• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Visiki katika safari ya Ruto kuelekea Ikulu

Visiki katika safari ya Ruto kuelekea Ikulu

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais William Ruto sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuteua mwaniaji mwenza, kuimarisha uhusiano na vyama vidogo na kukwepa visiki anavyowekewa na serikali huku akianza rasmi safari ya kuelekea Ikulu.

Dkt Ruto juzi aliidhinishwa na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kuwa mwaniaji wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 katika Mkutano Wakuu wa Wajumbe (NDC) uliofanyika uwanjani Kasarani, Nairobi.

Chama hicho kilimpa Dkt Ruto mamlaka ya kushauriana na vyama vingine na kutia saini mkataba wa maelewano na vyama vitakavyojiunga na muungano wa Kenya Kwanza.

Vyama vinavyoegemea Kenya Kwanza ni Bw Amani National Congress (ANC) chake Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Moses Wetang’ula, Chama cha Kazi kinachoongozwa na mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, Tujibebe Wakenya cha gavana wa zamani wa Kiambu William Kabogo na Chama cha Mashinani (CCM) chake Isaac Ruto.

Kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) Mwangi Kiunjuri na mfanyabiashara Jimi Wanjigi ambaye ameidhinishwa kuwania urais kupitia chama cha Safi – na, walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria kongamano hilo la UDA .

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuidhinishwa kwa Dkt Ruto ni mwanzo wa changamoto tele ambazo atahitaji kuzitafutia jawabu bila kupasua muungano wa Kenya Kwanza.

Viongozi wa vyama ambavyo vinaegemea Kenya Kwanza wamekataa kuvunja vyama vyao na kujiunga na UDA.

Vyama hivyo vimeshikilia vitaunga mkono Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais lakini vitasimamisha wawaniaji wa ugavana, useneta, ubunge, uwakilishi wa wanawake na udiwani.

Lakini Dkt Ruto amesisitiza chama cha UDA kitasimamisha wawaniaji viti vyote katika maeneo yote nchini.

Naibu Rais amekuwa akikataa kuungana na vyama vidogo huku akivitaja kuwa vya kikabila na kuvishuku kufadhiliwa na mahasimu wake wa kisiasa – Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

Katibu Mkuu wa UDA, Veronica Maina anasema vyama vidogo vinatia doa sifa ya chama hicho ambacho ‘kina mwonekano wa kitaifa’.

Katika Kaunti ya Kiambu, Naibu Rais atakuwa na kibarua kigumu kuamua atakayepeperusha bendera ya UDA kwenye kinyang’anyiro cha ugavana.

Seneta Kimani wa Matangi, aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mbunge wa Thika Mjini Wainaina wa Jungle wametangaza azma ya kuwania ugavana

wa Kiambu kupitia UDA.

Bw Kuria atawania kiti hicho kupitia Chama cha Kazi na Bw Kabogo anasaka wadhifa huo kupitia Tujibebe.

“Atakayepata tiketi ya UDA atamenyana na mwaniaji wa Jibebe na Chama cha Kazi na hivyo kugawanya kura. Hiyo itatoa nafasi kwa Gavana James Nyoro wa Jubilee kuibuka mshindi,” asema Bw Herman Manyora, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Kuna uwezekano watakaobwagwa katika mchujo wa UDA watagura na kuwania kama wagombea wa kujitegemea.

Naibu Rais pia atakuwa na kibarua kigumu kuamua ikiwa atateua Bw Mudavadi kuwa mwaniaji mwenza wake au atatengea nafasi hiyo eneo la Mlima Kenya.

Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala amekuwa akisisitiza kuwa, chama cha ANC hakitakubali kupatia UDA mwaniaji wa urais na mwaniaji mwenza.

Lakini Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata anasema nafasi hiyo imetengewa Kaunti ya Murang’a.

Anasema viongozi wa Murang’a wameidhinisha mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Kandara Alice Wahome kuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto. Wengine wanaomezea mate nafasi hiyo ni mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, Seneta wa Tharaka Nithi Kindiki Kithure na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ambaye ametangaza azma ya kuwania urais kupitia chama cha Democratic Party (DP).

“Mudavadi hatamletea kura Dkt Ruto kutoka Magharibi ikilinganishwa na eneo la Mlima Kenya. Ruto hatapata zaidi ya kura 300,000 Magharibi haswa ikizingatiwa kuwa Bw Odinga ana ushawishi mkubwa katika eneo hilo,” anasema Bw Joseph Kaguthi, afisa wa zamani wa utawala.

Dkt Ruto anakabiliwa na kibarua kigumu kukwepa ‘miiba’ anayowekewa na serikali katika safari yake kuelekea Ikulu.

  • Tags

You can share this post!

Prof Githu Muigai: Msomi mstaarabu na mwanasheria mtajika

Omanga kuzidi kunengua mauno kuonyesha utiifu kwa Ruto

T L