• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
DINI: Kuna njaa za aina nyingi ila zipo za lazima zinazohitaji Mungu pekee

DINI: Kuna njaa za aina nyingi ila zipo za lazima zinazohitaji Mungu pekee

Na FAUSTIN KAMUGISHA

NJAA zetu ni za aina nyingi.

Tuna njaa ya Mungu. Tuna njaa ya kujua maana. Tuna njaa ya kueleweka. Tuna njaa ya kukubalika.

Tuna njaa ya shukrani. Tuna njaa ya mahusiano mazuri. Tuna njaa ya kutiwa moyo. Tuna njaa ya matumaini. Tuna njaa ya imani. Tuna njaa ya upendo. Tuna njaa ya neema. Tuna njaa ya miujiza. Tuna njaa ya uzima wa milele.

“Njaa ya chaguo ni anasa inayoumiza. Njaa ya ulazima ni maumivu makali yanayoogofya,” alisema Mike Mullin.

Njaa ya Mungu ni njaa ya lazima. Njaa ya upendo ni njaa ya lazima. Njaa ya maana ni njaa ya lazima. Njaa ya imani ni njaa ya lazima. Mtu mwenye njaa akiwa amelala anaota chakula, chembe ya mkate kwake ni sikukuu. Waliomtafuta Yesu walikuwa na njaa.

“Amin, amin, nawaambieni, ninyi mnanitafuta si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.” ( Yohane 6: 26).

Kuna njaa ya Mungu. Unaweza kufanya mengi kwa saa moja pamoja na Mungu kuliko maisha yote bila Mungu.

“Kwa Mungu yote yawezekana” (Mathayo 19: 26). Mungu tosha. Mt. Augustino alikuwa na njaa ya Mungu. Alisema, “Ee Mungu umetutuma kwa ajili yako hatutulii mpaka tutakapotulia katika wewe.”

Tunasoma katika Biblia, “Mkutano wote wa wana wa Israeli wakawanung’unikia Musa na Haruni huko jangwani. Wana wa Israeli wakawaambia, “Afadhali tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, tulipoketi kwenye sufuria za nyama, tukala mkate tukashiba! Ninyi mmetuleta jangwani ili mpate kutuua kwa njaa mkutano huu wote” (Kutoka 16:2-3).

Baada ya majina sita, magumu ya jangwani yalianza kubadili misimamo ya Waisraeli. Waisraeli walianza kulalamika, macho yao yalichungulia sufuria za nyama za Misri kuliko kuchungulia Nchi ya Ahadi.

Habari za zawadi ya Mungu za kwale na manna zilisaidia zaidi kuonesha majaliwa ya Mungu jangwani. Maana haikuwa zawadi ya Musa.

Alikuwa Bwana aliyetoa chakula hiki kwa ajili ya Israeli. Mungu hakutuliza tu njaa ya chakula hata njaa ya Mungu. Kuna njaa ya maana. Mioyo yetu ina njaa ya kujua kwa nini? Kwa nini mimi? Kwa nini mambo mabaya huwapata watu wema? Bila shaka wana wa Israeli walitaka kujua kwa nini wanapata masumbuko hayo.

Niliwahi kuona katuni juu ya Waisraeli baada ya kupitia miaka mingi ya vita na mashambulio ya waliowazunguka.

Mwisraeli mmoja alisema, “Kama hii ndiyo maana ya kuwa taifa teule la Mungu afadhali Mungu ateue wengine kama Waitaliano au Wajerumani. Kuna kuhangaika kutafuta maana ya matukio.”

“Mioyo yetu haina njaa ya sifa, raha, mali au mamlaka. Thawabu hizo husababisha matatizo mengi kama zinavyoyatatua. Mioyo yetu ina njaa ya maana,” alisema Harold Kushner katika kitabu chake ‘When All You’ve Ever Wanted Isn’t Enough’.

Wana wa Israeli waliponung’unika hawakujua maana. Walikuwa na njaa ya maana. Mateso unayoyapata yape maana. Shida unazozipata zipe maana. Matatizo unayoyapata yatafutie maana.

“Kwa namna moja mateso yanakoma kuwa mateso wakati yanapata maana, kama maana ya sadaka,” aliandika Victor E Frankl katika kitabu chake ‘Man’s Search for Meaning’.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali isuluhishe uhaba wa walimu

‘Malenga Msafiri’ ni dereva wa masafa marefu ila...