• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
NDIVYO SIVYO: Aisee, ni kosa kusema kuwa simu imezima!

NDIVYO SIVYO: Aisee, ni kosa kusema kuwa simu imezima!

NA ENOCK NYARIKI

AGHALABU nguvu za betri ya simu zinapopungua, baadhi ya watu husema; ‘Simu yangu imezima.’

Yamkini kauli hii hutokana na lugha za kwanza za baadhi ya watu.

Neno ‘zima’ liko katika mnyambuliko wa kauli ya kutenda.

Vitenzi vilivyo katika kauli hii huwa havijaongezewa viambishi vyovyote navyo huonyesha kwamba jambo fulani linatekelezwa na mtendaji.

Jambo jingine ambalo ni muhimu kulifahamu ni kuwa vitenzi ambavyo asili yake ni Kibantu huisha kwa kiambishi ‘-a’ ambacho si sehemu ya mzizi wa neno.

Wakati mwingine, kiambishi ‘a’ katika kauli hii kinaweza kuibua dhana ya rai, himizo au amri kutegemea matumizi yake katika sentensi.

Mathalan, mtu anapomwambia mwenzake; ‘‘Zima simu’’ kauli hii inaweza kuibua rai, himizo, amri au kitendo cha kuelekeza tu.

Ifahamike kuwa vitenzi vilivyo katika kauli hii haviwezi kutumiwa kuonyesha kuwa mtu au kiumbe fulani kimejitenda kitendo.

Dhana hiyo (ya kujitenda kitendo) inaweza kuwasilishwa kwa kiambishi {ji} .

Mathalani, tunasema: simu imejizima; miti imejiotea; anajipenda n.k.

Ni kosa kusema kwamba simu imezima kwa kuwa kauli hii inaipa simu uwezo wa kutekeleza kitendo kinachorejelewa.

Iwapo lengo la mzungumzaji ni kuonyesha kwamba simu imejizima kwa sababu ya kupungukiwa na nishati au kawi, basi kitendo hicho kinaweza kuelezewa vyema kwa kutumia kauli ya kutendeka. Waama, katika kauli ya kutendeka, msababishaji wa kitendo hajitokezi ila tunaambiwa kuwa kitendo kimetokea katika hali fulani au wakati fulani.

Alhasili, ‘simu imezimika’ ni njia mwafaka ya kuelezea kuwa hapana mtu aliyehusika katika kukizima kifaa chenyewe.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Ryan Mwenda

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kuvumiliana na kupendana ndiko...

T L