• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Real Madrid wazamisha Liverpool na kunyanyua taji la UEFA kwa mara ya 14

Real Madrid wazamisha Liverpool na kunyanyua taji la UEFA kwa mara ya 14

Na MASHIRIKA

MATUMAINI ya Liverpool kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya saba katika historia yalizimwa na fowadi Vinicius Jr aliyefungia Real Madrid bao la pekee katika ushindi wa 1-0 mnamo Jumamosi usiku jijini Paris, Ufaransa.

Liverpool walipoteza nafasi nyingi za wazi huku makombora ya washambuliaji wao yakipanguliwa na kudhibitiwa vilivyo na kipa Thibaut Courtois aliyefanya kazi ya ziada katikati ya michuma ya Real.

Mohamed Salah, aliyelenga kulipiza kisasi baada ya kujeruhiwa mapema kwenye fainali iliyokutanisha Liverpool na Real mnamo 2018, alishuhudia fataki zake sita zikipanguliwa na Courtois aliyetawazwa mchezaji bora wa kipute hicho cha Jumamosi.

Ushindi wa Real ambao sasa wamenyanyua taji la UEFA mara 14 katika historia, unafanya mkufunzi wao Carlo Ancelotti kuwa kocha wa kwanza kuwahi kunyanyua mataji manne ya kivumbi hicho cha haiba kubwa zaidi katika soka ya bara Ulaya.

Real waliovizia Liverpool kwa muda mrefu katika kipindi cha pili, walifungiwa bao na Vinicius katika dakika ya 59.

Fainali ya Jumapili ilishuhudia visa vya fujo na vurugu tele nje ya uwanja wa Stade de France huku maelfu ya mashabiki wa Liverpool, baadhi wakirashiwa maji yenye pilipili kutoka kwa maafisa wa polisi nchini Ufaransa, wakizuiliwa kuingia ugani. Tukio hilo lilisababisha mechi kucheleweshwa kwa zaidi ya dakika 30.

Liverpool waliojivunia kampeni za kuridhisha zaidi, walikamilisha msimu huu kwa mataji mawili – Carabao Cup na Kombe la FA – ambayo walinyanyua baada ya kupepeta Chelsea kupitia penalti.

Hata hivyo, mwisho wa kampeni za msimu huu ulikuwa wa kusikitisha ikizingatiwa kwamba walipoteza fursa maridhawa za kujizolea mataji mawili makuu zaidi – Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na UEFA katika wiki ya mwisho.

Ushindi wa taji la UEFA ungeyeyushia Liverpool machungu ya kutotwaa taji la EPL ambalo Man-City walilinyanyua baada ya kutia kapuni alama 93, moja pekee kuliko Liverpool walioambulia nafasi ya pili.

Licha ya kuanza kampeni zao za UEFA kwa utepetevu mkubwa muhula huu, Real walijinyanyua upesi na kudengua Paris St- Germain, Chelsea na Manchester City kabla ya kuzamisha chombo cha Liverpool.

Real walikamilisha kampeni zao za muhula huu kwa mataji mawili. Walinyanyua pia ubingwa wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) chini ya kocha Ancelotti aliyerejea ugani Santiago Bernabeu mwaka mmoja uliopita baada ya kuagana na Everton.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

DINI: Siri ya kufungua milango iliyofungika

Wapinzani watoa habari za uongo kunivuruga – Kidero

T L