• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
DINI: Furaha imo katika kumaliza kila unachopanga kufanya maishani

DINI: Furaha imo katika kumaliza kila unachopanga kufanya maishani

Na PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

FURAHA ni hitaji la kimsingi kwa binadamu sawa na tunavyohitaji kupumua hewa safi.

“Furaha ni sala, nguvu, upendo, na neti ya upendo ya kuvua watu,” alisema Mama Teresa wa Calcutta.

Furaha ina maeneo mengi ya kujificha.

Eneo mojawapo ni kumaliza vizuri. Unapoipenda kazi yako na kumaliza unachofanya, furaha ni matokeo.

Kuna furaha unapomaliza kuandika insha.

Kuna furaha unapomaliza chuo au shule. Kuna furaha unapomaliza kazi uliyoianza.

Paulo alifurahi na kuandika: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda” (2 Tm 4:7).

Paulo alimaliza vizuri.

Katika sala ambayo Askofu husali katika ibada ya upadrisho ni “Mungu akamilishe kazi aliyoianzisha.”

Mungu alipomaliza kazi ya uumbaji alifurahi na alistarehe: “Basi, mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimalizia kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba,” (Mwanzo 2: 1-2).

Yesu alimaliza kazi: “Nimeimaliza kazi,” (Luka 17-4).

Paulo alimaliza mwendo (2 Timotheo 4:7).

Ukisoma maneno hayo inasikika toni ya furaha.

Mfalme wa Kirumi Nero aliamrisha michezo ya Olimpiki ifanyike mwaka 67 BC. Alishiriki katika michezo akiwa katika matembezi ya muda mrefu huko Ugiriki.

Kwenye programu waliongeza mashindano ya muziki na mashairi.

Nero alishinda kila shindano alipoingia kushindana kupitia kitu kidogo.

Aliingia kwenye mashindano ya farasi akokotwaye na gari la kukokotea farasi. Alianguka kutoka kwenye gari likokotwalo na farasi. Hakufanya vizuri katika mashindano. Hakumaliza mwendo. Lakini majaji wa mchezo walimtangaza kuwa ameshinda.

Alirudi Italia akiwa amepanda kwenye gari la kukotwa na farasi.

Alizunguka Jiji la Roma akiwa amepanda gari alilopanda Augustus Caesar katika kuingia jijini kwa ushindi.

Alivaa taji la Olimpiki. Umati ulimshangilia lakini kichinichini palikuwepo na mnong’ono wa ushindi wa kiudhalilishaji kwani hakumaliza mwendo. Nero aliporudi kutoka Roma Paulo alitunga wosia wake, “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda” (2 Tm 4:7).

Paulo alimkejeli Nero ambaye hakumaliza mashindano lakini alitangazwa mshindi. Watu walimpa taarifa Nero. Baada ya jambo hilo hati ilisainiwa ya kumuua Paulo. Hilo halikumsumbua Paulo kwa sababu alijua amemaliza mwendo.

Dkt Robert Clinton alitoa sababu za Paulo kumaliza vizuri. Kwanza, Paulo aliendelea kukua. Alisahau ya nyuma mabaya na kuyaona kama taka. Alipigania lengo lake. Pili, lililomsaidia Paulo kufanikiwa ni ubia na watu. Alimshukuru Mungu alipowakumbuka wanamtandao. Tatu, alimtii Mungu. Ukimtii Mungu naye anatii ombi lako.

Saa moja kasoro dakika kumi, jioni yenye utulivu katika Jiji la Mexico mnamo 1968, mkimbiaji wa Tanzania kwa maumivu alichechemea kuingia kwenye Uwanja wa Olimpiki akiwa mtu wa mwisho kumaliza marathon.

Uwanja wa michezo ulikuwa kwa kiasi fulani mtupu na mkimbiaji kutoka Tanzania peke yake, mguu ukiwa na bandeji, alijitahidi kuzunguka na kuingia kwenye mstari wa kumaliza.

Alipoulizwa kwa nini alijitahidi kwa shida kumaliza, kijana huyo kutoka Tanzania alijibu kwa upole: “Nchi yangu haijanituma maili 9,000 kuanza mashindano.”

Maliza unachokianza. Ukianza kujenga nyumba, maliza. Ukianza kuchumbia, maliza. Ukianza kulima shamba, maliza. Ukianza masomo ya shahada, maliza. Ukianza mradi, maliza. Ukianza kumeza dozi, maliza. Furaha inakuwa katika kumaliza bali sio katika kuanza.

You can share this post!

Mzozo wa Kalonzo, Mudavadi watishia kutawanya OKA

TAHARIRI: Shule zisiwafukuze wanafunzi kiholela