• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Jinsi walinzi wa Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Serikali walivyomuangamiza mwanamume aliyewavamia barabarani

Jinsi walinzi wa Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Serikali walivyomuangamiza mwanamume aliyewavamia barabarani

KITAVI MUTUA na LABAAN SHABAAN

WALINZI wawili wa mshauri wa Rais William Ruto kuhusu Usalama wa Kitaifa, Monica Juma, walishambuliwa Jumamosi usiku katika barabara kuu ya Mwingi – Garissa.

Ilibidi polisi hao wa kijeshi kufyatua risasi waliposimamishwa ghafla na mtu mwenye bunduki karibu na soko la Nguni kwenye eneo lenye upweke.

Mshambuliaji huyo anaaminika kuwa raia wa nchi nyingine.

Lakini, Dkt Juma, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi katika serikali ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, hakuwemo garini.

Kulingana na ripoti ya tukio hilo (OB) katika kituo cha polisi cha Nguni, walinzi hao wawili waliojihami kwa bastola, walikuwa wakisafiri kutoka Nairobi kuelekea Nuu, Mwingi Mashariki – nyumbani mwa Dkt Juma.

Maafisa hao walisema kuwa walidhani mshambulizi huyo alikuwa mmoja wa genge kubwa lililojificha gizani.

Wanaeleza kuwa waliamuriwa kutoka garini ambapo waliporwa vitu vyao huku wakitishwa kwa bunduki.

Inaripotiwa, alipokuwa anatoroka, mshambuliaji huyo alifyatua risasi tatu na kufanya polisi kujibu kwa kumpiga risasi akafa papo hapo.

Walipopekua begi lake, maafisa hao walipata sarafu za Somalia, vyakula, paneli ya jua na risasi 38 zilizohifadhiwa katika begi dogo jeusi.

Mshambuliaji huyo alikuwa na bunduki aina ya AK47 na risasi 23.

“Vifuatavyo vilipatikana kwake: jozi mbili za viatu wazi, sufuria ndogo zenye chakula, kisu, paneli ya jua, makasi, batri kavu 15, kalamu na kifaa cha kupima umeme,” Ripoti ya OB ilionyesha.

Wapelelezi wa Kitui wanajaribu kumtambua mshambuliaji huyo na jinsi alifaulu kutisha madereva kwa siku nyingi akijificha msituni.

Mapema kabla ya tukio, jambazi huyo alishambulia lori la maji la shule ya St Andrews, Mwingi ambapo alimiminia lori hilo risasi.

Dereva wa lori, Bw Patrick Mutie, aliambia polisi kuwa alipomwona mshambulizi mwenye bunduki akimwambia asimame, aliongeza kasi.

Japo tairi lake lilipigwa risasi, Bw Mutie anasema aliendelea na safari kwa gurudumu bovu hadi alipofika soko la Nguni.

Mwili wa mshambuliaji huyo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mwingi Level Four upelelezi ukiendelea.

  • Tags

You can share this post!

Dalili Gachagua sasa anajipanga kulinda nafasi yake katika...

Hofu fisi wakizurura vijijini

T L