• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Unavyoweza kufanikisha ufugaji wa nguruwe jijini

Unavyoweza kufanikisha ufugaji wa nguruwe jijini

NA SAMMY WAWERU

KENYA ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19, mamia, maelfu na mamilioni ya wananchi waliathirika.

Baadhi walipoteza nafasi za ajira, wengine kufunga biashara na maeneo waliyokuwa wakizimbulia riziki. Ni hali ambayo wengi hawajaweza kupata afueni, licha ya gharama ya maisha kupanda kwa kiasi kikubwa, mfumko wa bei ya chakula ukiwalemea.

Huku wengi wakiendelea kukadiria mkumbo wa changamoto hizo, baadhi walijituma katika sekta ya kilimo. Takwimu za Idara ya Kilimo na Ufugaji zinaonyesha idadi ya wakulima na wafugaji nchini imeongezeka, hasa baada ya Kenya kukumbwa Homa ya Corona.

Kuna waliorejea mashambani, na kujiunga na mtandao wa wazalishaji wa chakula nchini. Maeneo ya mijini yakishuhudia uhaba wa ardhi, Kaunti ya Nairobi na viunga vyake, kuna baadhi wanaendeleza shughuli za kilimo na ufugaji.

Katika mtaa wa Mumbi, kilomita chache kutoka barabara kuu ya Thika Super Highway ndiko makao ya Mzee Henry Njoroge. Ploti yake ikiwa na ukubwa wa robo ekari, ina shughuli chungu nzima anazotekeleza, kuanzia ukuzaji wa mseto wa mboga za kienyeji, ufugaji wa kuku halisi wa kienyeji na vilevile nguruwe.

Mradi wake wa nguruwe una mvuto zaidi. Licha ya mtaa wa Mumbi kuwa kiungani mwa jiji, katika Kaunti ya Kiambu, Mzee Njoroge amegawanywa ploti yake kusitiri mifugo hao, ambao nyama zao hutumika kutengeneza soseji.

Nguruwe wa mfugaji Henry Njoroge wakishambulia chakula kilichopikwa…Picha/SAMMY WAWERU

“Wateja wangu wengi ni wamiliki wa buchari Nairobi na Kiambu,” asema. Aidha, amejenga makazi yenye kipimo cha futi 60 kwa 13. “Nikifanya hesabu, yalinigharimu zaidi ya Sh200, 000,” afichua mfugaji huyo.

Kandokando, yameundwa kwa mbao, juu yakiezekwa kwa mabati. Sakafu, ameikorogea saruji na kuiinamisha kiasi ili kurahisisha kuondoa kinyesi na mkojo. “Hutumia kinyesi chao pamoja na cha kuku kukuza mboga,” aelezea.

Njoroge anasema muhimu kufanikisha ufugaji wa nguruwe maeneo ya mjini, ni mkazi mwenye ari kuwa na nafasi. Haijalishi ikiwa ni kipande kidogo cha ploti au kikubwa, akisisitiza kinaweza kupangwa.

Boma la nguruwe wa Mzee Njoroge, ameligawanya kwa makundi matatu makubwa; la kwanza wale wa kiume, likifuatwa na wa kike na wana – vivimbi. Kila zizi vilevile limegawanywa kulingana na umri wa nguruwe. “Waliozaa, wana eneo maalum ili kuweza kutunza vivimbi,” asema.

Aidha, wanapomaliza kunyonya malapulapu ya mama zao, huwahamishia katika zizi wale wachanga. Anapopata wateja, hususan wafugaji huwauza bei ya kivimbi ikianzia Sh3, 000. Nguruwe huzaa miezi mitatu, wiki tatu na siku tatu baada ya kujamiishwa. Hujifungua kati ya wana 7 hadi 15, Njoroge akisema wake huwa na wastani wa vivinimbi 12.

Wanunuzi wengi wa nguruwe waliokomaa wakiwa wanabuchari, anasema huuza kupitia kilo. Kilo moja inachezea kati ya Sh350 – 380. “Nikiondoa gharama ya matumizi, ninasalia na mapato ya kuridhisha,” akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano katika mradi wake.

Mzee Henry Njoroge akikagua hali ya nguruwe wenye ujauzito…Picha/ SAMMY WAWERU.

Wafugaji wakiendelea kulemewa na bei ya juu ya chakula cha madukani cha mifugo, Njoroge amekumabatia mbinu maalum kukabiliana nayo. Chini ya kipindi cha muda wa mwaka mmoja uliopita, kimeshuhudia mfumko mkubwa.

Mfugaji Njoroge hukusanya masalia ya mazao mabichi ya shambani, ambayo huyapikia nguruwe. “Nina mfanyakazi anayenisaidia kuyakusanya kutoka masoko ya Githurai. Kabla kuyapika huyaosha,” anaelezea.

Mazao hayo yanajumuisha mboga, viazi mbatata, karoti, matunda na nafaka mbichi kama vile mahindi, miongoni mwa mengine. “Isitoshe, huwapa miguu na vichwa vya kuku kwa minajili ya virutubisho vya Protini,” adokeza.

Mzee Njoroge ana ‘jiko’ maalum la mapishi. Mkondo anaotumia pia umekumbatiwa na Wanjiru Mwepu, mfugaji wa nguruwe. “Mabaki ya chakula na mazao ya kilimo ni njia mojawapo kupunguza kwa kiasi kikuu gharama ya juu ya chakula cha mifugo,”Wanjiru asisitiza.

Njoroge vilevile huwapa nguruwe wake chakula cha madukani, ambacho kimeafikia ubora wa bidhaa. Wafugaji hata hivyo wanahimizwa kuwa makini wanapokinunua, kwa sababu kingi hakijaafikia ubora wa virutubisho na madini faafu katika mifugo.

Wataalamu wa masuala ya ufugaji wanashauri wafugaji haja ya kujikuzia na kujiundia lishe. “Itakuwa vyema walime nyasi kama vile za mabingobingo na Lucerne, na kutengeneza hay na silage,” ahimiza Michael Ngaruiya, mtaalamu.

Mfugaji Henry Njoroge akionyesha jiko la dramu ambalo hutumia kupikia nguruwe wake masalia ya mazao mbichi ya shambani…Picha/ SAMMY WAWERU.

Msimu wa mvua, wakulima wajitume kuweka akiba ya nyasi hizo kwa wingi pamoja na mimea kama mihindi na majani yanayoshabikiwa na mifugo. “Akiba itawasaidia kuokoa mifugo kiangazi na ukame unapobisha hodi,” Ngaruiya asema.

Mzee Njoroge ni makini kufuatilia afya ya nguruwe wake, na anadokeza ana vetinari anayemfaa katika shughuli hiyo. “Nyakati zingine, maradhi hulipuka na mfugaji asipokuwa ange hupoteza nguruwe,” asema.

Mwaka wa 2020, Wanjiru alipoteza nguruwe wote aliokuwa nao wakati huo kufuatia mkurupuko wa Homa ya Swine. Kisayansi, H1N1 Influenza, maarufu kama Swine Flu, ni ugonjwa hatari unaoathiri mapafu.

Watu wanashauriwa kutotangamana na nguruwe walioathirika na pia maeneo walioko. Njoroge aliingilia ufugaji wa nguruwe zaidi ya miaka kumi iliyopita, na anasema mifugo hao wamemsaidia kwa kiasi kikubwa kusukuma gurudumu la maisha.

Mzee Henry Njoroge akiwa kwenye zizi la nguruwe…Picha/ SAMMY WAWERU.

You can share this post!

Impala yaendea Mwamba fainali ya Ligi Kuu ya raga ya...

Prof Githu Muigai: Msomi mstaarabu na mwanasheria mtajika

T L