• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
WALIOBOBEA: Nyota ya Kituyi ilianza kung’aa akiwa chuoni

WALIOBOBEA: Nyota ya Kituyi ilianza kung’aa akiwa chuoni

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

JINSI kijana Daudi alivyomuangusha Goliath kwa vipande vitano vya mawe huku waliotazama wakikosa kuamini, ndivyo ilivyokuwa kwa “Daudi” kutoka Kimilili aliyeangusha mbabe wa kisiasa, sio kwa vipande vya mawe, lakini kwa tsibili tsibili, alama ya vidole viwili vya kuonyesha siasa za vyama vingi.

Jina lake lilikuwa Mukhisa Kituyi. Mwanasisasa huyo aliyezaliwa na kulelewa katika wilaya ya Magharibi ya Kenya ya Bungoma, sasa kaunti ya Bungoma, alikuwa amesomea Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na Norway na kufanya kazi na mashirika kama Christian Michelsen Institute ya Norway na Norwegian Agency for International Development (NORAD).

Lakini siasa ilikuwa katika damu yake na alikuwa akisubiriwa kujibwaga uwanjani.

Akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Forum for the Restoration of Democracy (FORD), alikuwa katika uongozi wa chama kilichoanzisha vyama vingine katika Kenya.

Chama hicho kilipovunjika mara mbili (FORD Kenya chini ya Jaramogi Oginga Odinga na Ford Asili ya Kenneth Matiba mwaka wa 1992), Kituyi alijiunga na Bw Odinga na baadaye mwaka huo akashinda kiti cha ubunge cha Kimilili akimbwaga Bw Elijah Mwangale, mwanasiasa aliyekuwa na uzoefu wa miaka mingi ambaye alikuwa mbunge kwa miaka 23 na kusimamia wizara nne: Leba, Utalii na Wanyama Pori, Mashauri ya Kigeni na Kilimo.

Kituyi alikuwa akikaribia kutimiza umri wa miaka 40 alipomshinda Mwangale na kuanza kuhudumu kwa muhula wa kwanza kati ya mihula mitatu aliyokuwa mbunge wa Kimilili.

Ni akihudumu muhula wa tatu akiwa mbunge ambao ulisadifiana na serikali ya Rais Mwai Kibaki. Wakati huo alikuwa amejiunga na chama cha Kibaki cha National Rainbow Coalition-Kenya (NARC-Kenya) na kuchaguliwa mbunge wa Kimilili. Kibaki alimteua waziri wa biashara na viwanda.

Akiwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi alikokuwa akisomea sayansi ya siasa na masuala ya uhusiano wa kimataifa, Kituyi alifukuzwa mwaka wa 1979 kwa sababu ya siasa.

Mwaka uliotangula, Prof Ngugi wa Thiong’o, aliyesimamia idara ya fasihi katika chuo hicho alikuwa ametupwa kizuizini kwa sababu ya mchezo wake wa kuigiza, Ngaahika Ndeenda. Wanafunzi walizua ghasia na serikali ikapiga marufuku chama cha wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi (SONU) na kutwaa pasipoti za wahadhiri kama Mukaru Ng’ang’a, Micere Mugo, Anyang’ Nyong’o na Okoth Ogendo.

Kituyi alipofukuzwa chuoni, alisajiliwa katika chuo kikuu cha kikuu cha Makerere kukamilisha masomo yake kwa mwaka mmoja.

Ingawa aliteuliwa waziri wa biashara na viwanda wakati uchumi ulikuwa umedorora Kituyi hakuvunja moyo Wakenya kwa muda aliohudumu.

Waziri wake msaidizi alikuwa Petkay Miriti huku Margaret Chemengich akiwa katibu wa wizara.

Waziri msaidizi wa Biashara Abdirahman Ali Hassan alijiunga nao 2005 Baraza la Mawaziri lilipofanyiwa mabadiliko.Kituyi alipoteza kiti chake cha ubunge kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 lakini nyota yake ikaendelea kung’aa kwingine.

Kwa miaka minne iliyofuatia, alikuwa miongoni mwa wataalamu walioshauri Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alikuwa mshauri wa Muungano wa Afrika kwa mwaka mmoja kuhusu masuala ya biashara huru barani Afrika na mwaka wa 2012 akateuliwa Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo (UNCTAD) wadhifa alioanza kutekeleza rasmi 2013.

You can share this post!

Maguire aambiwa unahodha hautampa uhakika wa kuunga kikosi...

DINI: Mfumo mzima wa maisha ni orodha, andaa yako pia!

T L