• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
GWIJI WA WIKI: Heman Gitaa Angwenyi

GWIJI WA WIKI: Heman Gitaa Angwenyi

NA CHRIS ADUNGO

NDOTO ya kuwa mwanahabari ilianza kumtambalia Heman Gitaa Angwenyi katika umri mdogo.

Anapojitahidi sasa kufikia upeo wa taaluma yake, analenga pia kuwa mwandishi stadi wa vitabu ili abadilishe sura ya ujifunzaji na ufundishaji wa Kiswahili katika ngazi na viwango tofauti vya elimu.

Kipaji cha utangazaji kilianza kujikuza ndani yake akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Alitia azma ya kupalilia talanta hiyo kwa kuiga baadhi ya wanahabari wazoefu redioni na runingani.

Alifanya hivyo chini ya uelekezi wa Bw Nyamwaro Nyagemi aliyemfundisha Kiswahili katika shule ya Heshima Academy, Kaunti ya Nyamira (2007-2009).

“Nilikariri mashairi ya sampuli nyingi na kuwakilisha shule yangu katika mashindano mbalimbali. Kuwasilisha mbele ya hadhira kulinishajiisha na kuchangia kuimarika kwa matokeo yangu masomoni,” anasema.

Zaidi ya kusoma makala na habari za matukio mbalimbali gwarideni, alijiunga na makundi ya uimbaji na uigizaji na akawa mwepesi wa kutumbuiza waumini kanisani. Majukwaa hayo yalimnoa vilivyo, akaanza kukisarifu Kiswahili kwa ufundi mkubwa.

Mwanahabari Heman Gitaa Angwenyi wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Gitaa alizaliwa mnamo 1994 katika kijiji cha Keng’uso, eneo la Ekerenyo, Nyamira. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watano wa Bw John Angwenyi Nyataro na Bi Jane Osiemo.

Alianzia safari ya elimu katika shule ya msingi ya S.A Keng’uso (1997-2006) kabla ya kuhamia Heshima kisha shule za upili za Kiabonyoru, Nyamira (2010-2011) na Keng’uso (2012-2014).

Baada ya kukamilisha KCSE, ukubwa wa uwezo wake katika masomo ya lugha ulimchochea kujitosa katika tasnia ya uanahabari – alisomea Habari na Mawasaliano katika Chuo cha Nairobi Aviation, Bewa la Eldoret (2015-2017).

Alipokea mafunzo nyanjani katika shirika la Kenya News Agency (KNA) tawi la Nyamira kabla ya kujiunga na Minto FM (KBC) mnamo 2018.

Akitambuliwa kwa lakabu ‘Timboroa’, alikuwa miongoni mwa waendeshaji wa kipindi cha Ekegusii, ‘Bwakire’, kilichoongozwa na Moses Ng’wono na Evans Mising’a almaarufu Omong’ina Nyorosa.

Mbali na uanahabari, Gitaa pia ni mshairi mbobevu na mwandishi shupavu wa vitabu anayechangia makuzi ya Kiswahili kupitia mijadala ya kitaaluma mitandaoni na vyombo vya habari.

Mengi ya mashairi yake yamekuwa yakifana kwenye mashindano mbalimbali ya tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Ilhamu anayojivunia katika ulingo wa uandishi ilichangiwa zaidi na mwalimu Joash Wafula aliyetambua utajiri wa kipaji chake katika utunzi wa kazi bunilizi akiwa sekondari.

Gitaa amechangia mashairi katika diwani ‘Malenga wa Afrika’, ‘Wosia Na Mashairi Mengine’ na ‘Tasnia ya Mashairi’ huku baadhi ya tungo zake zikichapishwa katika gazeti la ‘Taifa Leo’ chini ya lakabu ‘Malenga Mlawandovi’.

Baadhi ya hadithi ambazo amechapishiwa vitabuni ni ‘Alikanyaga Chechele’ katika mkusanyiko ‘Mateka na Hadithi Nyingine’ na ‘Ndururu Iliua Msumari’ katika antholojia ‘Maisha Karakana na Hadithi Nyingine’.

  • Tags

You can share this post!

AU, UN zaunga jeshi la EAC kukabili waasi DRC

TAHARIRI: Kibaki anafaa kuigwa na kila mwanasiasa mwenye...

T L