• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
Siku ya Tatu: Maiti 36 zafanyiwa uchunguzi

Siku ya Tatu: Maiti 36 zafanyiwa uchunguzi

NA ALEX KALAMA

WATAALAMU wa upasuaji wa maiti ambao wanafanya upasuaji wa maiti zilizofukuliwa Shakahola katika Kaunti ya Kilifi leo Jumatano ikiwa siku ya tatu wamefanyia uchunguzi miili 36 katika mochari ya hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Malindi.

Miili 16 ilikuwa ya watoto miili 19 ikiwa ya watu wazima, ambapo miili 17 ilikuwa ya wanaume 19 ikiwa ya wanawake.

Na mwili mmoja haikubainika wazi iwapo ulikuwa ni wa mtoto au ni wa mtu mzima.

Miili 23 ilikuwa imeoza vibaya sana, miili 11 ikiwa imeoza kwa kiwango cha wastani huku miili miwili ikiwa imeoza kidogo.

Kati ya miili 36 iliyofanyiwa upasuaji, miili 23 ilionyesha dalili za kuwa watu walioaga dunia kwa sababu ya kukosa chakula na maji.

Nayo miili mitatu ya watoto na mwili mmoja wa mtu mzima ikionyesha dalili za kuwa watu waliofariki kwa sababu ya kukosa hewa safi ya oksijeni.

Miili saba ikikosekana kutambulika wazi kilichosababisha vifo vyao kwa sababu ilikuwa imeoza vibaya.

Mwili mmoja wa mtoto ulikuwa na alama za kupigwa kichwa huku mwingine ukionyesha dalili za kuvunjwa shingo.

Mwili wa mtu mzima mmoja ulionyesha dalili za kuwa alikuwa na shida ya moyo na figo ambavyo vilisababisha kifo chake.

Mpasuaji mkuu wa serikali Johansen Oduor amesema ni vigumu kujua walizikwa lini kwa sababu walizikwa katika awamu tofauti tofauti.

Huku akieleza kwamba wote walikuwa na viungo vyao kamili hakuna hata mmoja ambaye alipatikana akiwa ametolewa viungo.

Aidha mwanapatholojia huyo amedokeza kuwa shughuli ya kuchukua sampuli za vinasaba vya DNA kwa wale ambao wanatafuta jamaa zao inafanywa bure wala hakuna yeyote atakayetozwa fedha.

“Kwa jinsi tunavyofanya kazi kwa haraka, nafikiri katika siku mbili zijazo tutaweza kukamilisha kibarua kilicho mbele yetu na baada ya siku mbili nadhani tutarudi Shakahola ili kuangalia ikiwa hali ya hewa inaruhusu kuendelea na ufukuaji makaburi ili kutoa miili zaidi,” amesema Dkt Oduor.

Mbali na hayo ni kwamba mwanaume mmoja ameokolewa katika operesheni inayoendelea kwenye msitu wa Shakahola.

  • Tags

You can share this post!

Azimio wasitisha maandamano baada ya Kenya Kwanza kumwondoa...

GWIJI WA WIKI: Phylis Kemunto

T L