• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
GWIJI WA WIKI: Ryan Mwenda

GWIJI WA WIKI: Ryan Mwenda

NA CHRIS ADUNGO

MATAMANIO ya Ryan Mwenda, 14, ni kutikisa ulingo wa filamu kimataifa kiasi cha kufikia kiwango cha staa wa Amerika, Broderick Steve Harvey.

Mbali na kuwa daktari kitaaluma na lulu katika fani ya uigizaji, mwanafunzi huyu wa kidato cha kwanza katika shule ya upili ya Light Academy jijini Nairobi, analenga pia kuwa mwanasoka maarufu, chale shupavu, mshereheshaji stadi na mlumbi wa kustahiwa.

Wanaozidi kuweka hai ndoto zake ni mamaye mzazi, Bi Doris Kanario pamoja na Sean Katemah – kaka yake aliye na talanta ya uchoraji.

Mwingine anayemchochea pakubwa kisanaa ni afisa wa ubalozi mdogo wa Kenya katika jiji la Los Angeles nchini Amerika, Thomas Kwaka almaarufu ‘Big Ted’.

“Uigizaji na ulumbi ni vipaji vilivyoanza kujikuza ndani ya Ryan katika umri mdogo. Vyombo vya kidijitali vilimsisimua mno. Alivutiwa pia na vibonzo na michezo ya viwango vya juu vya ubunifu wa kiteknolojia,” akatanguliza Bi Kanario.

“Alianza masomo tayari akifahamu thamani ya michezo na sanaa mbalimbali. Walimu walitia azma kupalilia talanta zake na shule ikampa majukwaa mwafaka ya kutononoa vipaji hivyo,” akaeleza.

Kwa mujibu wa Bw Elias Mugambi anayefundisha Light Academy, Ryan ni mwanafunzi wembe masomoni ambaye sasa huongoza darasa lake katika kila mtihani.

“Zaidi ya Hisabati na Fizikia, anapenda pia masomo yanayoegemea masuala ya biashara, sanaa na mawasiliano. Anatazamia kuwa tabibu au mtaalamu wa sayansi ya michezo katika siku za usoni,” akasema.

Katika umri wa miaka minne na nusu pekee, Ryan alikuwa tayari amejikuza kisanaa kupitia kipindi maarufu cha ‘Churchill Show’ na akawa maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake. Alitamba kwa urahisi kutokana na kipawa cha ulimi kilichomfanya awe mwepesi wa kutema maneno ya kuvunja mbavu kwa ufundi mkubwa.

Alishiriki tamasha nyingi za muziki na drama na akaongoza shule yake ya msingi ya Riara kuzoa tuzo za haiba katika mashindano ya ngazi na viwango tofauti.

Weledi wake katika ulumbi na uigizaji uliwahi kumpa fursa adhimu za kuburudisha Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wengine wakuu serikalini katika uwanja wa Kasarani mnamo 2013 na 2017.

Mbali na kuvumisha bidhaa za kampuni na mashirika mbalimbali kupitia matangazo ya kibiashara, Ryan aliwahi kuigiza mhusika Simba katika ‘Zora’ (Citizen TV, 2020-21). Mchezo huo wa kampuni ya Jiffy Pictures ndio ulimkweza hadi ngazi ya juu zaidi katika ulingo wa filamu.

Ryan Mwenda wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Kipaji chake cha kutandaza soka kilianza kujidhihirisha mnamo 2016 na akasajiliwa na akademia ya Ligi Ndogo SC jijini Nairobi.

Akiwa huko, alipata nafasi za kuzuru Uingereza kati ya 2018 na 2019 na maarifa yake katika kabumbu yakamezewa mate na vikosi vya Manchester United, Manchester City, Bolton Wanderers na Aston Villa.

Ingawa kwa kawaida ni mpole, Ryan ana ukakamavu wa kuajabiwa. Zaidi ya kuwaelekeza watoto wengine katika sanaa ya uigizaji, ana ari ya kuhamasisha umma kuhusu masuala ya afya pamoja na umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kudumisha amani.

“Inatia moyo kwamba nazidi kutambulika kimataifa japo naamini safari bado. Siri ya kufaulu ni kudumisha nidhamu na kumtanguliza Mungu katika kila hatua,” anasema Ryan.

  • Tags

You can share this post!

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya msingi ya...

NDIVYO SIVYO: Aisee, ni kosa kusema kuwa simu imezima!

T L