• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Jamaa anayetembea na nyuki kichwani Murang’a aomba ufadhili wa mizinga 10, 000  

Jamaa anayetembea na nyuki kichwani Murang’a aomba ufadhili wa mizinga 10, 000  

NA SAMMY WAWERU

MWANAMUME eneo la Kigumo, Murang’a anayetembea na nyuki waliomzingira kichwani ameomba viongozi wa kaunti hiyo kumsaidia kununua mizinga ili kugeuza wadudu hao kuwa kitega uchumi.

Kupitia video inayosambaa mitandaoni, barobaro huyo anaskika akizungumza kwa lugha ya Agikuyu akisema “kuwa na nyuki ni talanta yangu”.

Akishirikishwa kwenye maswali na baadhi ya watu barabarani, anasema matamanio yake maishani ni kumiliki mizinga.

“Mheshimiwa wetu Munyoro (mbunge wa Kigumo Joseph Munyoro), na Diwani (MCA), si waungane wanipe mizinga kadhaa ya nyuki nijivunie kuwa kijana wa Murang’a. Sina mahali pa kuwaweka,” anasema.

Wanaomdadisi wanaskika wakitaka kujua sehemu ambayo atapeleka wadudu hao hatari japo wenye thamani kutokana na uzalishaji asali.

“Utawapeleka wapi?” mmoja wao anaulizia. Naye anajibu, “Labda niwaambie wapae.”

“Hawatavamia mtu mwingine?” maswali yanazidi kuulizwa.

Kulingana naye, atawaamuru waende wajenge ‘makao’ mahali kichakani na kwamba hawataenda kwa mtu yeyote.

Cha kushangaza zaidi ni kwamba mwanamume huyo anasema bumba la nyuki anaotembea nao hawajawahi kumdunga wala kumvamia.

“Nimetakaswa…Mungu yupo,” anaelezea, akisababisha watu kuangua kicheko.

Akiwa amebeba mzigo, nyuki wanaonekana wamemzingira kuanzia kisogo, kuelekea mashavuni, kwenye kidevu na shingoni.

“Naomba nipewe mizinga na hawa viongozi wetu, wainue na kupiga jeki talanta yangu. Sawa na vijana wanaocheza soka wanavyopewa mipira, nami pia nikabidhiwe mizinga,” anaomba.

“Hiki kipaji changu kiinuliwe kama cha wale wengine…Nikipewa mizinga 10, 000 nitafurahia sana,” anaendelea kueleza.

Aidha, jamaa huyo mkakamavu na jasiri kutoka Murang’a anakiri ana uwezo kuwaagiza waingie kwenye mzinga.

Huku wanaomdadisi kwa maswali wakiahidi kuzungumza na viongozi wa Kaunti ya Murang’a, mwanamume huyo anasema tamanio lake ni kukutana na Gavana Irungu Kang’ata akisisitiza mamlaka ya nyuki ndiyo ajira yake.

Kwenye mazungumzo na wadadisi wake, inafichuka kwamba ametumika mara kadha kufukuza nyuki wanaovamia makazi ya watu.

Murang’a ni mojawapo ya kaunti nchini zenye vituko na sarakasi.

Si mara moja, mbili, au tatu, vioja kuripotiwa humo.

 

  • Tags

You can share this post!

MCAs wa Nyeri ndio nambari moja katika uchapakazi, utafiti...

Simu ya mume ni sawa na kitunguu, itakuweka machozi,...

T L