• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
GWIJI WA WIKI: Damaris Ketrai

GWIJI WA WIKI: Damaris Ketrai

Na CHRIS ADUNGO

KINYUME na zamani ambapo uigizaji ulikumbatiwa kwa ajili ya burudani pekee, sanaa hiyo kwa sasa ni kazi ya kitaaluma katika soko la ajira kote duniani.

Ni jukwaa zuri linalozidi kuchangia ubidhaaishaji wa lugha katika juhudi za kupitisha elimu, kukuza maadili, kubainisha taratibu za maisha na kutoa fursa za kuthaminiwa kwa tamaduni za jamii mbalimbali.

Damaris Ketrai ni miongoni mwa wasanii wa humu nchini ambao wamefaulu kutumia ufundi wao wa lugha na vipaji vya uigizaji kuwa viwanda vya ubunifu, ajira na uvumbuzi.

Damaris alizaliwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na akalelewa katika mtaa wa Eastleigh, Nairobi. Ndiye wa tatu katika familia ya watoto tisa wa Bi Rael Oweya Okwaro na Bw Johnstone Tabbie aliyewahi kuwa mratibu wa klabu ya AFC Leopards.

Alisomea katika shule za msingi za Pangani na Highview jijini Nairobi kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Rovy Girls, Kaunti ya Nakuru.

Ingawa alipata fursa ya kusomea Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika chuo kimoja jijini Nairobi mnamo 2008, uchechefu wa karo ulimzimia mshumaa wa elimu.

“Vibarua nilivyovifanya baada ya masomo ya sekondari – kuuza mitumba na kuchuuza vipodozi – vilinijasirisha na kunielekeza zaidi katika fani ya uigizaji,” anasema.

Akiwa mwanafunzi wa darasa la nne, matamanio ya Damaris yalikuwa ni kujitosa katika ulingo wa muziki. Hata hivyo, uigizaji ulimteka akiwa na umri wa miaka 10 na kanisa likampa jukwaa la kuburudisha waumini kila Jumapili. Damaris hajawahi kupoteza dira tangu wakati huo.

Alijiunga na kikundi cha Jicho Four Productions mnamo 2009 na akapata fursa ya kuigiza vitabu vya fasihi vilivyokuwa vikitahiniwa katika shule za sekondari humu nchini. Moon Beam Productions na Phil It Productions ni makundi mengine ya filamu yaliyomkuza vilivyo kisanaa.

Baada ya kushiriki mchezo wa kwanza runingani, ‘Angel’s Diary’ (KBC, 2010), milango ya heri ilijifungua na akanogesha ‘Kenda Imani’ (KBC), ‘Vioja Mahakamani’ (KBC), ‘Daktari’ (KTN), ‘Auntie Boss’ (NTV) na ‘Inspekta Mwala’ (Citizen TV). Kwa sasa anaigiza mhusika Loretta katika ‘Zora’ (Citizen TV) na amekuwa akishiriki ‘Hullabaloo Estate’ (Maisha Magic East) Dstv tangu 2015.

Ulumbi

Mbali na uigizaji, Damaris ni mfawidhi wa sherehe, mjasiriamali na mshauri nasaha. Kipaji cha ulumbi anachokikoleza kwa sauti ya ninga na umilisi mkubwa wa Kiswahili na Kiingereza pia humpa fursa za kufyatua matangazo ya kibiashara kwa malipo ya kutamanisha.

Mwanamitindo huyu ni mwanandoa na mama wa watoto wawili. Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa miongoni mwa wasanii watakaotikisa ulimwengu wa uigizaji kwa kutoa filamu zitakazoendelea kukubalika kimataifa. Analenga pia kukuza na kulea vipaji vya waigizaji chipukizi katika ngazi na viwango tofauti.

“Usiingie katika fani ya uigizaji kwa kutamani kuiga watu waliobobea ndipo upate umaarufu. Jifunze kutoka kwa watangulizi wako na ujikuze hadi ufikie viwango vyao,” anashauri.

You can share this post!

Vuguvugu kutoa mwaniaji ugavana

Mtiririko wa vitushi na wahusika katika sura 10 –...

T L