• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
Ziara ya Mfalme: Ruto na Rigathi lawamani kwa kunyamazia mahangaiko ya Mau Mau

Ziara ya Mfalme: Ruto na Rigathi lawamani kwa kunyamazia mahangaiko ya Mau Mau

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya Mfalme Charles III wa Uingereza kukosa kuzungumzia malipo kwa Wakenya kutokana na mateso yaliyowakumba wapiganaji wa Mau Mau enzi ya kikoloni, inaonekana kuzima ndoto ya wapiganaji hao kupata fidia kutoka kwa Uingereza.

Kabla ya mfalme huyo kuwasili Kenya mnamo Jumanne, makundi tofauti yalikuwa yamemshinikiza kuomba msamaha kwa mateso ambayo serikali ya kikoloni iliwafanyia wapiganaji wa Mau Mau na kutangaza mikakati ya kuwalipa ridhaa wapiganaji wa vita hivyo waliobakia.

Tume ya Kutetea Haki za Binadamu Kenya (KHRC) ilikuwa imesema wakati umefika kwa kiongozi huyo kulipa waathiriwa wa ukatili wa kikoloni, kwani wengi wao wamekuwa wakipitia hali ngumu kutokana na mateso waliyofanyiwa na askari wa kikoloni wakiwa vizuizini.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bw David Lamber, alisema kuwa karibu miaka sitini baada ya Kenya kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza, suala la mateso mengi ambayo wapiganiaji uhuru walipitia mikononi mwa wakoloni bado halijashughulikiwa ifaavyo.

“Ni kinaya kwamba Uingereza imeendelea kupuuza miito ya kuomba msamaha na kuwalipa fidia wapiganaji wa Mau Mau waliobaki, licha ya juhudi zake kutaka kuendelea kuwa marafiki na Kenya,” akasema Bw Lamber.

Wapiganaji wa Mau Mau, wakiongozwa na Mzee Gitu wa Kahengeri, pia walikuwa wamewarai viongozi wakuu serikali nchini kutumia ziara ya Mfalme huyo kumrai kuhakikisha Uingereza imeomba msamaha na kutoa fidia kwa wapiganaji waliobaki.

“Itakuwa hatua nzuri sana ikiwa Mfalme atakubali ukatili uliotekelezwa na vikosi na maafisa wa kikoloni dhidi ya watu wetu na kuomba msamaha. Huo utakuwa mwanzo mpya kwenye ushirikiano baina ya Uingereza na Kenya,” akasema Mzee Kahengeri, siku chache kabla ya kiongozi huyo kuwasili nchini.

Hata hivyo, ikizingatiwa kuwa kiongozi huyo aliondoka nchini hapo Novemba 3, 2023 bila suala hizo kuzungumziwa hadharani, wapiganaji wengi wanasema kuwa huenda ndoto yao ya kuombwa msamaha na kulipwa fidia na Uingereza imepotea.

Kwenye hotuba aliyotoa Jumatano katika dhifa maalum ya chakula aliyoandaliwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi, Mfalme Charles alieleza “masikitiko yake makubwa kutokana na vitendo vya kikatili vilivyotekelezwa na wakoloni” japo hakuomba msamaha.

“Lazima tutambue nyakati ngumu kuhusu uhusiano wetu wa muda mrefu. Dhuluma za jadi ndizo chanzo cha masikitko makubwa,” akasema Mfalme Charles, bila kuomba msahama kama alivyokuwa ameshinikizwa na baadhi ya makundi.

Rais Ruto, kwenye hotuba yake, alimshukuru Mfalme huyo kwa kukubali na kutambua madhila ambayo wapiganiaji uhuru walipitia mikononi mwa wakoloni.

Hata hivyo, baadhi ya wakongwe walioshiriki kwenye vita hivyo wanasema kuwa Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua “hawakutumia vizuri ziara hiyo kumshinikiza kiongozi huyo kuhusu changamoto nyingi ambazo wapiganiaji uhurui wamekuwa wakipitia.”

Kulingana na Mzee Kabono Mungai kutoka Kaunti ya Nyandarua, na aliyekuwa mmoja wa wapiganiaji uhuru, Rais Ruto na Bw Gachagua “walifeli kutumia vizuri nafasi hiyo kuwatetea”.

“Hii ilikuwa nafasi nzuri kwa viongozi hao wawili kuwasilisha malalamishi yetu kwa Mfalme Charles. Baadhi ya viongozi wamekuwa wakijisawiri kama ‘Watoto na Watetezi wa Mau Mau’. Viongozi hao wanajua changamoto ambazo tumekuwa tukipitia, kwani wamekuwa wakihudhuria mazishi ya wakongwe wa Mau Mau. Wametusaliti. Ndoto yetu kulipwa fidia imepotea,” akasema mkongwe huyo, kwenye mahojiano na ‘Jamvi la Siasa’.

Hata hivyo, wadadisi na wasomi historia wanasema kuwa suala hilo ni nzito, hivyo linahitaji ushiriki wa taasisi nyingi kuliko viongozi wa kisiasa pekee.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi wanaume wanavyolaghaiwa na wanawake ili kulea watoto...

Sauti Sol kupiga densi ya mwisho leo na kuachana rasmi

T L