• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:17 PM
EL-NINO: Serikali yaahidi bei ya umeme itapungua hivi karibuni

EL-NINO: Serikali yaahidi bei ya umeme itapungua hivi karibuni

NA WINNIE ONYANDO

BEI ya umeme nchini huenda ikapungua katika miezi michache ijayo.

Waziri wa Nishati na Petroli, Davis Chirchir, Jumamosi Novemba 25, 2023 alisema mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo ya vyanzo vya Mto Tana imefanya maji kujaa katika Mabwawa ya Seven Forks ambayo imefanya uzalishaji wa umeme nchini kuwa rahisi.

Waziri huyo alisema mchango wa joto katika uzalishaji wa nishati nchini umepungua hadi takriban asilimia 4 huku mabwawa yakizalisha MW 498 ambayo inaweza kuongezwa zaidi katika siku zijazo kwa kuleta mkondo wa 40MW wa kituo cha umeme cha Masinga.

Alifichua kwamba uzalishaji wa umeme katika hifadhi kuu ya Seven Forks, Masinga, umezimwa kwa sasa wakati Kengen ikijaribu kujenga hifadhi ya maji.

Waziri huyo alikuwa akizungumza katika eneo la Masinga baada ya kukagua kiwango cha maji katika mabwawa ya Seven Fork akiandamana na Mbunge wa Garissa Dekow Mohamed, Katibu Mkuu wa Nishati Alex Wachira na Mkurugenzi Mtendaji wa Kengen Peter Njenga.

Kwa upande mwingine, Waziri Chirchir aliongeza kuwa kabla ya mvua kunyesha, viwango vya maji katika Seven Forks vilipungua na kupunguza uwezo wa kuzalisha umeme kwa asilimia 30 ambayo sasa imepanda hadi takriban asilimia 82.

Alisema kuwa serikali imeanza mchakato wa kuboresha bwawa la Grand Falls lililopendekezwa kwa muda mrefu katika Kaunti ya Tharaka Nithi ili kudhibiti maji kutoka kwenye mito ya Meru.

Naye Bw Wachira alisema watakuwa wakiwahamasisha wakazi eneo hili kuhusu maendeleo mapya serikali inapanga kuanzisha.

Aliwashauri wakazi wa kaunti za Garissa na Tana River kuwa waangalifu na kuwa tayari kuhama wanaposhauriwa.

Kwa upande wake, Bw Njenga alisema mabwawa hayo kwa pamoja yanazuia takriban nusu ya mtiririko wa Tana ambao ungeweza kusababisha uharibifu mkubwa.

Alisema bwawa la pili katika mteremko wa Kamburu, lilitarajiwa kujaa baada ya siku tatu.

Hata hivyo, Bw Mohamed alisema kuwa mabwawa hayo hayajajaa kwani mafuriko yanayoshuhudiwa katika maeneo karibu yanatokana na maji ya mito inayotoka Meru upande wa Mlima Kenya na kuungana na mto Tana.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi Uhuru anavyolenga kupangua mahesabu ya Ruto

Wakenya kuendelea kuumia Kamati ya Kitaifa kuhusu...

T L