• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:43 AM
Mbona Uhuru hampigii debe Raila Mlimani?

Mbona Uhuru hampigii debe Raila Mlimani?

NA CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amewaacha wakereketwa wa vuguvugu la Azimio la Umoja na maswali mengi kuhusu ni kwa nini hajajitokeza wazi wazi kumfanyia kampeni Raila Odinga katika eneo la Mlima Kenya.

Hii ni licha ya kuahidi kufanya hivyo alipohutubia makongamano ya kitaifa ya wajumbe (NDCs) vyama vya Jubilee na ODM mnamo Februari 26 mwaka huu jijini Nairobi.

“Baada ya hapa tutazunguka na ndugu Raila sehemu mbalimbali nchini ili tuwaeleze ni kwa nini wanfaa kuunga mkono Azimio la Umoja. Lakini ningependa kuwahakikishia kuwa tutatembea na wale wote wenye maono sawa na yetu ya kuunganisha taifa hili,” Rais Kenyatta akasema katika kongamano la Jubilee katika jumba la KICC.

Alikariri kauli hiyo saa moja baadaye alipowahutubia wafuasi wa Bw Odinga alipohudhuria kongamano la ODM katika uwanja wa Kasarani akieleza kuwa lengo lake ni kuacha taifa lenye umoja na uthabiti.

Rais Kenyatta alisema hayo siku mbili baada ya kuongoza mkutano wa viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya katika Ikulu ndogo ya Sagana, Nyeri, ambapo kwa mara ya kwanza, alitangaza wazi kuwa anamuunga mkono Bw Odinga kuwa mrithi wake.

“Sasa tumefurahi kwamba Rais Kenyatta ametupa mwelekeo kuhusu mkondo wa kisiasa ambao angetaka sisi kama wakazi wa Mlima Kenya kufuata. Ningependa kuwahakikishia kuwa tutajitosa uwanja kumfanyia kampeni Bw Odinga katika eneo hili ili kuzima wimbi la chama cha UDA katika eneo hili,” Bw Wambugu akanukuliwa akisema.

Lakini karibu mwezi mmoja baada ya mkutano huo wa Sagana 3 na makongamano ya wajumbe wa vyama vya Jubilee na ODM, Rais Kenyatta hajajitokeza waziwazi kumfanyia kampeni Bw Odinga, haswa katika eneo la Mlima Kenya lenye jumla ya wapiga kura 5.8 milioni.

Hii ni licha ya kufaulu kumvuta kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka upande wa Bw Odinga hadi kigogo huyo wa siasa za Ukambani akakubali kuweka kanda ndoto yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

MIKAKATI

Wadadisi wa masuala ya kisiasa sasa wanasema Rais Kenyatta amechelea kujibwaga uwanjani katika eneo la Mlima Kenya kumfanyia Bw Odinga kampeni baada ya mikakati yake ya kudhibiti wimbi la chama cha UDA eneo hilo kufeli.

“Rais amegundua kuwa hata baada ya yeye kumwidhinisha Raila katika mkutano wa Sagana III na katika makongamano ya Jubilee na ODM, wakazi wa Mlima Kenya wameendelea kumkaidi kwa kushabikia mrengo wa Dkt Ruto. Viongozi ambao aliwatwika wajibu wa kwenda mashinani kudhibiti mawimbi ya UDA wamemfeli,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Barrack Muluka.

Mnamo Januari mwaka huu, Rais Kenyatta alikutana na wabunge wandani wake kutoka Mlima Kenya na kuwaagiza kuendesha kampeni kabambe ya kuvumisha chama cha Jubilee katika kaunti zote 10 za eneo pana la Mlima Kenya.

Kaunti hizo ni; Kiambu, Murang’a,

Nyeri, Laikipia, Embu, Nakuru, Meru, Nyandarua, Tharaka Nithi na Kirinyaga.

Lakini baada ya kufanya mikutano michache katika maeneo hayo wabunge hao, kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na mkurugenzi wa uchaguzi katika Jubilee Kanini Kega wamekimya.

“Chama cha UDA kinaendelea kupata umaarufu katika eneo hili la Mlima Kenya kwa sababu viongozi ambao Rais Kenyatta aliwapa wajibu wake kuvumisha Jubilee wamezembea. Tangu wapewe kibarua hicho Jubilee imeendelea kusalia mahame baada ya wanasiasa kuigura na kujiunga na Jubilee. Hii ndio maana Rais amechelea kufanya mikutano ya kampeni kumuuza Raila,” akasema James Mwangi ambaye anagombea kiti cha ubunge cha Starehe, Nairobi kwa tiketi ya Jubilee.

Kwa mfano, wiki jana, wanasiasa kadha wa Jubilee na wale wa vyama vingine vidogo kutoka eneo la Mlima Kenya walijiunga na kambi ya Dkt Ruto, hali ambayo iliwavunja moyo wapanga mikakati katika kambi ya Azimio la Umoja.

Kwa mfano, Seneta wa Kiambu Kimani Wa Matangi na mwenzake wa Embu Njeru Ndwiga waligura chama cha Jubilee na kujiunga na UDA katika mkutano ulioongozwa na Dkt Ruto mjini Thika mnamo Machi 13, 2022.

Aidha, ni katika mkutano huo kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) Mwangi Kiunjuri, Moses Kuria (Chama cha Kazi) na William Kabogo (Tujibebe Party) walitangaza kuunga mkono azma ya urais ya Dkt Ruto chini ya mwavuli wa muungano wa Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Jubilee yazidi kuvuna Mlimani

Huenda Uhuru asiweze kudhibiti ‘Rais Raila’

T L