• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:47 PM
GWIJI WA WIKI: Phylis Kemunto

GWIJI WA WIKI: Phylis Kemunto

NA CHRIS ADUNGO

Ingawa alianza kuimba katika umri mdogo, kipaji chake cha utunzi kilipaliliwa zaidi akiwa mwanafunzi wa shule ya upili. Walimu walimpa fursa tele za kushiriki tamasha za kitaifa za muziki na wazazi pia wakamruhusu ajiunge na makundi mbalimbali ya uimbaji kanisani.

Alitamba kwa urahisi kwenye mashindano ya ngazi na viwango tofauti katika sanaa ya uimbaji kutokana na ukakamavu na kipawa cha ulimi kilichomfanya maarufu miongoni sana mwa walimu na wanafunzi wenzake.

Phylis alijikuza zaidi kisanaa akiwa na Magena Youth Choir iliyompokeza malezi bora ya muziki kuanzia mwaka wa 2010. Anajivunia kutungia kwaya hiyo ya nyimbo za Kiadventista vibao vinne – ‘Japo ni Machungu’ (2016), ‘Mungu wa Yakobo’ (2017), ‘Ayubu’ (2019) na ‘Rafiki’ (2019).

Alijiunga na kundi maarufu la Msanii Music Group mnamo Disemba 2020, mwaka mmoja baada ya Top Sound Studios kumfyatulia kibao ‘Omoika Omochenu’ (Roho Mtakatifu Niongoze).

‘When You Pray’, ‘Unastahili’, ‘Inuka Uangaze’ na ‘Maisha ya Mwanadamu’ ni nyimbo ambazo alirekodi na Msanii Records kati ya Mei 2020 na Novemba 2022.

Still Alive Production ilimchomolea kibao ‘Asante’ mnamo Januari 2023, miezi mitatu kabla ya Dokta B kumtolea wimbo ‘Nafasi ya Pili’.

Phylis amekuwa akiendesha kampeni maalumu ya kulisha watoto wa mitaani, masikini na wasio na makao kupitia mpango wa Favoured Generation tangu 2020.

Kubwa zaidi katika maazimio yake kisanaa ni kuhifadhi nyimbo zake katika albamu na kuchomoa wimbo mpya kila atakapohisi ana ujumbe wa kuipa jamii mwelekeo. Mbali na kupanua wigo wake wa ujasiriamali, anapania pia kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanamuziki chipukizi huku akikushirikiana na baadhi ya wasamii wazoefu kutumia uimbaji kueneza Ukristo.

Alilelewa katika kijiji cha Magena, Kaunti ya Kisii. Ndiye wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto wanane wa Bw Samwel Maina na Bi Josephine Nanjala. Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Magena (2000-2008) kabla ya kujiunga na shule ya upili ya St John’s Ichuni Mixed, Kisii (2009-2012). Ana shahada ya sayansi ya habari kutoka Chuo Kikuu cha Maasai Mara, Kaunti ya Narok (2013-2017).

“Fahamu unachokitaka na utambue unakokwenda. Kipende unachokifanya. Shindana na wakati. Weka Mungu mbele, jitume, omba sana na usikate tamaa,” anashauri.

  • Tags

You can share this post!

Siku ya Tatu: Maiti 36 zafanyiwa uchunguzi

Isaac Ruto ateuliwa mwanachama wa JSC kuwakilisha umma

T L