• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
DINI: Mfumo mzima wa maisha ni orodha, andaa yako pia!

DINI: Mfumo mzima wa maisha ni orodha, andaa yako pia!

NA PADRE FAUSTINE KAMUGISHA

MAISHA ni orodha.

Kuna orodha ya vipaumbele. Kuna orodha ya matendo ya huruma. Kuna orodha ya amri za Mungu. Kuna orodha ya mashujaa wa taifa. Kuna orodha ya waliochaguliwa. Kuna orodha ya watakatifu. Kuna orodha ya wachangiaji. Kuna orodha ya wadaiwa sugu. Kuna hadithi ya mtu aliyeaga dunia na Kwenda mbinguni.

Kwenye mlango wa mbingu alimkuta Mt. Petro akiwa na orodha ya watu wa kuingia mbinguni.

Mtakatifu Petro alipoangalia kwenye orodha hakuona jina la mtu huyo. Mtu huyo alimuomba Mtakatifu Petro atazame kwenye orodha ya watu wa Kwenda toharani. Mtakatifu Petro hakuliona jina lake. Hatimaye alimwambia, “Utaenda motoni.” Mtu huyo alisema, “Kwa nini niende motoni, sikufanya lolote.”

Mt. Petro alimwambia kwa kuwa hukufanya lolote utaenda motoni. Kuwa na orodha ya matendo ya huruma. Haitoshi kuwa na orodha fanya, tenda, timiza na tekeleza. Kuna orodha ya mambo ya kufanya kila siku.

“Kila siku nitatimiza jambo moja kwenye orodha yangu ya mambo ya kufanya,” alisema Lailah Gifty Akita. Kuna orodha ya nipe nikupe. Bwana wetu Yesu Kristu alipinga orodha ya nipe nikupe.

“Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, ‘Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako tajiri; ukifanya hivyo wao nao watakualika kwao na hivyo utakuwa umelipwa kwa kuwaalika. Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu; nawe utapata baraka kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa” (Luka 14: 12-14).

Kuwa na orodha ya watu ambao hawatakulipa. Mt. Irenaeus wa Lyons alikuwa na haya ya kusema, “Waalike vilema, vipofu na maskini na utabarikiwa, kwa vile hawawezi kukulipa, lakini utalipwa wakati wa ufufuko.” (Mathayo 5:46)

Kuna orodha ambayo haina ubaguzi. Sherehe zinatutenga. Harusi zinatutenga. Misiba haitubagui. Bwana wetu Yesu Kristu alipinga orodha yenye ubaguzi. Alipendekeza orodha ambayo inawahusisha maskini, vilema, viwete, vipofu.

Mtakatifu Yohane Krosostomu alisema, “Lakini unasema maskini sio msafi ni mchafu. Muoshe na mfanye akae mezani pamoja na wewe. Kama ana nguo chafu mpe mpya. Kristu anakuja kwako kupitia yeye.”

Kuna hadithi juu ya tajiri aliyetembelewa na maskini. Tajiri huyo alimletea chakula barazani. Alimwambia wasali sala ya Baba Yetu. Walipoanza kusali maskini alisema, “Baba yako aliye mbinguni…” Tajiri alimkosoa na kusema, “Sema Baba Yetu aliye mbinguni.” Maskini alisema, “Kama unajua ni Baba Yetu usingeniweka barazani ungenikaribisha ndani ya nyumba.” Sala ya Baba Yetu haina ubaguzi. Sote tuko kwenye neno “Yetu.”

Katika ratiba kuna vipengele vya tukio, wahusika. Kwa Yesu chakula ni wote. Tendo la upendo ni wote. Huruma ni wote. Zaka ni wote. Sadaka ni wote. Ujenzi wa kanisa ni wote. Sensa ni wote. Hata Yozefu na Maria walienda kuhesabiwa.

Kuna orodha ya unyenyekevu. Kuna orodha inaitwa Orodha ya Mama Teresa wa Calcutta ya Unyenyekevu. Alisema, “Unyenyekevu ni mama wa fadhila zote; usafi wa moyo, upendo na utii. Ni katika kuwa wanyenyekevu upendo unakuwa halisi, mwenye ibada. Kama uko mnyenyekevu hakuna kitu kitakuchanganya iwe kusifiwa au kuaibishwa. Ukilaumiwa hautakata tamaa. Ukiitwa mtakatifu hautajiweka kwenye kinara.”

Zingatia orodha ya unyenyekevu. Kuwa na orodha ya mashujaa wako yaani kundi rejea. Ni orodha ya watu wa kukuinua. Mfalme Daudi alikuwa na orodha ya mashujaa, orodha ya wawezeshaji si wakwamishaji.

“Hii ndiyo orodha ya wakuu wa mashujaa wa Daudi, ambao pamoja na watu wengine wote wa Israeli, walimuunga mkono kwa pamoja ili awe mfalme, sawa na neno la Mwenyezi Mungu-Mungu alilotoa juu ya Waisraeli” (1 Mambo ya Nyakati 11:10).

Kuwa pia na orodha ya vipaumbele: Mungu kwanza, familia na kazi na mambo mengine.

“Kutoa katika orodha ya vipaumbele ni muhimu kama kuongeza,” alsema Frank Sonnenberg.

Lakini usimtoe Mungu katika orodha ya vipaumbele. Usiitoe familia katika orodha ya vipaumbele.

Kuwa na orodha pia ya mtu gani uwe: mnyenyekevu, mwaminifu, mtiifu, mwenye huruma. Tengeneza orodha ya kufanya na ya kuwa.

  • Tags

You can share this post!

WALIOBOBEA: Nyota ya Kituyi ilianza kung’aa akiwa chuoni

KIGODA CHA PWANI: Yaelekea PAA haijatosha kuwa sauti ya...

T L