• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:55 AM
DINI: Ukianguka, okota kitu; okota funzo muhimu

DINI: Ukianguka, okota kitu; okota funzo muhimu

NA PADRE FAUSTINE KAMUGISHA

KUSHINDWA sio neno la mwisho. Walt Disney (1901 – 1960) mzaliwa wa Marekani alifukuzwa kwenye kampuni ya magazeti kwa kutokuwa na “ubunifu wa kutosha.”

Alianzisha kampuni ambayo ilishindwa na baadaye alianza kampuni iliyobeba jina lake iliyofanikiwa. Alikuwa mtengenezaji filamu na mvumbuzi katika filamu. Aliokota somo la kuwa mbunifu.

Tunasoma katika Biblia, “Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru kwangu (Mika 7:8). Unapoanguka Bwana anakuwa nuru ya kukumulikia somo. Litafute. Kifutio kiligunnduliwa kwa sababu moja kutenda kosa ni jambo la kibinadamu. Makosa yanasamehewa, ukitubu.

Steve Jobs alifukuzwa katika kampuni aliyoianzisha na kurudi tena mwaka 1996. Alirudi akiwa na mawazo mapya ya kupunguza mambo ambayo kampuni ilikuwa inayafanyia kazi ili kuzalisha. Alipoanguka aliokota somo la kupunguza.

Mtakatifu Simon Petro alikuwa mtu wa karibu wa Yesu. Lakini alimkana Yesu. Alimkana mara tatu. Alianguka. Kwa nini alianguka guru wa uongozi Dkt John C. Maxwell anatoa sababu tatu: Alijiweka kiroho juu ya wengine, alifikiri anajijua vizuri kuliko Yesu anavyomjua na tatu alijihisi ana nguvu kuliko alivyokuwa. Lakini matumaini hayakupotea mwishoni Mtakatifu Simon Petro aliagukia mbele. Alikabili kushindwa kwake alitubu kwa kulia machozi, alikutana na Yesu na kupata matumaini. Aliokota somo: kuwa na matumaini yaani kutokukakata tamaa, kutubu na kumgeukia Mungu. Alifanya kitu kwa ajili ya wengine. Aliwaimarisha katika Imani.

“Ukiangukia uso bado unaenda mbele,” alisema Victor Kiam.

Mfame Daudi baada ya kuanguka na kutenda dhambi na mke wa mtu. Angalisho, mke wa mtu ni sumu. Lakini Mfalme Daudi, alitubu. Aliamua kuokota somo. Aliamua kufanya kitu kwa ajili ya wengine.

Alimwambia Mwenyezi Mungu, “Nitawafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watarejea kwako” (Zaburi 51: 13). Aliamua kuwa somo kwa wengine.

Kuna ambao wamekuwa walevi. Lakini baada ya kuacha ulevi wamewafundisha walevi njia za Mungu. Kuwa somo kwa wengine.

Mchungaji Levi Lusko alielezea hadithi jinsi yeye na binti yake Clover walivyokuwa wanaokota maganda ya wanyama wa baharini. Baba yake aliokota mazuri tu. Binti yake aliokota yale ambayo yalikuwa yamevunjika. Alimwambia baba yake yaliyovunjika nayo ni mazuri. Mungu anaona hivyo.

Kitabu cha Waebrania katika Biblia sura ya 11 kitawataja mashujaa wa Imani. Kinataja nguvu zao. Hakitaji udhaifu wao. Ibrahimu Baba wa Imani alidanganya mara mbili kuwa mke wake ni dada yake. Sara aliicheka ahadi ya Mungu ya kuwa atazaa wakati alikuwa mzee. Yakobo alidanganya na kuchukua haki ya mzaliwa wa kwanza. Noa alilewa.

Samson alichezewa na Delila. Gideoni alikuwa na woga. Eliya alikata tamaa na hakutaka kuendelea kuishi. Yona alimkimbia Mungu. Watu hawa walianguka lakini waliangukia mbele. Waliokota somo.

“Mafanikio yapo kwenye barabara moja na kushindwa; mafanikio yapo chini kidogo kwenye barabara,” alisema Jack Hyles.

Kushindwa ni sehemu ya mchakato wa kushinda. Somo likiokotwa kushindwa kunakuwa sehemu ya kushinda.

“Wale ambao wameshindwa vibaya sana wanakuwa wa kwanza kungundua kanuni ya Mungu ya mafanikio,” alisema Erwin Lutzer.

Licha ya mapungufu machache mtu anaweza kuwa mzuri. Mwanamke mmoja huko India wakati wa kusema neno kwenye mazishi ya mume wake alisema, “Sitaimba sifa za mume wangu. Sitasema jinsi alivyokuwa mzuri. Nitasema kile kilichotokea kitandani. Ulishawahi kuwasha gari lakini haliwaki. Ndivyo alivyokoroma. Wakati wa ugonjwa wake nilifurahi kusikia sauti ya kukoroma nilijua bado yuko hai. Sasa siwezi kusikia tena. Watoto wangu nafikiri mtapata wenzi ambao ni wazuri katika mapungufu yao.”

Maneno hayo yanatufundisha umuhimu wa binadamu, hadhi ya binadamu, mazuri ya binadamu ni mengi kuliko mapungufu yake.

You can share this post!

Ruto aidhinishwa rasmi na IEBC kuwania urais

Baya amfokea Joho kwa kujihusisha na siasa za eneo la Kilifi

T L