• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 12:42 PM
Arati alipukia kamishna akidai bodaboda ‘wafuasi wake’ wanavamiwa na magenge

Arati alipukia kamishna akidai bodaboda ‘wafuasi wake’ wanavamiwa na magenge

NA WYCLIFFE NYABERI 

GAVANA wa Kisii Simba Arati amemsuta Kamishna wa Gatuzi lake, Tom Anjere kwa ongezeko la visa vya utovu wa usalama.

Bw Arati, mnamo Jumatatu, Novemba, 13, 2023 alitumia hafla ya upandaji miti, iliyofanyika katika eneobunge la Bobasi kumshambulia vikali kamishna Anjere mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Mawasiliano Prof Edward Kisiang’ani, aliyekuwa mgeni wa heshima.

Mbunge huyo wa zamani wa Dagoretti Kaskazini hakuchelewa kumshambulia Bw Anjere na Kamati ya Usalama ya Kisii kwa kile alichodai ni kuzembea kazini katika kukabiliana na mauaji ya kiholela, mengi aliyosema yanaelekezwa kwa wahudumu wa bodaboda, hasa wale ambao ni wafuasi wake.

Akionekana kupandwa na mori, Gavana Arati alimtaka Kamishna Anjere kutuliza hali hiyo na kuwazima wahuni wanaohangaisha wakazi Kisii kwa kushirikiana na kamanda wa polisi wa Kisii Bw Charles Kases.

Akifoka neno baada ya jingine, Bw Arati alidai kuwa baadhi ya wanasiasa walikuwa wakichangia kudorora kwa kiwango cha usalama Kisii.

Cha kustaabisha, alidai vitendo vya wanasiasa hao vinashabikiwa na maafisa wa polisi wanaoshinikizwa kufanya hivyo kwani wanasiasa hao wanajipiga vifua kuwa wamo serikalini.

“Hivi karibuni hali ya usalama haijawa nzuri hasa pale Kisii Mjini. Wanasiasa wameleta siasa chafu. Hakuna vile viongozi wa kisiasa wanaweza kutoa amri kwa karibu vituo vyote vya polisi vilivyomo Kisii,” Bw Arati alilalama.

Bosi huyo wa kaunti alifichua kuwa kuna mbunge mmoja kutoka Kisii (hakumtaja) aliyekuwa akihujumu utendakazi wa polisi wanaokwenda kinyume na anavyotaka.

Gavana Arati alimwomba Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki na Rais William Ruto kuingilia kati.

“Haiwezekani kila mara polisi wanapowakamata wahalifu ambao wanaunga mkono mbunge huyo, wanahamishiwa maeneo mengine yenye kiangazi kwa kuwa mbunge huyo anajipiga kifua kuwa yuko karibu na serikali kuu. Kenya ina serikali ndogo 47 na moja kuu na lazima viongozi wote wa serikali washirikiane. Ndugu yangu meza hugeuka na uongozi huisha. Kawaulize waliokuwa karibu na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta waliko,” Bw Arati aliongeza.

Katibu Kisiang’ani aliwaomba wakazi wa Kisii kuishi kwa amani na kuunga mkono serikali ya sasa.

Prof Kisiang’ani pia alisisitiza haja ya serikali za kaunti kuheshimiwa.

“Rais William Ruto ndiye kiongozi wa taifa na lazima aheshimiwe kwani ndiye aliye mamlakani kwa sasa. Vilevile, Simba Arati ndiye Gavana wa Kisii na lazima pia apewe taadhima zake. Kenya ni nchi ya Demokrasia na kila mmoja yuko huru kuunga mrengo autakao bila kushurutishwa wala kutishwa,” Prof Kisiang’ani alisema.

  • Tags

You can share this post!

Wanaharakati: Serikali ya Ruto ilitumia Sh1 bilioni...

Mnataka kukaa msituni hadi 2032? Gachagua akejeli jamii ya...

T L