• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 5:50 AM
KIGODA CHA PWANI: Jinsi mkono wa Joho utakoroga kampeni za ugavana Mombasa

KIGODA CHA PWANI: Jinsi mkono wa Joho utakoroga kampeni za ugavana Mombasa

Na PHILIP MUYANGA

HATUA ya Gavana Hassan Joho kuashiria kumuunga mkono Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir kuwania ugavana Mombasa huenda ikabadili mwelekeo wa kampeni za kiti hicho hasa za kusaka tikiti ya chama cha ODM.

Kando na Bw Nassir, tikiti hiyo ya ODM inawaniwa na mfanyabiashara Suleiman Shahbal na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi.

Bw Joho huandamana na mbunge huyo kwa shughuli nyingi za kisiasa na maendeleo Pwani na hivyo kuibua hisia baina ya wadadisi wa kisiasa kwamba anamwandaa kutwaa uongozi.

Hivi majuzi, wawili hao walikuwa pamoja katika hafla ya kuzindua karakana ya meli inayosimamiwa na jeshi la ulinzi wa Kenya (KDF) katika eneobunge la Likoni, Kaunti ya Mombasa.

Hafla hiyo iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ilihudhuriwa pia na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Baadaye, waliandamana kwa mikutano mingine tofauti ukiwemo ule wa kuwasha taa ya Krismasi katika eneo la Treasury Square kisha kwa mkutano wa wazee waliotoka kaunti ndogo za Mombasa kupigia debe Azimio la Bw Odinga kuwania urais katika uchaguzi ujao.

Ni katika hafla ya Treasury Square ambapo Bw Joho alitoa matamshi yaliyofasiriwa na wengi kuwa ishara tosha kwamba anaunga mkono azimio la Bw Nassir, aliposema utawala wake ulioanza mwaka wa 2013 tayari umeonyesha mwelekeo wa uongozi unaofaa kufuatwa katika uchaguzi ujao.

Gavana huyo alisema hayo alipozungumza baada ya hotuba za wanasiasa wengine waliomtaka amuunge mkono Bw Nassir.

Gavana Hassan Joho akizungumza na Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir aliyetangaza azma ya kuwania ugavana Mombasa. PICHA | MAKTABA

Kwa mujibu wa wadadisi wa kisiasa, uamuzi wa Bw Joho utakuwa na uzito kwa kuwa yeye ni naibu kiongozi wa ODM na pia bado anaaminika kuwa na ushawishi wa kisiasa Mombasa licha ya kuwa amepanga kuelekeza siasa zake katika ulingo wa kitaifa atakapostaafu ugavana.

Mchanganuzi wa siasa, Prof Halimu Shauri asema kuwa mkono wa ODM kwa matamshi ya Bw Joho ya kumuunga mkono Bw Nassir hauwezi kupuuzwa.

“Joho ni mfadhili mkubwa wa chama cha ODM, kwa hivyo hatuwezi kukwepa uwezekano kuwa kuna mkono wa chama katika uamuzi wa gavana huyo wa kumuunga mkono Bw Nassir,” alisema Prof Shauri.

Prof Shauri aliongeza kuwa kwa sasa inaonekana asilimia kubwa ya viongozi wa chama cha ODM Pwani wanamuunga mkono Bw Nassir na hivyo kuibua hisia kuwa yeye ndiye chaguo la chama.

Hata hivyo, aliongeza kuwa kama chama ni cha kidemokrasia basi uchaguzi wa mchujo uandaliwe kwa njia ya haki.

Kwa mujibu wa mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Pwani, kilicho katika Kaunti ya Kilifi, wanasiasa wengine wanaomezea mate tikiti ya ODM kuwania ugavana Mombasa huenda wakahisi hakutakuwa na haki katika kura ya mchujo ikiwa Bw Joho ataendelea kuonekana anamwandaa Bw Nassir, ilhali yeye ni naibu mwenyekiti wa chama kitaifa.

Hii ni licha ya kuwa Bw Odinga alihakikishia wanasiasa kwamba kutakuwa na uteuzi kwa njia ya haki.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga (kati) akiwa na Waziri Msaidizi (CAS) wa Ugatuzi Gideon Mungaro (kushoto) na mfanyabiashara Suleiman Shahbal. PICHA | MAKTABA

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, msaidizi wa karibu wa Bw Shahbal alisema wao wanafuata kile ambacho kiongozi wa chama anasema, na wala hawatavurugiwa kampeni zao na misimamo ya wanachama wengine kuhusu anayestahili kuwa gavana wa pili wa Mombasa.

“Baba (Bw Odinga) husisitiza wazi kuwa chama hakipendelei mgombeaji yeyote, nasi tunamwamini. Kampeni zetu ni za kutafuta uungwaji mkono kwa wananchi tunaotaka kuwatumikia wala si kwa viongozi wa kisiasa jinsi wanavyofanya wapinzani wetu,” akasema msaidizi huyo wa Bw Shahbal.

Bw Joho huepuka kusema wazi kuwa anamuunga mkono Bw Nassir ila dalili nyingine ambayo huashiria msimamo wake ni jinsi wanasiasa ambao ni wandani wake humpigia debe Bw Nassir.

Hawa ni pamoja na mbunge wa Likoni Mishi Mboko, Seneta wa Mombasa Mohamed Faki, Mwakilishi wa Wanawake Asha Mohamed na Mbunge wa Jomvu Badi Twalib.

Bi Mboko alikanusha dhana ya kuwa wanasukumwa na Bw Joho kumuunga mkono Bw Nassir kuwania kiti cha ugavana.

“Mimi sijasukumwa na Bw Joho kumuunga mkono Bw Nassir, namuunga mkono kwa kuwa ni kiongozi anayestahili kuongoza Mombasa,” Bi Mboko alikuwa ameliambia Jamvi la Siasa.

Bi Mboko alisema kuwa Bw Nassir ni mwezake katika bunge la kitaifa na kwamba amefahamu siasa zake kwa muda mrefu ndiposa alionelea ni kiongozi bora anayefaa kuchaguliwa kuwa gavana wa Kaunti ya Mombasa.

Mbuge huyo wa Likoni alisema kuwa anamuunga mkono Bw Nassir kwa kuwa yeye ni kiongozi ambaye husikiliza watu.

“Bw Nassir akichaguliwa nitakuwa huru kumfikia na tutajadiliana kuhusu maswala yanayowakabili watu wa Mombasa, kiongozi ni vitendo,” alisema Bi Mboko.

Kwa upande mwingine, Bw Shahbal amepata ufuasi wa idadi kubwa ya washauri wa kisiasa ambao walihusika pakubwa katika kampeni zilizopita za Bw Joho, na baadhi ya madiwani wa Mombasa ambao pia ni wandani wa Bw Joho.

Mshauri wa kampeni za kisiasa, Bw Bozo Jenje alisema ingawa mwanasiasa anaweza kunufaika akiungwa mkono na Bw Joho, kuna hatari kwamba watu wanaweza kumdhania Bw Nassir kuwa mradi wa Bw Joho na kushuku sababu za gavana huyo kumsukuma amrithi.

“Iwapo kutakuwa na njia ya kuonyesha kuwa hajawekwa kama mradi wa Joho itakuwa bora kwake, lakini bila hivyo haitaenda vizuri na baadhi ya watu ndiposa inafaa ajionyeshe kama mtu ambaye anajitegemea mwenyewe,” alisema Bw Jenje.

Itakumbukwa kuwa, katika uchaguzi uliopita, ODM ilipoteza viti vya ubunge Kisauni na Nyali licha ya wagombeaji kupiga kampeni pamoja na Bw Joho.

Bw Mohamed Ali ndiye alishinda ubunge Nyali akiwa mgombeaji huru baada ya kuhama ODM akidai kulikuwa na dhuluma katika uteuzi, naye Bw Ali Mbogo akashinda Kisauni kupitia kwa tiketi ya chama cha Wiper.

You can share this post!

UDAKU: Pepeta iwake! Szczesny, Marina waimarisha ngoma...

SOKOMOKO WIKI HII: Kisiasa Savula ni Mudavadi kimwili...

T L