• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Dalili Gachagua sasa anajipanga kulinda nafasi yake katika Kenya Kwanza

Dalili Gachagua sasa anajipanga kulinda nafasi yake katika Kenya Kwanza

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameonekana kuanza kujipanga kisiasa kwa kujiweka katika nafasi bora ya kuibuka kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya na kulinda nafasi yake katika serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Gachagua amechukua hatua bayana za ‘kujilinda’ kwa kuunganisha eneo la Mlima Kenya nyuma yake huku ishara zikijitokeza kuwa Rais William Ruto anayachangamkia maeneo mengine nchini katika juhudi za kuzidisha umaarufu wake.

Bw Gachagua amehakikisha kuwa eneo la Mlima Kenya linaungana yeye akiwa kiongozi huku akiapa kuunganisha viongozi wote wakiwemo waliounga Upinzani kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Kabla ya Rais Ruto kufanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri mwezi jana, Bw Gachagua alitangaza kuwa angemtafuta Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ili waridhiane akisema lengo lake ni kuhakikisha eneo la Kati litampa Dkt Ruto asilimia 80 ya kura kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Rais Ruto alimpandisha hadhi Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kwa kumuongezea wizara ya Mashauri ya Kigeni, hatua iliyoonekana kupunguza ushawishi wa Gachagua serikalini.

Naibu Rais amekutana zaidi ya mara tatu na viongozi wa eneo la Kati ili kuweka mikakati ya kuunganisha ngome yake ambayo wadadisi wanasema Rais Ruto ni maarufu zaidi Mlimani kumshinda.

“Tunaona Gachagua mpya kisiasa; ameacha kumshambulia Bw Uhuru Kenyatta na familia yake na anahubiri maridhiano. Hizi ni dalili za kujipanga kwa kuwa katika Mlima Kenya, Dkt Ruto anamshinda kwa umaarufu,” asema mdadisi wa siasa Dkt David Gichuki.

Aidha, ameonekana kufaulu kumshawishi aliyekuwa kiongozi wa Mungiki, Bw Maina Njenga kumuunga mkono.

Duru za kuaminika zinasema wawili hao waliafikiana kushirikiana kwa sharti kuwa Bw Njenga asiandamwe tena na serikali.

Mnamo Jumamosi Oktoba 21, 2023, Bw Gachagua alikutana na viongozi wa eneo la Mlima Kenya mjini Nyeri katika hafla ya mchezo wa gofu ambayo wito wa umoja wa Mlima Kenya ulipigiwa chapuo.

Alizungumza Jumamosi hiyo usiku akiwa Nyeri Golf Club ambapo alikuwa ameandaa mkutano na wafanyabiashara, wasomi na viongozi kutoka Mlima Kenya. Mkutano huo ulilenga kuonyesha kuwa eneo hilo linaunga mkono utawala wa Rais Ruto. Bw Gachagua alikuwa mdhamini wa tamasha la Gofu ya Mlima Kenya ambalo ililenga kuwaleta pamoja wanasiasa wote wa Mlima Kenya.

Bw Gachagua alisema kuwa ataendelea kuzungumza na viongozi wa Azimio la Umoja kutoka Mlima Kenya ili kuwarai waunge mkono ajenda ya maendeleo ya Dkt Ruto. Dkt Gichuki anasema lengo la Bw Gachagua ni kuongeza usemi wake katika serikali.

“Kama mwanasiasa, ukiwa maarufu katika ngome yako, unakuwa na usemi kitaifa. Anachofanya Bw Gachagua ni kuongeza umaarufu wake eneo la Mlima ili aweze kuwa na nguvu zaidi kitaifa sasa na siku zijazo,” akasema.

Mchambuzi wa siasa Michael Odero anasema Gachagua aligundua kuwa hawezi kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya likiwa limegawanyika.

“Kugawanyika kwa Mlima Kenya kunaweza kuwa pigo kwa Bw Gachagua na anaonekana kugundua hilo mapema na kuanza kujipanga mapema,” asema Bw Odero.

Inasemekana mbali na mkutano wa Jumamosi, Bw Gachagua anapanga mikutano na makundi mengine, wakiwemo wazee wa jamii za Mlima Kenya huku akionekana kupunguza madai yaliyozua mgawanyiko nchini ya Kenya ni kampuni.

“Rais na mimi tunataka watu wote wazungumze lugha moja ambayo ni maendeleo bila kumpuuza mtu yeyote. Sisi sote tunastahili kuwa na mwelekeo mmoja ambao ni maendeleo,” akasema.

Rais Ruto alionekana kutofautiana na Bw Gachagua hivi majuzi kuhusu mgao wa rasilimali za kitaifa huku akisema hakuna eneo linalostahili kusalia nyuma kwa kuunga mkono Upinzani.

Akizungumza kwenye eneobunge la Ugenya, Kaunti ya Siaya wakati alipozuru Nyanza, Rais aliahidi kufanya kazi na maeneo yote kwa sababu “hata raia wa maeneo hayo wanalipa ushuru”.

“Mtu asiwaambie kuwa mpo nje ya serikali hii kwa sababu mnalipa ushuru na nyinyi ni Wakenya. Hii ni serikali yenu na sitaruhusu eneo lolote la Kenya libaguliwe kimaendeleo kutokana na miegemeo yao ya kisiasa,” akasema Rais Ruto.

Juhudi zake zinaonekana kuzaa matunda huku wataalamu na wafanyabiashara kutoka Mlima Kenya wakizichangamkia.

Mwenyekiti wa 1010 Group Foundation, Dkt John Kinyua, alisema kaunti 10 za eneo la Mlima Kenya zitapoteza pakubwa iwapo halitaungana.

  • Tags

You can share this post!

Vyama 38 vipya mbioni kusajiliwa kupigania mabilioni kutoka...

Jinsi walinzi wa Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Serikali...

T L