• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Jinsi Uhuru anavyolenga kupangua mahesabu ya Ruto

Jinsi Uhuru anavyolenga kupangua mahesabu ya Ruto

HUENDA Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akaendelea kushawishi siasa za nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, na kugeuka kizungumkuti tena kwa Kenya Kwanza.

Hii ni baada ya kiongozi huyo kukariri kuwa atasalia mwanachama wa Azimio la Umoja One-Kenya na kuhimiza viongozi wa muungano huo kuungana “kwani nyota yetu ya kisiasa itaendelea kung’aa.”

Akiongea Jumapili, Novemba 19, 2023 katika mji wa Mwingi Kaunti ya Kitui, Bw Kenyatta alielezea matumaini kuwa upinzani bado una nafasi ya kuunda serikali ijayo.

“Mimi ni mwanachama wa Azimio na ninasema hivyo wazi, msimamo wangu haujabadilika. Tuko mahala tulipo na hatubanduki kwa sababu ninaweza kuona mustakabali mzuri kwetu,” rais huyo mstaafu akawaambia waumini wa Kanisa la Full Gospel alikoongoza hafla ya kuchanga fedha.

Alipokelewa na mwenyeji wake, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye ni mmoja wa vinara wa Azimio, pamoja na viongozi wakuu wa kisiasa kutoka eneo zima la Ukambani.

Vyama vingine tanzu katika muungano huo wa upinzani ni Jubilee kinachoongozwa na yeye, Bw Kenyatta, ODM inayoongozwa na Raila Odinga, Narc Kenya yake Martha Karua, chama cha Democratic Action Party-Kenya (DAP-K) chake aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa miongoni mwa vingine.

Bw Kenyatta ndiye mwenyekiti wa Baraza Kuu la Azimio huku Bw Odinga akiwa kiongozi wa muungano huo.

Akijibu miito ya viongozi wa Ukambani kwamba aunge mkono azma ya urais ya Bw Musyoka mnamo 2027 Bw Kenyatta alijibu hivi: “Nimesikia yale yote mliyosema. Nani ajuaye, ni Mungu tu”.

“Nitaendelea kuzungumzia masuala yenye umuhimu wa kitaifa yanayowaathiri Wakenya kama vile kupanda kwa gharama ya maisha.

Na hawa watu wakome kunilaumu kwa changamoto hizi kwa sababu huu ni wakati wao kuendesha masuala ya nchini huku wakishughulikia matatizo yanayowakumba Wakenya,” Bw Kenyatta.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa tuliozungumza nao wanasema kuwa jibu la Bw Kenyatta, kwa ombi la viongozi wa Ukambani kwamba aunge mkono Bw Musyoka, linaashiria wazi kwamba bado yu tayari kushiriki katika siasa kwa kuunga mkono mgombeaji wa urais atakayeteuliwa na Azimio.

“Uhuru alionyesha wazi kuwa japo amestaafu kama Rais, hajastaafu kama mwanasiasa na kwamba Wakenya wawe tayari kuendelea kuhisi ushawishi wake katika ulingo wa siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027,” anasema Bw Martin Andati.

Kulingana Bw Andati, usemi wa Bw Kenyatta mjini Mwingi wiki jana ulilenga kutoa onyo kwa Rais William Ruto serikali yake ya Kenya Kwanza kwamba Azimio inalenga kutumia mapungufu yake kujinadi tena kwa raia ili imwondoe mamlakani katika uchaguzi mkuu ujao.

“Kwa kudokeza kuwa yuko radhi kuunga mkono Bw Musyoka katika kinyang’anyiro cha urais 2027, Bw Kenyatta anamwambia Ruto kwamba kando na Raila kuna vinara wengine katika Azimio ambao wanaweza kupambana naye,” anaeleza.

Kupanda kwa gharama ya maisha kutokana na baadhi ya sera za serikali ya Rais Ruto, kama vile kupandishwa kwa aina mbalimbali za ushuru, kumedororesha imani ya wengi wa Wakenya kwa serikali hii.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke aliyetishia kudunga kisu mjakazi akishuku...

EL-NINO: Serikali yaahidi bei ya umeme itapungua hivi...

T L