• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Kitendawili cha walemavu wengi kijijini chakosa jibu

Kitendawili cha walemavu wengi kijijini chakosa jibu

NA MAUREEN ONGALA

KATIKA kijiji cha Mpirani kilicho eneobunge la Magarini, Kaunti ya Kilifi, kuna hali ambayo imegeuka kuwa kitendawili kwa wakazi.

Hiki ni kijiji ambacho kina idadi kubwa zaidi ya walemavu wa rika tofauti, kiasi cha kuwa wakazi na wataalamu wa afya wamekuwa wakijikuna vichwa kuhusu chanzo cha hali hii kwa muda mrefu sasa.

Kulingana na wakazi, wameshindwa kuelewa iwapo hali ya watoto kuzaliwa wakiwa walemavu na vile vile watu wazima kukumbwa na ulemavu inasababishwa na matibabu duni wanayopata katika vituo vya afya nyanjani au kuna tatizo lingine la kimaumbile linalotoka kwa kizazi kimoja hadi kingine.

Hiki ni mojawapo ya vijiji vilivyo maeneo ya ndani mashambani, ambapo hakuna kiwango cha kutosha cha miundomsingi ya huduma za afya inayoweza kusaidia kuwafanyia utafiti bora wa kimatibabu.

Katika mahojiano na Taifa Leo, walieleza kuwa watoto wanapozaliwa huwa wana miili midogo isiyokuwa na nyama ya kutosha huku miguu yao ikiwa miembamba bila misuli.

Wengi wao wanapokua huanza kutembea kwa kutatizika, wasiweze kukunja magoti, huku visigino vyao vikiwa virefu kupita kawaida.

Sasa wametoa wito kwa Wizara ya Afya kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ulemavu huo.

Eneo hilo linakadiriwa kuwa na zaidi ya walemavu 200. Baadhi yao walipelekwa katika kituo cha walemavu cha Magarini ambapo wanapokea usaidizi.

Katika kituo hicho, kuna wanakijiji tisa wa kutoka Mpirani walio na kifafa, tisa wenye changamoto za akili, viwete 69, viziwi 18, vipofu tisa, zeruzeru wawili, wenye matende watatu na bubu sita. Licha ya kuwa wanasema wanawake huwa wanahudhuria kliniki zao bila kukosa wanapokuwa wajawazito, wengi hujifungua watoto walemavu.

Kulingana na mwenyekiti wa kikundi cha walemavu cha Magarini, Bi Simakeni Charo, ambaye ni mzawa wa kijiji cha Madunguni aliyeolewa Mpirani, hali hiyo imekuwa changamoto kubwa kwa wakazi wa eneo hilo huku wengi wao wasijue la kufanya kutokana na umaskini ambao umewakumba.

“Shida yetu ya Mpirani ni changamoto ya walemavu wengi sana takriban 500 wakiwemo watoto, wanawake na wanaume,” akasema.

Bi Charo aliamua kuwaleta walemavu pamoja baada ya kuona shida walizopitia. Ana wajukuu watatu ambao ni walemavu.

Kulingana naye, imekuwa changamoto kwa familia hizo kujitafutia riziki kutokana na hali ya ulemavu ya jamaa zao. Alisema ni hatari kwa familia hizo kuwaacha peke yao kwani wengi wao huwa hatarini kudhulumiwa kijinsia.

Alitoa wito kwa Serikali ya Kaunti ya Kilifi na ile ya kitaifa kuingilia kati na kuwasaidia wakazi ambao wanaendelea kuteseka huku wakiendelea kukosa matumaini maishani.

“Shida hii inayotukumba ni ngumu sana na hatujapata usaidizi wowote kwa hivyo tunataka serikali itusaidie.

Wazazi wamelemewa, wanazaa watoto walemavu wasioweza kwenda hata shambani. Ikiwa baba atatoka kwenda kutafuta chakula, mama atabaki akiwatunza watoto hao kwa sababu hawawezi kubaki peke yao. Ikiwa atakosa, basi watalala njaa,” akasema.

Mahitaji muhimu

Alisema kuwa gharama za matibabu zimechangia familia nyingi kukosa pesa za kutosha kujenga nyumba nadhifu za kuishi na pia kugharimia mahitaji mengine muhimu ikiwemo lishe bora.

Mara kwa mara, wakazi wa eneo hilo hulazimika kuchanga pesa kwa ajili ya kuwasaidia walemavu kununua dawa. Lakini, licha ya wanakijiji hao kujitotolea kuchanga, kiwango wanachopata huwa kidogo sana kwa sababu wao pia wanakumbwa na umaskini wa kupindukia.

Bi Charo anaendelea kueleza kuwa, mateso wanayopitia yamefanya walemavu wengi kuapa kutopiga kura.

“Walemavu katika eneo hili wametengwa. Wanasiasa wanasubiri wakati wa kura tu na hili linatuhuzunisha.

Lakini wameapa kuwa hawatapiga kura tena kwa sababu matakwa yao hayatekelezwi,” akasema.

Imesemekana kuna idadi kubwa ya walemavu ambao wamekufa kutokana na hali zao za maisha Alisema pia kuna haja kwa serikali kufanya utafiti wa chanzo cha ulemavu na pia kuwekeza katika kuhakikisha kuwa vituo vya afya nyanjani vina vifaa vya kisasa vya kuwachunguza kinamama wajawazito ikiwemo mashine ya kupiga picha.

“Ni lazima wajawazito wachunguzwe kwa kina kwa sababu watoto wengi wanazaliwa na ulemavu. Je, ulemavu huu unatoka wapi?” akasema.

Bw Ndokolani Badi ana ulemavu wa miguu yake baada ya kukumbwa na ugonjwa usiojulikana kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Malengelenge

Kulingana na Mzee Badi, alianza kuwashwa na kisha kupata malengelenge kwenye miguu hali ambayo ilianza kuathiri vidole vyake na vikaanza kukatika.

Hali hiyo ilisambaa mwili wote na kuchangia kukatwa kwa mguu wake wa kushoto. “Sijui kilichosababisha malengelenge hayo na miguu yangu kuathirika. Tunaomba serikali itusadie kupata matibabu kwa sababu tunateseka sana,” akasema.

Alisema kwa sasa, anamtegemea mkewe kutafuta chakula na mahitaji mengine. Kabla ya kuwa mgonjwa, Mzee Badi alikuwa akifanya kazi mjini Mombasa.

Bi Eunice Boki, 29, alizaa watoto watano walemavu. Kati yao, wawili waliaga dunia. Anaeleza kuwa hangeweza kujua kilichochangia kuzaa watoto walemavu ambao mikono na miguu yao haijikunji.

“Nilienda kliniki tangu nilipokuwa na ujauzito wa miezi mitatu lakini bado nilizaa watoto walemavu. Kila mara daktari alinipima na kunieleza kuwa mtoto yuko sawa tumboni,” akasema. Kiongozi wa kundi la kina mama katika Kaunti ya Kilifi, Bi Caroline Chi – lango, alisema ni vigumu kwa wakazi hao kubaini chanzo cha changamoto hiyo kwa sababu wanaishi kijijini.

Alisema watoto wengi wameshindwa kwenda shuleni kwa sababu ya changamoto ya ulemavu ikizingatiwa kuwa wengi wao hawajasajiliwa kwa mradi wa Inua Jamii.

Utafiti

“Hakuna kiwanda wala ma – ji machafu ambayo wakazi hawa watasema yanasababisha ulemavu.

Suluhisho litapatikana tu kupitia kwa utafiti wa kutosha,” akasema.

Anatoa wito kwa baraza linashoghulikia masuala ya walemavu nchini kuhakikisha wanazingatia masuala ya walemavu hao ikiwemo huduma bora za afya.

Kwa sasa wakazi hao wanategemea huduma kutoka katika zahanati ya Marekebuni. “Kuna hatari ya kupoteza walemavu zaidi ikiwa hatutaboresha hospitali zetu nyanjani kuhakikisha wanapata huduma bora,” akasema Bi Chilango.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Kilifi, Bw Charles Dadu, alisema wanafa – hamu kuna vijiji kadhaa kaunti hiyo vinavyokumwa na changamoto ya ulemavu ambayo sio ya kawaiada.

Bw Dadu alisema kuwa wizara ya Afya inaendeleza uchunguzi kubainisha sababu za ulemavu katika maeneo hayo.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi kampuni inavyowafaa wakulima 8,000 wa pilipili Pwani

Chager achukua uongozi wa EA Safari Classic Rally siku ya...

T L