• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
KIGODA CHA PWANI: Yaelekea PAA haijatosha kuwa sauti ya Wapwani

KIGODA CHA PWANI: Yaelekea PAA haijatosha kuwa sauti ya Wapwani

NA PHILIP MUYANGA

JE chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kimeweza kutimiza matarajio ya kuwa chama chenye ushawishi mkubwa wa kisiasa katika ukanda wa Pwani hususan baada ya uchaguzi wa Agosti 9 kumalizika?

Swali hili limo vinywani mwa wakazi wa Pwani kwani wakati kilipoanzishwa kilijitwika jukumu la kuwa chombo cha cha kisiasa cha kuunganisha wapwani katika kaunti zote sita za ukanda huo.

Chama hicho cha PAA pia kilionekana kuwa kitakita mizizi na kuwa na ushawishi mkubwa nje ya ukanda wa Pwani na kupigania mahitaji ya wapwani kitaifa.

Viti vitatu vya ubunge

Hata hivyo kumekuwa na shauku kubwa baada ya uchaguzi wa Agosti 9 kwani chama cha PAA kiliweza kupata viti vitatu pekee vya ubunge na zaidi ya kumi na vitano vya uwakilishi katika bunge za kaunti.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, idadi hiyo ya walioshinda viti hivyo ni chache mno kuweza kukifanya chama cha PAA kuwa na usemi mkuu wa kisiasa eneo la Pwani.

Hii ni kwa sababu matokeo ya uchaguzi yameenda kinyume na matarajio ya wakaazi wengi wa ukanda wa Pwani waliokiona chama hicho kama suluhisho la matatizo ya kisiasa.

Suala hili linatiliwa mkazo kwa kuwa kumekuwepo na vyama vingine vyenye chimbuko la ukanda wa Pwani ambavyo havijakuwa na ushawishi mkubwa na huonekana kuchipuka tu wakati wa uchaguzi mkuu unapowadia.

Chama cha PAA kilichoanzishwa takriban mwaka mmoja uliopita kiliweza kujinyakulia viti vya ubunge vya Kinango (Gonzi Rai), Rabai (Anthony Mupe) na Ganze (Ken Charo).

Katika mojawapo ya mikutano ya kisiasa ya hapo awali,aliyekuwa gavana wa Kilifi Amason Kingi ambaye ni kiongozi wa chama hicho alinukuliwa akisema kuwa PAA ndio chanzo cha safari ya eneo la Pwani kuelekea ikulu ya urais mwaka wa 2027.

“Chama cha PAA kitawasilisha wagombeaji viti kwa kila nyadhifa (mwaka wa 2022) na mwaka wa 2027 ni ikulu, faida ya PAA haiji kwangu,inakuja kwa wananchi,” alisema Bw Kingi wakati huo.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa za kitaifa Bi Maimuna Mwidau, chama cha PAA kina uwezo mkubwa wa kuwa chama chenye ushawishi mkubwa eneo la Pwani iwapo kitakuwa na uongozi bora.

“Chama hicho kinaonekana kusimama na malengo bora na kitakuwa na usemi mkuu iwapo kitakuwa na uongozi thabiti,” alisema Bi Mwidau.

Bi Mwidau alisema kuwa chama cha kisiasa kikihusishwa na kiongozi ambaye hakubaliki basi hakitaendelea na ni jambo la busara iwapo chama hakibinafsishwi.

Alisema kuwa chama cha PAA kina malengo mazuri ambayo yatawafaa wananchi iwapo wataelezewa kuyahusu mapema.

“Kwa sasa ukanda wa Pwani utazidi kusubiri kuwepo kwa chama kitakachowasilisha maswala yake katika ulingo wa kitaifa kwani baadhi ya viongozi hawaoni faida ya umoja wa kisiasa wa ukanda wa Pwani,” alisema Bi Maimuna.

Mchanganuzi wa siasa Bw Mndwanmrombo Mwakera alisema kuwa iwapo Bw Kingi angebaki katika muungano wa chama cha Azimio One Kenya, chama cha PAA kingezoa viti vingi kuliko ilivyozoa katika ukanda wa Pwani.

Bw Mwakera alisema kuwa, kiongozi huyo wa PAA anaweza kujipiga kifua kisiasa kwa sasa kwa kusema kuwa idadi ya viti chama hicho imechukua kwa mara ya kwanza si mbaya na idadi hiyo imekiweka katika ngazi ya juu ya siasa za kitaifa.

“Kilipoundwa miezi kadhaa kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, PAA kilikuwa chama kilichoundwa kwa madhumuni ya kuwa safina ya wapwani katika kudai uwepo wake kwenye siasa za kitaifa,” alisema Bw Mwakera.

Hata hivyo Bw Mwakera aliongeza kusema kuwa iwapo ushindi wa viti hivyo vitatu vya chama cha PAA na ule wa wawakilishi wa bunge za kaunti hautapaliliwa vizuri, basi yale yaliovifika vyama vingine ambavyo chimbuko lake ni Pwani yatafikia pia chama cha PAA.

“Chama cha PAA kinaweza kujizatiti na kuinuka na kuendelea na malengo ya umoja wa kisiasa wa Pwani iwapo kitatoa ubinasfi wa wasimamizi wake,” alisema Bw Mwakera.

Uongozi

Baadhi ya wandani wa chama cha PAA ambao hawakutaka kutajwa, walidai kuwa uongozi wa chama hicho ndio umekifanya kutozoa viti vingi katika ukanda wa Pwani na kuendeleza ndoto ya umoja wa kisiasa wa Pwani.

“Wagombea viti walikuwa wasaidiwe katika kampeni zao kwa hali na mali, lakini walipopewa vyeti vya kugombea viti waliwachwa peke yao ndiposa wengi hawakufaulu,” alidai mmoja wa wandani wa chama hicho.

Aliongeza kudai kuwa chama cha PAA kilikuwa kimewapatia wananchi na wagombea wengi matumaini ya kubadilisha siasa za Pwani lakini ubinasfi ulikithiri kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama ndiposa hakikufanya vizuri katika uchaguzi wa Agosti 9.

Kando na chama cha PAA, kumekuwa na vyama vingine ambavyo asili yake ni ukanda wa Pwani lakini havijaweza kuwa na msisimko mkubwa wa kisiasa.

Hata hivyo,baadhi ya wachanganuzi wa siasa wamedai kuwa wapiga kura eneo la Pwani wameshindwa kuvipigia debe vyama vya asili ya Pwani na kuwapigia kura watu wao ndiposa vyama hivyo havionekani kuwa na ushawishi.

Wachanganuzi hao wanasema kuwa wapiga kura ni wa kujilaumu wenyewe kwa kuwa wanawasukuma viongozi wao kwa vyama vingine.

  • Tags

You can share this post!

DINI: Mfumo mzima wa maisha ni orodha, andaa yako pia!

MIKIMBIO YA SIASA: Weta acheza pata potea

T L