• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Hofu visa vya kaswende kwa wajawazito kuzidi

Hofu visa vya kaswende kwa wajawazito kuzidi

NA ANGELA OKETCH

IDADI kubwa ya wanawake wajawazito walipatikana na ugonjwa wa kaswende baada ya kupimwa Januari ikilinganishwa na miezi mingine kwa muda wa mwaka mmoja uliopita, takwimu za Wizara ya Afya zimeonyesha.

Miongoni mwa wanawake 128,767 waliohudhuria kliniki za kina mama wajawazito kote nchini, wanawake zaidi ya 4,000 walipatikana na maradhi ya kaswende, kwa mujibu wa data kwenye Mfumo wa Habari kuhusu Afya Nchini.

Hii ndiyo idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika mwaka mmoja pekee.

Idadi hiyo inawakilisha asilimia tatu ya idadi ya jumla (ya waliohudhuria kliniki hizo).

Mnamo Novemba 2021, wanawake 2,000 walipatikana na ugonjwa wa kaswende, 1,536 mnamo Septemba na katika mwezi wa Aprili, 1, 527.

Miongoni mwa wanawake 1.2 milioni waliofanyiwa uchunguzi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, 19,000 walipatikana na ugonjwa huo.

Kipindi kati ya Aprili na Juni 2021 kilikuwa na idadi ya juu zaidi ambapo wanawake 4,329 walipatikana na maradhi hayo ya zinaa miongoni mwa 328, 228 waliopimwa kikifuatiwa na miezi kati ya Julai na Septemba ambapo wanawake 4,217 walipatikana na ugonjwa huo.

Kati ya Oktoba na Disemba 2021, kulikuwa na visa zaidi ya 4,000 huku kipindi cha kati ya Januari na Machi kikiwa na visa 2,800.

Mnamo Februari, wanawake karibu 37, 117 walifanyiwa uchunguzi ambapo 700 walipatikana na ugonjwa hilo.

Kenya ilianzisha vifaa vya kupima HIV na kaswende vinavyotumiwa katika kliniki za wajawazito mnamo Machi 2018.

Kila mwanamke anayehudhuria kliniki ya wajawazito ni sharti apimwe iwapo ameambukizwa kaswende na HIV.

Mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Ukimwi (NACC) Ruth Masha. PICHA | MAKTABA

Mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Ukimwi (NACC) Ruth Masha alithibitisha kuongezeka kwa mara nyingine kwa maradhi ya zinaa licha ya kuwepo kwa tiba mwafaka na mikakati thabiti ya kuzuia maradhi hayo.

“Miongo miwili iliyopita, hatukuwa tunarekodi visa vyovyote vya kaswende, inasikitisha kuwa tunaona kurejea kwa maradhi hayo na ni sharti hatua ichukuliwe. Hii sio tu kwa wanawake wanaohudhuria kliniki za kina mama wajawazito bali miongoni mwa vijana chipukizi vilevile,” alisema.

“Hii ni hatari kwa sababu ugonjwa huo ndio chanzo cha pili kikuu zaidi kinachosababisha visa vya watoto kuzaliwa kabla ya wakati duniani. Hata ikiwa ni mama mmoja anayepatikana na maradhi hayo ni sababu tosha ya kuzua wasiwasi,” alisema.

Visa vya maambukizi ya kisonono miongoni mwa vijana chipukizi vilipanda kwa asilimia 28 ambapo kaunti zenye idadi kubwa ya HIV ziliandikisha idadi kubwa zaidi ya visa.

Hii ina maana kuwa wasichana wawili miongoni mwa kumi waliofanyiwa vipimo wanaugua kisonono.

Kisonono ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria na uliwahi kusahaulika kabisa wakati mmoja lakini sasa umeibua wasiwasi miongoni mwa wahudumu wa afya wanaojikakamua kuhakikisha umeangamizwa kabisa hasa mingoni mwa wajawazito.

You can share this post!

HADITHI FUPI: Majibu kwa maswali ya ‘Shibe Inatumaliza’

Museo aghairi nia, sasa kutetea cheo chake uchaguzini

T L