• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 9:13 AM
Jinsi kampuni inavyowafaa wakulima 8,000 wa pilipili Pwani

Jinsi kampuni inavyowafaa wakulima 8,000 wa pilipili Pwani

Na PETER CHANGTOEK

MALINDI ni mji unaotambulika mno kwa wageni wanaozuru nia ikiwa kuutalii.

Ni mji ulioko umbali wa kilomita takriban 120 kutoka jijini Mombasa.

Hata hivyo, ni katika mji huo ulioko katika Kaunti ya Kilifi, ambako kuna kampuni moja inayowafaa wakuzaji wa pilipili.

Equator Kenya Limited, ni kampuni ambayo imewapa kandarasi wakulima kutoka kaunti za Kilifi na Taita Taveta, pamoja na kaunti nyinginezo ili wawe wakizizalisha pilipili aina ya African Bird’s Eye Chillis (ABE), ambazo inanunua na kuzichakata na kuziuza ughaibuni.

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Almut van Casteren, ni kuwa, wakulima kutoka kaunti kama vile Kilifi na Taita Taveta, walipewa kandarasi ili kuzikuza pilipili aina ya ABE, ambazo inanunua.

Wakulima hao huzikuza pilipili hizo katika mashamba robo ekari na zaidi.

Almut anasema kuwa, mmea wa pilipili ukikuzwa kwa kuzingatia utaratibu unaohitajika, huzaa pilipili kwa mwaka mmoja mfululizo.

“Ni mmea ambao unaweza kuwa na maua, pilipili za njano na nyekundu kwa mwaka mzima. Pia, ni mmea ambao hauwezi kuathiriwa na magonjwa au kuvamiwa na wadudu kwa urahisi,” aongeza Almut.

Ili kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inazipokea pilipili kila wakati, wakulima walipewa kandarasi ya kuzalisha tu aina hiyo ya pilipili.

Kufikia wakati huu, kampuni yenyewe ina wakulima 8,000 waliopewa kandarasi ya kuzizalisha na kuziwasilisha piplipili kwayo.

Baadhi ya wakulima wakiwa na pilipili tayari kuziwasilisha katika kampuni ya Equator. PICHA | PETER CHANGTOEK

Ili kuwapunguzia wakulima gharama ya usafirishaji wa pilipili, kampuni hiyo ina vituo kadhaa ambapo mazao huchukuliwa katika eneo zima la pwani.

Mwasisi wa kampuni hiyo, Jan Willem van Casteren, anafichua kuwa kuhusishwa kwa wakulima ni thibitisho tosha kwamba, maendeleo yanaweza kufanyika kwa kuwashirikisha kwa biashara inayohusu uchakataji wa chakula.

Ili kupata mazao yenye ubora wa kimataifa, kampuni hiyo hutumia teknolojia inayojulikana kama eProd, ambayo hurekodi kila mambo mengi, kuanzia kwa mbegu za pilipili zinazokuzwa hadi mazao yanayozalishwa.

Aidha, teknolojia hiyo, hurekodi maelezo kumhusu mkulima, tarehe kamili ambapo mazao yanawasilishwa, pamoja na bidhaa zinazouzwa ughaibuni.

Mfanyikazi akikagua pilipili katika kampuni hiyo. PICHA | PETER CHANGTOEK

Kwa mujibu wa Almut ni kwamba, mazao yanayouzwa nje ya nchi yanafaa kuidhinishwa na shirika la Global Gap.

Matumizi ya pembejeo kama mbolea na dawa za kunyunyuzia mimea pia ni changamoto.

“Uchakataji wa bidhaa hufanya bidhaa hizo kuafiki viwango bora vinavyohitajika kimataifa,” afichua Almut.

Bidhaa za kampuni hiyo, aghalabu huuzwa katika bara Uropa na bara Asia, na wateja hao wa ughaibuni, mara nyingi, ni wachakataji wa viungo na vya kula.

Kampuni hiyo ina kifaa cha kuzikausha pilipili, na huwapa wakulima mafunzo kuhusu jinsi ya kuzizalisha pilipili zilizo na ubora.

“Kuna aina nyingi za pilipili, na aina zote zina matumizi mbalimbali. Mambo muhimu ni harufu nzuri, rangi, saizi – kwakutaja tu machache,” adokeza Almut.

Wao hupakia bidhaa kwa kilo 25, na huuza kilo 6,300, japohufanyahivyo, maranyingi, kuambatananaodazawateja.

Kupitia kwa teknolojia wanayotumia, Almut anasema kuwa, si lazima wao wawe shambani ili wakutane na wakulima.

Aidha, kupitia kwa teknolojia hiyo, wanaweza kuwasiliana na wakulima na hata kuwapa habari kuhusu hali ya hewa.

Kupitia kwa mradi huo, wakulima wengi katika eneo la pwani wamekuwa na uwezo wa kuwalipia wana wao karo za shule, na kuboresha maskani yao.

Wao huziuza pilipili zao kwa Sh60 kwa kilo moja.

You can share this post!

Kesi ya mauaji ya ndugu wawili wa Embu dhidi ya maafisa...

Kitendawili cha walemavu wengi kijijini chakosa jibu

T L