• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 6:55 PM
Gachagua adai walinzi wa viongozi wa Azimio waliondolewa ili wawatwange wakati wa maandamano 

Gachagua adai walinzi wa viongozi wa Azimio waliondolewa ili wawatwange wakati wa maandamano 

NA SAMMY WAWERU 

NAIBU RAIS, Rigathi Gachagua amesema vinara wa upinzani watarejeshewa askari serikali itakaposhawishika wamekoma kuishambulia. 

Bw Gachagua, alisema kwa sasa viongozi wa Azimio la Umoja wataendelea kusalia bila walinzi hadi pale watahakikishia serikali ya William Ruto kwamba hawana uhasama nayo.

Serikali ilitangaza Julai 2023 kuondoa askari wanaolinda viongozi wakuu wa Azimio, wakiongozwa na Bw Raila Odinga (ODM), Martha Karua (Narc-Kenya), Kalonzo Musyoka wa Wiper, miongoni mwa wengine.

Magavana walioathirika ni pamoja na Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Ochillo Ayacko wa Migori, na Gladys Wanga (Homa Bay).

Akizungumza Ijumaa, Agosti 18, 2023 wakati wa kufunga rasmi Kongamano la Ugatuzi 2023 lililofanyika Uasin Gishu, Naibu Rais alisema serikali ilichukua hatua hiyo kutokana na upinzani kuihangaisha kupitia maandamano.

“Tunataka mnaposhiriki maandamano, askari tuliowapokonya wawatwange,” Bw Gachagua alihoji.

Hata hivyo, alisema serikali itawarejeshea ulinzi itakaposhawishika wamelainika na kusitisha wito wa maandamano.

“Tukishawishika mmeacha kuhangaisha serikali kupitia maandamano, tutawarudishia ulinzi. Hata hivyo, mambo yalivyo kwa sasa inaonekana ‘vita’ havijaisha,” Gachagua alielezea.

Maandamano ya upinzani yalisimamishwa kwa muda kuomboleza waliouawa na kujeruhiwa kupitia ukatili wa polisi, na pia kuruhusu mazungumzo kati ya Azimio na serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Raila aliyatetea akisema yanalenga kushinikiza serikali ya Rais William Ruto kushusha gharama ya maisha.

Ametishia endapo matakwa ya Azimio hayataangaziwa, upinzani hautakuwa na budi ila kurejea barabarani.

  • Tags

You can share this post!

Pasta Ezekiel alivyodai wasanii wa Bongo Flava hawana...

Makanisa matano yaliyozimwa na serikali

T L