• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
HUKU USWAHILINI: Usishangae kuona tukichakata ubongo kupita kiasi Uswahilini

HUKU USWAHILINI: Usishangae kuona tukichakata ubongo kupita kiasi Uswahilini

NA SIZARINA HAMISI

USWAHILINI kuna mengi ambayo wale wasioishi huku wanaweza wasielewe.

Kikubwa huku kwetu ni matumizi makubwa ya akili katika shughuli zetu za kila siku.

Kwamba harakati za huku kwetu zimetufanya ubongo uende mwendo mkali wakati mwingine kupita uwezo wake. Ukiishi Uswahilini huwa ni muhimu kutumia akili katika kupanga maisha.

Huku kwetu kila ukionacho ni zao la kuchakata ubongo, kuanzia mtu anapoamka asubuhi hadi anapoenda kulala usiku. Na mojawapo ya matumizi ya akili ni katika maisha ya ndoa na hata kwa wale wapendanao.

Tunajua baadhi ya akina dada ni wataalamu wa kuchovya na kuonja, ndiposa waume wengi wamekuwa wakitumia akili za ziada kuhakikisha kwamba mali zao hazikaguliwi na wajanja hao.

Mfano ni huyu jirani yangu ambaye tunajua tabia yake kwamba kila mkewe akirudi jioni lazima afanye ukaguzi wa kitaalamu kwa kutumia akili. Kwamba hatumii mabavu wala lugha kinzani bali anatumia mbinu kuhakikisha ukaguzi unafanyika ili kujua iwapo vivuruge wameshavuruga kisima cha mwenyewe.

Katika hizi harakati tumewaona wanaume ambao wameruhusu mawazo yao yakimbie mwendo kasi kwenye njia yenye mabonde na kona. Wengi tumewaona wameharibu ndoa na wengine wameachana na wapenzi wao kwa kutozuia kasi ya akili zao.

Huu mwenendo wakati mwingine umekuwa ukishangaza hasa tunapoona na kusikia baadhi ya wanandoa wanaishi kwa kupelelezana kila siku kama askari wakaguzi wa dawa za kulevya.

Harakati hizi huvuka mipaka wakati mwingine kiasi kwamba tunawajua wanaoweka wapelelezi uchwara wakiwepo madereva wa bodaboda ili kufuatilia mke ama mume ameenda wapi na amefanya kitu gani. Ili anaporudi jioni, vumbi linatifuka kiasi cha kukosa mtatuzi.

Inapofikia hatua kama hii, ndiposa wale wenye busara hushauri na kuzungumza na wanaotumia akili kupindukia kuhusu umuhimu wa kulegeza mwendo wa akili na wakati mwingine kufumba macho na kuacha mengine yapite.

Huwa tunashauriana kwamba wakati mwingine unaweza kuamua kujisemea hutawaza sababu ya jambo ambalo halina suluhu. Na huwa tunafanya hivi kwani tunajua ni sawa na dereva anayeendesha gari lenye injini yenye kasi kubwa lakini ameamua kwa makusudi tu kupunguza mwendo kwa usalama wa maisha yake.

Huwa tunasema funika kombe, mwanaharamu apite, kwani wakati mwingine hizi akili zetu tunazozichakata kupita kiasi huwa zinatuletea shida.

[email protected]

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Morgan Freeman na Jung Kook...

Mwili wa mlinzi wapatikana ndani ya darasa

T L