• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:16 PM
Wanaharakati: Serikali ya Ruto ilitumia Sh1 bilioni kusafirisha mawaziri kwa helikopta kupanda miti

Wanaharakati: Serikali ya Ruto ilitumia Sh1 bilioni kusafirisha mawaziri kwa helikopta kupanda miti

NA CHARLES WASONGA

VUGUVUGU la ‘Operation Linda Jamii’ limekosoa hatua ya serikali kuwatuma mawaziri kuongoza shughuli ya upanzi wa miti sehemu mbalimbali nchini, likisema hiyo ni njia mojawapo ya matumizi mabaya ya pesa za umma.

Kwenye kikao na wanahabari Jijini Nairobi Jumatatu, Novemba 13, 2023 kiongozi wake Profesa Fred Ogola alisema kuwa badala ya serikali kutuma mawaziri 22 na maafisa wengine wakuu kuongoza shughuli hiyo, maafisa wa utawala wa mkoa kama machifu na makamishna wa kaunti wangetumika.

“Kwa mtazamo wangu kama mtaalamu wa masuala ya kiuchumi, naona kwamba huo ni ubadhirifu wa pesa za umma kwa serikali kukodisha ndege za helikopta kwa mawaziri kwenda kaunti mbalimbali kuongoza shughuli ya upanzi wa miti. Inagharimu kati ya Sh150, 000 na Sh170, 000 kwa saa moja kukodisha helikopta.

“Kwa hivyo nakadiria kuwa leo hii (Jumatatu, Novemba 13, 2023) serikali imetumia zaidi ya Sh1 bilioni kusafirisha mawaziri huku na kule kuongoza upanzi wa miti ilhali kuna maafisa wa utawala katika maeneo yote nchini; ambao ni maafisa wa serikali kuu,” Profesa Ogola akaambia wanahabari katika jumba la Chester, Nairobi.

Kwa mfano, Waziri wa Usalama Profesa Kithure Kindiki aliongoza shughuli hiyo katika kaunti za Mandera, Wajir, Garissa, Turkana na Marsabit, ambako alifikia kwa helikopta.

Siku ya Jumatatu ilitengwa na serikali kama Siku ya Kitaifa ya Upanzi wa Miti na kutawazwa kuwa siku ya mapumziko.

Serikali ililenga kuhakikisha kwa jumla ya miti 500 milioni ingepandwa Jumatatu pekee kufanikisha azma ya serikali ya kupanda angalau miti 15 bilioni ndani ya miaka 10 ijayo (kufikia 2032).

Profesa Ogola alisema kuwa ajenda ya upanzi wa miti imesukumiwa serikali ya Kenya na mashirika ya kimataifa ya kifedha kama vile; Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Benki ya Dunia (WB).

“Sisi kama Operation Linda Jamii tunahimiza Rais William Ruto kukoma kuingiza masharti ya IMF na Benki ya Dunia katika Sera ya Bajeti ya Serikali (BPS) kwani baadhi ya sera hizo zinaumiza Wakenya,” akasema.

Profesa Ogola aliorodhesha hatua kadha ambazo serikali inaweza kuchukua kuwapunguzia Wakenya mzigo wa kupanda kwa gharama ya maisha.

Miongozi mwa hatua hizo ni kupunguzwa kwa viwango aina mbalimbali za ushuru, kufutiliwa mbalimbali kwa Mamlaka ya Kusimamia Kawi na Mafuta (EPRA), kupunguzwa kwa bajeti ya serikali, kusawazishwa kwa madeni ya kitaifa, kuimarishwa kwa vita dhidi ya ufisadi na kutekelezwa kwa miradi ambayo itaweka pesa mfukoni mwa wananchi moja kwa moja.

“Aidha, tungependa serikali kuiga mfano wa mipango ya usimamizi wa kiuchumi unaokumbatiwa na mataifa kama Singapore, Korea Kaskazini na Malaysia. Nchi hizi zilikuwa katika kiwango sawa cha ukuaji wa kiuchumi na Kenya katika miaka ya 1970s lakini wakati huu zimeipiku taifa letu kimaendeleo,” akasema katika kile alichokitaja kama Taarifa ya Operation Linda Jamii kuhusu Hali ya Taifa.

Profesa Ogola alikuwa ameandamana na Katibu Mkuu wa vuguvugu hilo Calystus Wafula miongoni mwa maafisa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Koome ashangazwa na rundo la kesi 500,000 za wanafamilia...

Arati alipukia kamishna akidai bodaboda ‘wafuasi wake’...

T L