• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Haja ipo kurejelea mbinu asilia kupika na kupakua, kuhifadhi chakula na maji

Haja ipo kurejelea mbinu asilia kupika na kupakua, kuhifadhi chakula na maji

Na SAMMY WAWERU

ENZI za kina babu na nyanya maradhi yanayosababishwa na lishe yalikuwa nadra kuripotiwa.

Huku kasi na visa vya Saratani vikitajwa kuchangiwa na vyakula, miaka ya zamani ugonjwa huu hatari ulihusishwa na nasaba au ukoo.

Waliogonjeka, katika historia ya ukoo wao, watu kadha walisemekana kuugua kansa.

Hata hivyo, katika karne ya sasa, karne ya 21 tuliyopo, visa vya saratani vimekuwa vingi.

Katika kila familia, jamaa na marafiki nchini, hakujakosa kuripotiwa maafa yaliyosababishwa na Saratani.

Kwa mujibu wa tafiti na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka uliopita, 2020, zinasema watu milioni 10 ulimwenguni hufariki kila mwaka kutokana na Kansa.

Ni gonjwa hatari na ambalo limetajwa kuongoza kusababisha vifo.

Isitoshe, gharama yake ya matibabu ni ghali mno, wengi wakilemewa na mzigo wa bili, kikwazo ambacho ni sawa na kuweka chumvi kwenye kidonda kinachouguza majeraha.

Kenya, takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kila mwaka zaidi ya watu 20,000 huaga dunia kutokana na saratani.

Aidha, ni takwimu za kuogofya, na ambazo zinapaswa kutia kila mmoja wasiwasi.

Saratani imepokonya taifa viongozi tajika na waliokuwa na maono kuliboresha, kama vile aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mawasiliano ya Safaricom, Bw Bob Collymore, Gavana wa Bomet Bi Joyce Laboso, mbunge wa Juja na wa hivi karibuni kuangamizwa na kansa, Bw Francis Waititu maarufu kama Wakapee, kati ya wengineo.

Aina ya mlo, umetajwa kuwa miongoni mwa visababishi vya ugonjwa huu.

Agosti 2019 katika mazishi ya Gavana Laboso, Rais Uhuru Kenyatta alihimiza Wakenya kutathmini lishe wanayokula.

“Hivi vyakula vilivyosindikwa, tunapaswa kuvitathmini, tusiwe watu wenye mazoea ya kuvila.

“Vinaendelea kutuletea hasara, tumepoteza wananchi wengi kutokana na saratani,” alishauri kiongozi huyo wa nchi, akihimiza watu warejelee vyakula asilia.

Ni matamshi ambayo pengine wengi hawakuyatilia maanani wala mkazo, ila Rais Kenyatta alikuwa na ujumbe maalum “tutathmini aina ya vyakula tunavyotia tumboni”.

Kando na aina ya lishe, jinsi ambavyo inapikwa ni suala muhimu kuzingatia.

Mosi, vifaa kama vile sufuria vinapaswa kuwa salama, kupitia malighafi yanayotumika kuzitengeneza.

Vihifadhio tusivipuuze. Baadhi vimeundwa kwa kutumia malighafi tusiyojua au tusiyofahamu uhalisia wake.

Aidha, vingine vimetengenezwa kwa kutumia kemikali, na ambazo ni hatari kwa afya ya binadamu.

Huku Mamlaka ya Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini (Kebs), ikiwa na kibarua kigumu kujua vile bora na ambavyo havijaafikia ubora, baadhi ya vyombo vya mapishi, kuhifadhi chakula na pia kupakua huenda vikawa kisababishi cha maradhi.

Winny Mwangi hutengeneza vyungu vya mapishi na maji. Picha/ Sammy Waweru

Matamshi ya Rais Kenyatta, “haja ipo turejelee vyakula asilia”, vilivyoliwa na kina babu na nyanya zetu, yanapaswa kuenda sambamba na vifaa vya mapishi na kusafu.

Wangwana hao, na waliokuwa wakwasi wa busara japo walitutangulia mbele ya haki walitumia vyungu katika mapishi, kuyahifadhi na pia kupakua.

Ni enzi ambazo teknolojia ya sasa haikuwa imechipuka.

Tukijiita ‘wanadijitali’ na tunaoenda na nyakati, chakula hatutakiepuka kwa sababu ndicho msingi wa kuishi.

Winny Mwangi, na ambaye ni mfinyanzi anahisi mahangaiko yanayosababishwa na Saratani, watoto kuachwa yatima, familia, jamaa na marafiki kupoteza wapendwa wao, kupitia Kansa yataangaziwa na kupunguzwa ikiwa tutarejelea mfumo asilia kufanya mapishi.

“Zamani, vyungu vya udongo ndivyo vilitumika kupika, kina babu na nyanya, na waliowatangulia hawakulalamikia usalama wa mlo. Kwa sababu gani? Vifaa walivyotumia vilikuwa salama,” Winny anafafanua.

Aidha, vyungu huundwa kutokana na udongo tunaotumia kukuza vyakula, hivyo basi ni ishara kuwa salama.

“Isitoshe, udongo una madini faafu katika mwili wa binadamu kama vile Iron, Calcium, Magnesium, kati ya mengineyo, na hii ina maana kuwa vyungu vinasaidia kuongeza virutubisho kwenye chakula,” asisitiza, akiongeza kuwa vyungu vilivyofinyangwa kwa udongo husaidia kusawazisha Asidi na Alkali kwenye maji (p.H).

Mama huyu hutengeneza vyungu vya mapishi na kuyahifadhi kabla kupakuliwa.

“Vifaa vya mapishi ninavyounda pia hutumika kupakua mlo,” anaelezea.

Mbali na vyungu vya mapishi, kuna vya kuhifadhi maji na ambavyo huyaongeza ladha, kuwa tamu.

“Umewadia wakati turejelee mbinu asilia kufanya mapishi na kuhifadhi tunachotia tumboni. Kinga ni bora kuliko tiba,” Winny anashauri.

You can share this post!

RIZIKI: Mwanadada msomi anayejikimu kwa ung’arishaji wa...

Kipa Matasi amezewa mate na miamba wa TZ na Zambia