• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Huenda Uhuru asiweze kudhibiti ‘Rais Raila’

Huenda Uhuru asiweze kudhibiti ‘Rais Raila’

NA LEONARD ONYANGO

MPANGO wa Rais Uhuru Kenyatta kutaka kudhibiti serikali ya kinara wa ODM Raila Odinga iwapo atachaguliwa kuwa rais Agosti 9, huenda ukagonga mwamba, wadadisi wameonya.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Rais Kenyatta analenga kutumia vyama vilivyo ndani ya muungano wa Azimio la Umoja kuhakikisha kuwa anakuwa na usemi katika serikali ya Bw Odinga.

Chama cha Jubilee kimetia saini mkataba wa ushirikiano na zaidi ya vyama 20 na Rais Kenyatta atakuwa msemaji wa vyama hivyo ndani ya muungano wa Azimio la Umoja.

Lengo la Rais Kenyatta, kulingana na Bw Kioni, ni kuwa na wabunge wengi watakaotetea masilahi yake serikalini.

Miongoni mwa vyama vilivyotia saini mkataba wa maelewano na Jubilee ni Party of National Unity (PNU) kinachoongozwa na waziri wa Kilimo Peter Munya, Pamoja African Alliance (PAA) chake Gavana wa Kilifi Amason Kingi, Kenya Union Party (KUP) cha Gavana wa Pokot Magharibi chake John Lonyangapuo, United Progressive Alliance (UPA) na Democratic Action Party (DAP) chake waziri wa Maji Eugene Wamalwa.

Naibu wa Rais William Ruto amekuwa akidai kuwa vyama hivyo vinafadhiliwa na Rais Kenyatta kwa lengo la kugawanya kura kwa misingi ya kikabila.

Ushawishi wa Rais Kenyatta umemwezesha Bw Odinga kujipatia uungwaji mkono mkubwa katika kaunti 11. Kaunti ambazo Bw Odinga huenda akavuna kura nyingi kutokana na uhusiano wake wa karibu na Rais Kenyatta ni Garissa, Mandera, Wajir, Marsabit, Isiolo, Nyamira, Kajiado, Narok, Samburu na Pokot Magharibi.

Chama cha Jubilee, hata hivyo, kinataka ODM kutosimamisha wawaniaji katika kaunti hizo, Nairobi na maeneo ya Mlima Kenya ili kukiwezesha kupata idadi kubwa ya wabunge.

Lakini wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa huenda Rais Kenyatta akakosa idadi wabunge itakayomwezesha kudhibiti serikali ya Bw Odinga ikiwa atafanikiwa kuingia Ikulu baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

“Ushawishi wa Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya ni mdogo sana. Hivyo uwezekano wa chama cha Jubilee kupata angalau nusu ya wabunge kutoka eneo hilo ni mfinyu mno,” anasema Bw Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Eneo la Mlima Kenya lina zaidi ya wabunge 50 ambao wengi wao huenda wakachaguliwa kupitia tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu wa Rais William Ruto.

“Ni sawa na mchezo wa patapotea kwa Rais Kenyatta kuweka matumaini yake kwa wabunge wa vyama vingine. Atakuwa na usemi zaidi ikiwa chama chake cha Jubilee kitakuwa na idadi kubwa ya wabunge,” anasema Bw Bigambo.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa Bw Odinga kumsaliti Rais Kenyatta akishinda Uchaguzi Mkuu ujao.

Bw Musyoka anasema kuwa huenda Bw Odinga akaiga Rais wa Jamhuri ya Kidemokraia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi aliyemsaliti mtangulizi wake Joseph Kabila licha ya kumsaidia kuingia mamlakani mnamo 2019.

Chama cha Kabila cha Common Front for Congo (FCC) kilidhibiti asilimia 75 ya wabunge katika Bunge la DRC hivyo kulazimisha Rais Tshisekedi kuungana naye ili kuunda serikali.

Lakini miaka miwili baadaye, Rais Tshisekedi alifanikiwa kushawishi wabunge wa chama cha FCC kumuunga mkono – hatua iliyomsaidia kutimua waziri mkuu Sylvestre Ilunga Ilunkamba ambaye alikuwa mwandani wa Kabila.

“Labda uwe kiongozi mcha Mungu kama Kalonzo, mtu yeyote anayeingia mamlakani anaweza kubadilika. Rais Kenyatta ambaye atakuwa mstaafu huenda akatakiwa kutuma ombi la kutaka kukutana na Rais mwezi kabla,” anasema Bw Musyoka.

  • Tags

You can share this post!

Mbona Uhuru hampigii debe Raila Mlimani?

Mchujo: ODM yazidi kujiponza

T L