• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Harusi hatuna: Jinsi gharama imeingiza baridi wapenzi waliotaka kufunga harusi 2023

Harusi hatuna: Jinsi gharama imeingiza baridi wapenzi waliotaka kufunga harusi 2023

NA WINNIE ONYANDO

GHARAMA ya maisha inapoendelea kupanda, wapenzi wanaopanga harusi sasa wamebaki njia panda kwani bei za bidhaa mbalimbali zimepanda maradufu.

Harusi huhitaji huduma mbalimbali, na kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha, baadhi ya wapenzi sasa wanahepa kuandaa harusi ya kukata na shoka kama njia ya kuhifadhi pesa.

Maandalizi ya harusi yanahusisha huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukodisha ukumbi, upishi, mavazi, mapambo, picha na video, burudani, ada za mratibu, magari, keki, pete za harusi, leseni ya ndoa, nywele na huduma za vipodozi, malazi, chakula cha jioni, matukio ya kabla ya harusi, gharama za baada ya harusi na gharama nyinginezo zisizotarajiwa.

Hata hivyo, gharama zinazohusiana na maandalizi ya harusi sasa imekuwa mzigo kwa wapenzi wanaopanga harusi.

Kwa sasa, bei ya petroli imepanda jambo ambalo limefanya bei za bidhaa mbalimbali kupanda maradufu.

Kutokana na hilo, baadhi ya wapenzi sasa wanapunguza idadi ya wanaohudhuria harusi yao.

Kwa mfano, hapo nyuma, Sh200,000 ingetosha kushughulikia wageni zaidi ya 100 ila kwa sasa, ikiwa umewaalika watu 100 kuhudhuria harusi yako, utalazimika kutumia kati ya Sh350,000 na Sh500,000.

Beth Patience, 26, ambaye anajitayarisha kufunga ndoa Mei 2024, alionyesha wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa gharama ya huduma mbalimbali.

“Bajeti yetu ni Sh450,000 ambayo ni pamoja na mahari. Hata hivyo, kwa kuwa gharama za bidhaa na huduma kama vile upishi, upigaji picha na video na gharama za usafiri imepanda mara dufu, tunalenga kuondoa huduma mbalimbali. Hii huenda ikatulazimisha kutumia pesa zaidi ili kuwa na sherehe ya kupigiwa mfano,” akasema Beth.

Kando na hayo, alieleza kuwa ikiwa gharama ya maisha itaendelea kupanda, basi huenda wakasongeza tarehe ya harusi mbele.

“Kupanga harusi chini ya hali ya sasa ya kiuchumi ni changamoto kubwa. Watoa huduma wanatoza bei za juu. Kutokana na utafiti wetu wa hapa na pale, bei za upigaji picha na video ni kati ya Sh70,000. Kwa upande mwingine, gharama ya kukodisha au kununua gauni ni kati ya Sh20,000. Kumbuka tutahitaji huduma za upishi, na hata mapambo,” akaongeza Beth.

Ili kupunguza mzigo wa kifedha, Beth na mpenziwe wanapanga kulipa mahari ya Sh150,000 mnamo Desemba, na kuwapa muda zaidi wa kutafuta pesa za ziada.

Licha ya vizuizi vya kifedha, Beth na mpenzi wake wanapanga kufunga ndoa haraka iwezekanavyo kabla hali ya uchumi kuwa mbaya zaidi.

Naye Pinto Odhiambo, ambaye anajitayarisha kufunga ndoa Aprili mwaka ujao, alikiri kwamba kupanda kwa gharama ya bidhaa na huduma kutawalazimu kutafuta usaidizi wa ziada wa kifedha kutoka kwa marafiki na familia.

“Ingawa rasilimali ni chache, tumejitolea kutafuta suluhu. Lazima tupate suluhu kwa kuwa hatupangi kuahirisha harusi yetu,” akasema Pinto.

Pinto pia alitambua kuwa kupanda kwa gharama ya maisha kunaweza kusababisha wapendanao kukumbatia ndoa za muda.

Hata hivyo, anawahimiza vijana wanaopanga kufanya harusi kuanza kujipanga mapema.

“Mnafaa kuanza kuwekeza mapema. Fanyeni mipango yenu mapema ili masuala ya kupanda kwa gharama ya maisha yasiwe kikwazo kwenu,” akasema Pinto.

  • Tags

You can share this post!

LUGHA NA FASIHI: Tafsiri ya riwaya ‘The Alchemist’

Wauguzi wakemea visa vya kushambuliwa na jamaa wa wagonjwa...

T L