• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
‘Malenga Msafiri’ ni dereva wa masafa marefu ila hakosi pia kutunga mashairi

‘Malenga Msafiri’ ni dereva wa masafa marefu ila hakosi pia kutunga mashairi

Na HASSAN MUCHAI

FRANK Orina anayetumia lakabu ‘Malenga Msafiri’ ni msafiri kweli.

Ni dereva wa magari ya uchukuzi na daima amekuwa barabarani kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Mombasa hadi mataifa jirani ya Uganda, Rwanda, DRC, Tanzania, Sudan na hata Burundi.

Frank ni mzaliwa wa kijiji cha Matongo (Gekonge), tarafa ya Nyamusi, Kaunti ya Nyamira na mtoto wa pili katika familia ya watoto sita wa Mzee Edison Omwenga na Bi Penina Bosibori.

Malenga Msafiri alipata masomo yake ya msingi kupitia shule mbali mbali kutokana na uhamisho wa mara kwa mara wa baba yake aliyekuwa akifanya kazi ya utabibu.

Baadhi ya shule hizo ni Kerenga, Kericho Headquarters, Migaa, Chagaik na Kericho Township kabla ya kuingia ya Matongo Boys kwa masomo ya upili.

Ingawa ndoto yake ilikuwa kuwa mhasibu kutokana na elimu ya kitaaluma aliyopata kupitia chuo kimoja mjini Kisumu, Orina alijaliwa kuwa dereva wa magari ya uchukuzi, kazi ambayo anasema amekuwa akiifanya kwa muda.

Kwa sasa ameajiriwa na kampuni ya Transpares Long Distance Hauliers jijini Mombasa.

Uhusiano wake na Kiswahili ulitokana na malezi yake kwani alikuwa mwepesi kutoa hoja akitumia lugha hii.

Akiwa shuleni alishiriki makongamano mengi na mashindano ya kuchemsha bongo yaliyokuwa yakiendeshwa kupitia idhaa ya KBC na marehemu Said Karama.

Hata hivyo, aliyemchochea sana kujitoma katika ushairi ni marehemu Abdalah Mwasimba aliyekuwa mghani hodari wa mashairi.

Sauti yake Mwasimba ilimfanya mshairi wetu kuzidi kukipenda Kiswahili na hata kutaka kutunga mashairi.

Aliboresha upeo wake kwa kusoma vitabu vya riwaya na hadithi fupi. Alitunga shairi lake la kwanza akiwa Matongo Kidato cha Kwanza 1992, shairi ambalo alilikariri mbele ya tamasha ya sikukuu ya mashindano ya nyimbo kwa mada ‘Kipi cha Kumpa Mama?’

Alikuwa akitoa onyo kwa wanaomtelekeza mama bila kujali kazi kubwa ya ulezi anayoifanya.

Ingawa shairi hilo halikuvuma jinsi alivyotaka, Orina hakufa tamaa.

Aliendelea kuandika hadi alipokutana na mshairi Nyagemi Nyamwaro Mabuka ‘Malenga wa Migombani’ mwaka wa 2010 na kumsajili kwenye makundi mbali mbali ya wakeretekwa wa lugha mathalan kisima cha mashairi.

Aliwaandama magwiji wengine kama vile, Masito Ali, Mohamed Bakari, Mzee Kijaluba, Hamisi Kisamvu, Rashid Mwachinyebwe, Mfaume Hamisi, Lilian Alividsa, Gilbert Kinara, Moses Chesire, Mwanaisha Salim, Sara Fina, Moshi wa Koko Badi, Martha Sheeri, Jibril Adams na wengine wengi.

Shairi lake la kwanza kuchapishwa Taifa Leo lilikuwa ‘Kilio Changu Sikia’.

Shairi hili la beti sita lilikuwa ombi kwa Mungu kuwahifadhi mayatima dhidi ya madhila ya ulimwengu.

Haki zangu waninyima, bure wanidalilisha,

Chema changu chawauma, na mili kuwakondesha,

Urithi wangu ‘mechuma, ndoto wamenikatisha,

Mungu wangu ninalia, kilio changu sikia.

 

Nakosa tonge yatima, wala sioni mlisha,

Mie nala mchelema, nanywa visotamanisha,

Nashindwa simama wima, njaa yanitepetesha,

Mungu wangu ninalia, kilio changu sikia.

Hadi sasa ametunga mashairi 200, mengi yakiwa ya muundo wa tarbia.

Mbali na Taifa Leo, ametunga na kupachika mengine kupitia mitandao ya kijamii.

Pia amehifadhi mengine akiwa na lengo la kuchapisha diwani yake siku za usoni.

Kupitia ushairi amepata faida lukuki. Amekutana na marafiki wengine na kujifunza mengi kuhusu Kiswahili.

Orina ambaye kujisifu anasema hivi;

 

Niandikapo Napanga, mwishowe ninapangua,

Maneno naunga unga, nashindwa kuendelea,

Nabananga nikitunga, maneno yatokomea,

Japo kutunga natunga, bado natunga visivyo.

 

Changamoto kubwa anayokumbana nayo ni kupata muda wa kutosha kutunga kutokana na kazi nyingi na safari zinazomkodolea macho.

You can share this post!

DINI: Kuna njaa za aina nyingi ila zipo za lazima...

JAMVI: Ruto kukabiliwa na mtihani mkali 2022 bila ya...