• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Baya amfokea Joho kwa kujihusisha na siasa za eneo la Kilifi

Baya amfokea Joho kwa kujihusisha na siasa za eneo la Kilifi

NA WINNIE ATIENO

MBUNGE wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya amemuonya Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho dhidi ya kile anachokitaja kama kupotosha wakazi wa Kilifi.

Wiki iliyopita, Gavana Joho alikita kambi Kilifi akiuza sera za muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya akiwasihi wakazi wa kaunti hiyo kuwapigia kura wagombeaji wa ODM pekee.

Gavana huyo na viongozi wa ODM akiwemo Gideon Mung’aro, Teddy Mwambire (mbunge wa Ganze), Mishi Mboko (mbunge Likoni), na Stewart Madzayo (seneta) walimshtumu Naibu wa Rais William Ruto kwa kuhadaa Wapwani, wakisema alihusika katika uhamisho wa huduma za Bandari ya Mombasa hadi Naivasha na sasa anatumia suala hilo kisiasa akisema akichaguliwa kuwa rais atazirejesha.

Pia walimtaka Dkt Ruto awape maskwota shamba la ekari 2,536 ambalo alisema alizawidiwa na aliyekuwa mbunge wa zamani wa Taveta, Bw Basil Criticos.

Bw Joho aliyechaguliwa na Bw Raila Odinga kusimamia kampeni zake eneo la Pwani, alianza rasmi kampeni hizo eneo la Kilifi akiwasihi Wapwani kumuunga mkono Bw Odinga ili wanufaike na uongozi wake.

Hata hivyo, viongozi wa UDA wakiongozwa na Bw Baya walimtaka akome kupotosha wakazi wa Kilifi na jamii ya Wamijikenda.

Bw Baya alimtaka Bw Joho aendeleze siasa zake Mombasa na kukoma kuingilia siasa za Kilifi. Bw Baya alisema ujio wa aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko katika ugavana wa Mombasa umemtia Bw Joho kiwewe.

“Sisi kama watu wa Kilifi hatutamruhusu aje awe tena mkoloni hapa, alete utawala wa ukoloni mamboleo. Kama anamwogopa Bw Mike Sonko sasa anakimbilia Kilifi, sisi pia tutamfukuza kama vile watu wa Mombasa wamemfukuza,” alisema.

Bw Baya alisema Kilifi ‘ina wenyewe’.

“Sisi viongozi wa Mijikenda akiwemo Aisha Jumwa (mbunge wa Malindi), Jimmy Kahindi (Spika wa Bunge la Kilifi) na mimi tutasimama na Wamijikenda na hatutaki utawala wa Bw Joho. Afunge virago na watu wake aende huko Mombasa. Bw Joho wakati wako wa kutawala wakazi wa Kilifi umeisha funga virago uende,” alisema Bw Baya.

  • Tags

You can share this post!

DINI: Ukianguka, okota kitu; okota funzo muhimu

Kampeni kuchacha Boga, Mwakwere wakiidhinishwa kugombea

T L