Wanawake ndio huwa na hatari ya juu ya kupata ugonjwa huu kuliko wanaume,” akasema Profesa Lukoye. Hii ni sababu ya maumbile yao haswa ya kihomoni, misingi ya kijamii kwa mfano matarajio ya majukumu ya kijinsia, unyanyasaji katika mahusiano ya kimapenzi ambao sana sana unaegemezwa kwa matarajio ya jamii kwa mwanamke na mwishowe matukio aliyopitia mtu nyakati zake za utoto.

Watoto walioshuhudia mivutano majumbani kati ya wazazi ama watoto waliopigwa sana na wazazi wao huku wazazi hao wakiamini kuwa hiyo ndiyo njia ya kuwaadhibu huchangia sana namna mtu atakua na kuwa katika siku zake za usoni.

Mtaalamu wa masuala ya kiakili katika Chuo Kikuu cha Aga Khan, Profesa Lukoye Atwoli. Picha/ Hisani

Wasichana haswa, huwa na wakati mgumu kwani jamii imeamini kuwa rasilimali zikiwepo mtoto wa kiume ndiye wa kwanza kuzipata rasilimali hizi.

Profesa Lukoye anakiri kuwa “Watu ambao wapo kwenye mahusiano ya kimapenzi yenye ugumu, watu ambao hawana marafiki wanaowaeleza shida wanazopitia, watu wanaoishi kwenye umaskini na wanasumbuka na kina mama wajawazito ambao wana mimba inayotatiza ni baadhi ya watu walio kwenye hatari ya wakapata msongo wa mawazo baada ya kujifungua (Post Natal Depression).”

Hata hivyo, magonjwa haya ya msongo wa mawazo yanaweza kuzuiwa kwa kupima chembe chembe za maumbile au DNA. Pili, mtu kuhakikisha kuwa anakula lishe bora na anafanya mazoezi mara kwa mara.

Tatu, mwanamke mjamzito anapaswa kuhakikisha kuwa hatumii dawa zozote za kulevya na pia anamahusiano mazuri na wanajamii wenzake. Pia anapaswa kuwa na masomo ya msingi sana kwani yatamfaa akimlea na kumchunga mwanawe.

Kwa kuangazia masuala ya kitamaduni, Profesa Lukoye ni mwepesi wa kukiri kuwa mjadala kuhusu masuala ya afya ya kiakili yamebadilika lakini watu wenye matatizo ya kiakili wanakabiliwa na unyanyapaa wa jamii na wa mtu binafsi.

Profesa Lukoye anaeleza kuwa jinsi ya kukabiliana na unyanyapaa huu ni kuwapa watu maarifa, kuunda mawazo mazuri na kuwa na mikakati itakayowashurutisha watu kutosema na kufanya mambo yanayodunisha haki za watu wenye matatizo ya akili.

Kwa Mercy na Mary, safari ya kupata uponyaji ni ndefu kutokana na jamii ambayo haina ufahamu kuhusu matatizo ya akili kwa mujibu wa Profesa Lukoye.

You can share this post!

CORONA: Mombasa yapiga marufuku matibabu ya nyumbani

Dandora Youth FC yadhaminiwa kwa Sh2 milioni