• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
HADITHI FUPI: Mbinu za kimtindo katika ‘Mapambazuko’

HADITHI FUPI: Mbinu za kimtindo katika ‘Mapambazuko’

MWANDISHI ametumia mbinu anuai katika hadithi Fupi Mapambazuko.

Naomba tudondoe kadhaa zifuatazo:

Majazi – majina yaliyotumiwa yanalandana na sifa za wahusika. Mzee Makutwa anaitwa hivyo kutokana na yaliyomfika. Uhalifu wake unagunduliwa anapofumaniwa na Mzee Makucha. Macheo hurejelea wakati jua hupambazuka. Mawazo ya Bi Macheo ndiyo yanamshinikiza mumewe kumpeleleza Mzee Makutwa na anafaulu kutegua kitendawili cha afanyacho pale kijijini na vijana kila siku. Majina mengine yaliyotumiwa kimajazi ni la mzee Makucha na mji wa Kazakamba.

Methali imetumiwa kupambanua matukio. Methali ‘jambo usilolijua ni usiku wa giza’ inaelezea jinsi wanakijiji hawakujua ni nini Mzee Makutwa alikuwa akifanya na vijana aliowajaza garini mwake kila uchao.

Maswali ya balagha yametumiwa kusisitiza ujumbe unaorejelewa. Mzee Makucha anaashiria Mzee Makutwa hakumfaa alipofutwa kazi. Alimuuliza mkewe, “Je, alinisaidia alipokuwa waziri? Ng’o!. Ili kuelezea hawana urafiki wa karibu, anamweleza, “… mtu akija kwako kukujulia hali umfukuze?”

Nidaa au siyahi ni tamko linalomwelekeza msomaji abainishe hisia za mhusika fulani. Ili kusisitiza Makutwa aliyapuuza masaibu yaliyomfika Makucha, anajibu swali aliloliuliza na tamko ‘Ng’o! Alipoachishwa kazi, inaelezwa Makucha alihasirika zaidi shirika alilokuwa akidai lilipofilisika. ‘… hata marupurupu yake hakupata kulipwa!’

Utohozi umejitokeza kwa wingi. Maneno yaliyokopwa kutoka lugha ya Kiingereza na kuswahilishwa ni kama veranda ( verandah), kesi (case), noti (notes), dereva (driver), teksi (taxi) na matoroli (trolleys).

Semi zimetumiwa kufumba ujumbe. Mwandishi anatumia msemo ‘alipigwa kalamu’ kuelezea Makucha alifutwa kazi. Wale vijana walioajiriwa katika migodi walikuwa pale kuzumbua riziki, kumaanisha walikuwa wameajiriwa pale.

Tashbihi imetumiwa kulinganisha matukio. Inaelezwa machungu yaliyompata Makucha baada ya kufutwa kazi yalikuwa ni sawa na yale ya kupigiliwa msumari moto kwenye kidonda kibichi. Matarajio yake ya kuwa na maisha mema uzeeni yakaporomoka kama jabali la barafu juani.

Jazanda – awamu za maisha ya mwanadamu zimefananishwa na safari ya jua angani. Jua kupambazuka inawakilisha mwanzo wa jambo. Dai anaeleza wako alasiri mwa maisha yao kumaanisha wako katika kipindi cha maisha wanachoweza kutekeleza mengi, namna wakati wa alasiri waja huwa na muda wa kutosha wa kutekeleza azma zao. Magharibi yanawakilisha wakati wa uzeeni, waja wanapokaribia kufikia hatima ya maisha yao. Mzee Makutwa anakiri yuko katika kipindi hiki.

Tashihisi – Bi Macheo alipomnasihi mumewe, alihisi kama maneno yale yalimtwanga kichwa. Mzee Makucha aliamini kuna siku jua la macheo lingembishia mlango. Alitumaini angefanikiwa maishani, japo siku zake za uzeeni.
Mifano mingine ni; tauria, uzungumzi nafsia, lakabu, simango, kisengere nyuma na utabiri.

Grace Ogoye

Kisumu Girls High School

  • Tags

You can share this post!

TAMTHILIA: Mtiririko wa matukio katika sehemu 11, Onyesho I

MIZANI YA HOJA: Ni vizuri kutenda wema maishani lakini...

T L