• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Hatimaye Uganda yakweza Kiswahili kuwa lugha rasmi

Hatimaye Uganda yakweza Kiswahili kuwa lugha rasmi

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya Uganda kupitisha Kiswahili kuwa moja ya lugha zake rasmi siku ya Jumanne, ni mwisho wa safari ambayo ilianza tangu enzi ya ukoloni.

Kutokana na idhini ya Jumanne ya Baraza la Mawaziri la Uganda, sasa Kiswahili kitakuwa somo la lazima katika shule za msingi na upili nchini humo.

Kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) na Mwongozo wa Kitaifa nchini humo, Dkt Chris Baryomunsi, Kiswahili pia kitakuwa miongoni mwa masomo ambayo wanafunzi watakuwa wakitahiniwa.

Je, safari ya Kiswahili kukwezwa hadi kufikia kiwango cha kutambuliwa kama lugha rasmi nchini Uganda ilianzia lini?

Wabaganda walipinga kusomeshwa Kiswahili katika shule zao wakati serikali ya kikoloni ilikuwa tayari kukuza Kiswahili.

Wakati sera ya lugha ilipobadilika dhidi ya Kiswahili kote katika Afrika Mashariki kuanzia mwaka 1950, Kiswahili kiliondolewa shuleni kwa kuwa hakikuwa tena lugha iliyotambuliwa kusomeshwa nchini Uganda.

Kuanzia mwaka wa 1925, suala la ni lugha zipi za Kiafrika zingetumiwa kusomesha katika madarasa ya awali ya shule za msingi kote nchini Uganda lilijadiliwa na serikali ya kikoloni.

Uamuzi

Kwanza, uamuzi ulitolewa kwamba Kiluganda kitumiwe katika eneo lote lililokuwa likitumia lugha za Kibantu.

Kisha, kamati ikaundwa kuchagua lugha mwafaka ya kutumia katika eneo la Kinailoti la mikoa ya Kaskazini na Mashariki.

Kamati hiyo pia ilipaswa kutayarisha tafsiri ya vitabu vya shule katika lugha zilizochaguliwa.

Kiingereza kingetumiwa kuanzia madarasa ya juu ya shule za msingi na kuendelea. Mwaka wa 1926, Idara ya Elimu iliamua kutumia lugha tatu za Kiafrika katika shule za msingi. Lugha hizo ni:

(a) Kiluganda – iliyotumiwa Buganda na sehemu ya Kaskazini ya Mkoa wa Mashariki

(b) Kiacholi – iliyotumika katika Mkoa wa Kaskazini

(c) Kiiteso – lugha iliyotumiwa katika shule za eneo la kati la Mkoa wa Kati

Uamuzi wa kusomesha Kiswahili uliafikiwa kwa sababu ya matatizo ambayo hayakuweza kutatuliwa wakati wa kutafsiri vitabu kwa lugha za Kiteso na Kiacholi.

Sababu nyingine kubwa pia ni ile athari iliyotokana na kutumiwa kwa Kiswahili katika nchi za Kenya, Tanganyika na Zanzibar.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Chimbuko na Asili ya lugha ya Kiswahili

Taasisi zinazofundisha Kiswahili ulimwenguni

T L