• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Prof Githu Muigai: Msomi mstaarabu  na mwanasheria mtajika

Prof Githu Muigai: Msomi mstaarabu na mwanasheria mtajika

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

Professa Githu Muigai alijiunga na Baraza la Mawaziri kama kipenzi cha wengi. Kama mtangulizi wake Amos Wako, alikuwa wakili wa kuheshimika, msomi na mtumishi wa umma wa kimataifa.

Muigai alikuwa mhadhiri wa sheria aliyependwa na wanafunzi wake kwa utaalamu wa hali ya juu.

Ni mshirika mwanzilishi wa moja ya kampuni kubwa za mawakili Wakenya asili, Mohammed Muigai LLP, ambapo uwezo wake katika masuala ya sheria hauna kifani.

Alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi alikohitimu 1983 na akasomea uzamili katika sheria katika Columbia Law School.

Baada ya kurejea, alifunza katika chuo chake cha zamani na kukuza kampuni yake ya sheria. Mnamo 2000 alichaguliwa katika Tume ya Mageuzi ya Katiba (CKRC), iliyohusisha watu mashuhuri, wengi wakiwa wasomi waliopatiwa jukumu la kuongoza juhudi la kwanza la kubadilisha katiba.

Muigai aliacha alama kwa kuonyesha uvumilivu na ustadi wa kushughulikia masuala tata. Baada ya kuteuliwa katika

CKRC, alisomea uzamifu katika sheria na kuhitimu Novemba 2002. Mnamo 2008, aliteuliwa mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wa rangi mamboleo, na dhuluma zinazohusiana na ubaguzi wa rangi.

Muigai pia alihudumu kama jaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kati ya 2008 na 2010. Kwa hivyo. aliingia serikalini akiwa mtaalamu wa kuheshimika aliyestahili zaidi kuwa Mwanasheria Mkuu.

Alichukua kazi hiyo na kuendelea na kazi ya utekelezaji wa katiba mpya. Akiwa mnenaji shupavu, alialikwa kuhutubu katika mikutano mingi ya sekta tofauti. Mtindo wake wa usimamizi uliandamana na mageuzi makubwa katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu.

Akiwa msitari wa mbele kuongoza, Muigai alifurahisha Wakenya wengi, hasa mawakili wanaohudumu na wanaotaka kuwa mawakili kwa kufika kortini binafsi kuwakilisha serikali iliposhtakiwa katika Mahakama ya Juu, Mahakama ya Rufaa katika Mahakama ya Juu.

Katika sheria za kimataifa, sifa za Kenya ziliimarishwa na ustadi na weledi wa Muigai. Alikomesha utamaduni wa kuajiri mawakili wa kimataifa kuwakilisha Kenya na kuanza kuwatuma maafisa wa afisi yake akiongoza katika msitari wa mbele.

Kumbukumbu nyingine ya Muigai ni kuteua mawakili wa serikali katika Mashirika ya Serikali kuhudumu kama Maafisa Wakuu Watendaji na katika bodi za wakurugenzi.

Juhudi za Muigai kuleta mabadiliko katika Afisa ya Mwanasheria Mkuu zilitatizwa na mitandao ya wafisadi ambao walitumia washirika wao serikalini na katika siasa.

Siasa katika taasisi yoyote ni siasa tu na inahitaji mtu kujiunga na upande wa wahusika ili kuwafurahisha. Hii ilikuwa kinyume na heshima na utaalamu ambao Muigai alikumbatia.

Hii ni kwa kuongeza ukweli kwamba Muigai alikuwa mgeni katika Afisi ya Mwanasheria Mkuu na Serikalini. Wakuu wa Sheria wote tangu uhuru walikuwa wanafunzi wa zamani wa Shule ya Wavulana ya Alliance sawa na walivyokuwa mawakili wakuu wa serikali.

Uchaguzi wa urais uliopingwa vikali ulisababisha kesi kali katika Mahakama ya Juu. Muigai alitetea ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya malalamishi ya Raila Odinga.

Baadhi ya taasisi za serikali zilitajwa na Muigai aliziwakilisha na kukabili vikali madai ya Odinga.

Uamuzi wa kesi hiyo ulivunja moyo karibu nusu ya nchi na makundi ya washirika wa siasa za Odinga. Kipindi cha ushindi kilifungua milango ya mwisho wa kazi ya Muigai kama Mwanasheria Mkuu wa Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Unavyoweza kufanikisha ufugaji wa nguruwe jijini

Visiki katika safari ya Ruto kuelekea Ikulu

T L