• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Mzozo wa Kalonzo, Mudavadi watishia kutawanya OKA

Mzozo wa Kalonzo, Mudavadi watishia kutawanya OKA

Na IBRAHIM ORUKO

MGAWANYIKO umezuka ndani ya Muungano wa One Kenya Alliance (OKA), kati ya kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Wiper, Kalonzo Musyoka.

Tofauti hizo zimeibuka kuhusiana na mbinu ya kukabiliana na mwenzao wa ODM, Raila Oding kwenye uchaguzi wa 2022.

Licha ya wanasiasa hao wawili kutangaza kuwa wanalenga kuwania urais, msimamo wa Rais Uhuru Kenyatta wa kumpendelea Bw Odinga umeonekana kusambaratisha mikakati yao.

Pia imedokezwa kuwa Seneta wa Baringo, Gideon Moi ambaye ni mshirika wao katika OKA, anampendelea Bw Odinga, jambo linalotatiza Bw Musyoka na Bw Mudavadi.

Huku wawili hao wakiendelea kulumbana kila mmoja wao akidai atapeperusha bendera ya OKA, kuingia kwa aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo ndani ya muungano huo kumewafanya wajikune vichwa zaidi.

Washirika wa wanasiasa hao wawili, ambao wamewahi kuwa makamu rais, sasa wanashukiana kiasi kwamba wamekuwa wakilaumiana kuhusu mwelekeo ambao OKA inafaa kuchukua kabla ya 2022.

Taifa Jumapili imebaini kuwa tatizo la Bw Mudavadi na Bw Musyoka ni kuwa wanahisi kuwa muungano huo ni wao, na hivyo ndio wanafaa kutoa mwelekeo wa kisiasa kuhusu masuala ya ndani kuliko Seneta Moi na Kinara wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula.

Mrengo wa Bw Mudavadi unasema kuwa unashuku Bw Musyoka yupo njiani kutoroka OKA, na kama tahadhari umeanza kuvumisha muungano mpya kwa jina Kenya Kwanza Alliance ambao kiongozi huyo wa ANC analenga kutumia kujipigia debe.

“Mudavadi atakuwa debeni liwalo na liwe hata kama hiyo inamaanisha atapuuza msimamo wa Uhuru,” akasema mwandani mmoja wa Bw Mudavadi.

Wandani wa Bw Mudavadi wamemkashifu Bw Musyoka kwa kukataa kuwapa wanachama wengine stakabadhi zilizotumika kusajili OKA wakati ambapo anaonekana kutotilia maanani masuala ya muungano huo.

“Hajakuwa akiitisha mikutano au kuhudhuria ile ambayo huandaliwa,” akaongeza mwandani huyo.

Nao wandani wa Bw Musyoka wanadai kiongozi wao ana udhibiti wa ngome yake ya Ukambani kuliko Bw Mudavadi anavyodhibiti Magharibi, na ndiyo maana wanapendelea apeperushe bendera ya OKA.

Mrengo wa Bw Mudavadi pia haujafurahishwa na kuingizwa kwa Bw Jirongo ndani ya OKA wakidai anasukumwa na Bw Moi na Musyoka ili kudidimiza uwezekano wa kinara huyo wa ANC kuwania urais.

“Mimi sasa ni mmoja wa vinara wa OKA nikiwakilisha chama changu cha UDP,” akasema Bw Jirongo ambaye hata alihutubu wakati wa Kongamano la Wajumbe wa Kanu lililoidhinisha Bw Moi kuwania kiti cha urais wiki jana.

Aidha mbunge huyo wa zamani wa Lugari amekuwa akiandamana na Bw Moi katika hafla mbalimbali ikiwemo juzi alipomtembelea mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria hospitalini.

You can share this post!

UNESCO kufanya ushirikiano na vyuo vikuu viwili nchini

DINI: Furaha imo katika kumaliza kila unachopanga kufanya...