• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:47 AM
FAIDA YA UBUNIFU: Anatengeneza mitambo ya kilimo kusaidia katika uongezeaji thamani

FAIDA YA UBUNIFU: Anatengeneza mitambo ya kilimo kusaidia katika uongezeaji thamani

Na BENSON MATHEKA

MNAMO Oktoba 2010, Thomas Nzuki alihudhuria maonyesho ya kimataifa ya kilimo na biashara ya Nairobi akiwa amevunjika moyo baada ya kupoteza ajira kampuni iliyokuwa imemwajiri ilipopunguza wafanyakazi.

Alitumia pesa alizokuwa nazo kununua mashine ya kukatakata lishe ya mifugo kwa kuwa alinuia kufuga ng’ombe wa maziwa.

Baada ya mwaka mmoja, akitumia mashine hiyo wakazi wa kijiji cha Mbiuni, Mwala Kaunti ya Machakos walivutiwa sana nayo wakawa wanamuomba waitumie kuandalia mifugo wao lishe.

Walitamani kununua mashine kama hiyo lakini wakatatizika kufika Nairobi zilikokuwa zikiuzwa. Hapo ndipo Nzuki alipojiwa na wazo la kuanza kutengeneza mashine hizo na kuwauzia wakazi.

“Nilimwendea fundi mmoja na kumuuliza iwapo angeweza kuunda mashine kama hiyo na alipoikagua, akasema haikuwa ngumu kuunda.

Shida ilikuwa ni vifaa. Nilijikuna kichwa. Nikakodisha vifaa alivyohitaji na tukaunda mashine ya kwanza mwaka wa 2012 ambayo niliuza,” asema Nzuki. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa biashara anayofanya hadi wakati huu.

“Nilijibwaga katika biashara ya kuunda mashini mbalimbali za kilimo ambazo wakazi walikuwa wakihitaji. Nilikuwa nikiwauzia kwa bei nafuu na baada ya mwaka mmoja nikaanza kupata wateja kutoka maeneo ya mbali Kaunti ya Kitui, Embu na Makueni,” asema Nzuki.

Mnamo 2014, alifungua karakarana yake karibu na uwanja wa maonyesho ya kilimo wa Machakos ambayo huwa anatumia kutengeneza na kuuza mitambo ya kubambua mahindi maarufu kama maize sheller, mitambo ya kusaga unga, mashini tofauti za kuandaa lishe ya mifugo na pampu za maji.

“Lililoanza kama wazo la kusaidia wakazi wa kijiji changu wakome kuomba mashini yangu limekuwa kampuni kubwa ya kuunda na kuuza mashini za kilimo na kuongeza thamani mazao ya kilimo,” asema Nzuki.

Kampuni yake Masaku Simba Farm Machinery and Fabricators imeajiri watu zaidi ya 50 wakiwemo mafundi watatu, wauzaji na wanaoiuzia vifaa na kutoa huduma tofauti.

Thomas Nzuki akionyesha mitambo ya kilimo anayotengeneza katika kampuni yake ya Masaku Simba Farm Machinery and Fabricators. Picha/ Benson Matheka

“Hata kabla ya serikali kuweka ajenda ya ustawi wa viwanda vya humu nchini katika mipango yake, nilikuwa nimeanza,” asema. Kwa kuwa anatumia vifaa vya humu nchini kuunda mashine zake, anasema bei huwa nafuu kuwezesha wakulima wa kawaida kumudu.

“Tunauza mashine zetu kwa bei ya kati ya Sh40, 000 na Sh100,000. Ni mtambo wa kusaga unga ambao tunauza Sh100,000 kwa sababu wengi huutumia kwa biashara na pia unagharama kubwa kuunda,” asema.

Akizungumza na Akilimali katika karakana yake, Nzuki alisema juhudi zake zimetambuliwa na Idara za serikali na mashirika yanayohusika na kilimo ambayo huwa yanamualika kwa warsha tofauti kuonyesha bidhaa zake na kuwafunza wakulima.

“Sijawahi kutafuta kazi tangu nianze biashara hii. Ni mashirika, idara za serikali na wateja wanaonitafuta nikawahudumie, kuwauzia au kutengeneza mashine ninazowauzia zikiharibika,” asema. Anafichua kwamba pesa za chini ambazo amewahi kupata kwa mwezi ni Sh370,000.

“Hii ilikuwa mwaka jana wakati janga la corona liliathiri uchumi. Kwa kawaida, tunaweza kuuza mashini za Sh700,000 kwa mwezi,” asema. Yeye na mafundi wake huwa hawatozi wateja gharama ya kusafirisha na kuwawekea mitambo wanayonunua.

“Tunapatia mteja udhamini wa muda wa miaka miwili ambapo tunajukumikia mashine tunayomuuzia mteja ikipata hitilafu za kiufundi,” asema na kuongeza wanazingatia utaalamu wa hali ya juu ili kudumisha imani ya wateja wao.

“Changamoto tunayopata ni kuwa baadhi ya wateja huwa wanashindwa kutumia mashine na kutupigia simu wakidhani imeharibika. Huwa tunalazimika kuweka mipango ya kumtembelea au kumshauri ailete katika karakana yetu na kumfundisha upya jinsi ya kuitumia. Huduma hii tunatoa bila malipo japo inatugharimu,” asema.

Ili kuepuka hali kama hii, huwa anahakikisha wateja wanaelewa kuitumia mashini kabla ya kuinunua. Changamoto nyingine ni kutoaminika kwa wateja wanaoagiza mashine kwa simu wakiwa mbali kisha unapowapelekea unapata wamezima simu.

“Hii inanilazimu kushauri wateja kutembelea karakana wachague mashine, tuwafunze, walipe kabla ya kuwapelekea makwao,” asema.

Anasema kuwa anatangaza mitambo yake kupitia mitandao ya kijamii. Nzuki anaongeza kuwa ndoto yake ni kupanua biashara yake hadi maeneo ya mengi ya mashinani.

“Mitambo yetu inatumia dizeli na stima kwa hivyo inaweza kutumika eneo lolote,” anaeleza.

You can share this post!

AKILIMALI: Aliacha ubawabu sasa anapepea katika kilimo cha...

FAIDA YA UBUNIFU: Hajuti kuacha kazi ya benki na kujiajiri...