• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
FUNGUKA: ‘Sina ubaya, langu ni kuhudumia wenye njaa’

FUNGUKA: ‘Sina ubaya, langu ni kuhudumia wenye njaa’

Na PAULINE ONGAJI

BRAYO, kama anavyotambulika miongoni mwa wenzake, ni mwanafunzi wa chuo kikuu fulani jijini Nairobi, ambapo ukimtazama utadhani kuwa ni kaka wa kawaida anayendelea na shughuli zake za masomo.

Chuoni, ni mmoja wa wanafunzi stadi sio tu kimasomo, bali pia katika masuala ya michezo. Mbali na hayo, uhusiano wake na wanafunzi wenzake ni mzuri sana.

Ni suala ambalo limemzolea umaarufu sio tu miongoni mwa wanafunzi wake, bali pia walimu.

Lakini nyuma ya picha hii nzuri anayoonyesha watu, kaka huyu ameficha tabia ambayo huenda kwa wengi ni chafu sana. Brayo mwenye umri wa miaka 27, amekabwa na udhaifu wa kuvizia wake wa watu.

Mtaani yeye ni shujaa wa kuwapa burudani wake wa watu, na anafanya hivi bila majuto yoyote.

“Mimi ni ‘Msamaria Mwema’ na nia yangu ya kufanya hivi ni kutokana na huruma ninayo kwa wanawake hawa, ambao mara kwa mara nimewasikia wakilalama kuhusu jinsi waume wao ni mabwege hasa katika masuala ya mahaba.

Nia yangu ni njema kwani siitishi pesa na mradi nimemhudumia bibi, hakuna muunganisho mwingine wa kuunda uhusiano. Sina nia ya kuvunja nyumba ya mtu mie kwani pindi baada ya kuwapa burudani mimi husisitiza warudi kwa waume wao.

Mabinti wengi ninaoburudisha hurudi tena na tena kwa sababu mbali na ukwasi wangu katika masuala haya, siri kati yangu nao iko salama.

Nia yangu ni kuhakikisha kuwa wanawake na hasa wake wa watu hawaendi mbali kila wanapozidiwa na uchu wa kimahaba, kwani huko nje kuna hatari nyingi na hasa maradhi.

Kwa upande wangu, suala la kinga nalitilia maanani sana, na hivyo kuhakikisha usalama sio tu wangu, bali pia wa wenzangu.

Sina nia mbaya ndiposa nimedumisha uhusiano mzuri na waume wao na sidhani kati yao kuna hata mmoja anayeshuku huduma ninazowapa wake wao.

Nilianza uraibu huu miaka michache iliyopita baada ya kuwasili jijini Nairobi na kujiunga na chuo kikuu kimoja. Kutokana na sababu kuwa mimi huhudhuria masomo siku rasmi za kazi, niliona kuwa nilikuwa na wakati mwingi wakati wa wikendi, muda ambao ningetumia kutoa huduma kwa jamii.

Situmii ustadi wangu kama kitega uchumi, bali kazi hii kwangu ni huduma ya kuokoa ndoa za watu huko nje.

Siitishi pesa baada ya kutoa huduma hii kwani nia yangu sio kupata manufaa ya kiuchumi, ila tu kuzima kiu ya mabinti ambao huenda wangenaswa na fisi huko nje.

Nimebobea katika masuala haya kiasi cha kuwa kwa miaka hii yote sijawahi na siwezi kufumaniwa na waume wao kwani najua ratiba zao kamili.

Kwa ufupi, nimeumbwa kupenda burudani na hivyo kwa nini nimnyime binti uhondo huu asioweza kupata kutoka kwa mumewe?

Ni wakati wa akina kaka wenzangu kukumbatia huduma hii kwani wanawake wengi huko nje wanaumia kimahaba licha ya kuolewa, na hawajui pa kupata usaidizi.”

You can share this post!

MUTUA: Weka mipango ya maisha sio tu maazimio ya mwaka

Spurs wapepeta Leeds United 3-0 na kuruka hadi nafasi ya...