• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Morgan Freeman na Jung Kook wanogesha sherehe za ufunguzi ugani Al Bayt

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Morgan Freeman na Jung Kook wanogesha sherehe za ufunguzi ugani Al Bayt

Na MASHIRIKA

FAINALI za Kombe la Dunia 2022  zilianza Jumapili kwa sherehe za ufunguzi zilizotamalakiwa na mbwembwe za kila sampuli ugani Al Bayt kabla ya mechi ya kwanza ya mashindano hayo kati ya wenyeji Qatar na Ecuador.

Mwigizaji maarufu wa Amerika, Morgan Freeman alinogesha sherehe hizo pamoja na mwanaYouTube wa Qatar, Ghanim Al-Muftah.

Mwanamuziki mashuhuri wa mtindo wa pop kutoka Korea Kusini, Jung Kook alitumbuiza mashabiki akishirikiana na mwimbaji wa Qatar, Fahad Al Kubaisi katika uwanjani huo ulioko mjini Al Khor.

Dakika 90 kabla ya kupulizwa kwa kipenga cha kuashiria mwanzo wa michuano ya Kombe la Dunia, Freeman ambaye ni mshindi wa tuzo ya Oscar, alisimulia kwa video jinsi kandanda ilivyo na uwezo wa kuunganisha dunia.

Maandalizi ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika nchi ya Kiislamu iliyoko Mashariki ya Kati yametawaliwa na mizozo ya kadhaa, ikiwa ni pamoja na vifo vya wafanyakazi wahamiaji na kubaguliwa kwa wasagaji na mashoga (LGBT) nchini Qatar.

Akitumbuiza hadhira kwa mara ya kwanza, Freeman alipokelewa kwa shangwe na vifijo alipojitokeza uwanjani na Al Muftah aliyezaliwa na ugonjwa nadra au tatizo la ‘Caudal Regression Syndrome’.

“Kila mmoja anakaribishwa,” Freeman aliuambia umati.

Tumbuizo moja liliangazia matembezi ya timu 32 zinazoshiriki mashindano ya mwaka huu na vinyago vya Kombe la Dunia lililopita pamoja na maskoti.

Jung Kook na Fahad Al Kubaisi walitumbuiza pamoja kabla ya Emir Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani kutoa hotuba ya ufunguzi kwa Kiarabu.

Mrithi wa utawala wa Saudi Arabia na marais wa Misri, Uturuki na Algeria pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, walikuwa miongoni mwa viongozi wa dunia katika uwanja huo wenye umbo la hema kabla ya mechi ya ufunguzi.

Sherehe hizo za dakika 30 zilikamilika kwa fataki kulipuliwa na ngoma kupigwa kabla ya wanasoka wa Qatar na Ecuador kushuka ugani kupasha misuli moto.

Baada ya panda-shuka, tetesi za kila aina na mashaka, hii ilikuwa fursa maridhawa kwa Qatar kukaribisha ulimwengu na kuwasilisha hoja yake kwa hadhira ya mabilioni ya watu duniani kote.

Licha ya kuwa sehemu ya mbali na katikati ya jangwa lisilo na watu, uwanja wa Al Bayt ulitoa mazingira mazuri kwa ufunguzi wa Kombe la Dunia ambalo ni ghali na lenye utata zaidi katika historia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MALEZI KIDIJITALI: Athari mseto za matumizi ya dijitali kwa...

HUKU USWAHILINI: Usishangae kuona tukichakata ubongo...

T L