• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 5:55 AM
Kesi ya mauaji ya ndugu wawili wa Embu dhidi ya maafisa sita wa polisi yaanza kusikizwa

Kesi ya mauaji ya ndugu wawili wa Embu dhidi ya maafisa sita wa polisi yaanza kusikizwa

Na RICHARD MUNGUTI

KESI ya mauaji ya ndugu wawili kaunti ya Embu dhidi ya maafisa sita wa polisi ilianza kusikizwa Jumatano huku shahidi akikiri hakuwaona washtakiwa wakitekeleza kifo hicho.

Akitoa taarifa ya utangulizi kiongozi wa mashtaka Bi Tabitha Ouya alisema atawasilisha ushahidi kuthibitisha Benson Mputhia, Consolata Njeri, Martin Wanyama, Nicholas Sang, Lillian Cherono na James Mwaniki walihusika na mauaji ya kinyama ya Benson Njiru Ndwiga na Emmanuel Mutura Ndwiga.

Bi Ouya alimweleza Jaji Daniel Ogembo kuwa washtakiwa hao walitekeleza mauaji ya ndugu hao usiku wa Agosti 1,2021 kisha wakadai “walijirusha kutoka kwa gari ya polisi ikienda kasi wakaanguka barabarani wakapasuka vichwa.” Jaji Ogembo alifahamishwa ushahidi utakaowasilishwa dhidi ya polisi hao maarufu kama “Kianjakoma Sita” utathibitisha ni wao na sio wengine walio waua Emmanuel na Benson.

Bi Ouya alisema maafisa hao wa polisi walikuwa wamepanga kuwaua ndugu.Mahakama ilielezwa ushahidi utawasilishwa kuthibitishwa washtakiwa walitekeleza mauaji hayo ya kinyama. Akitoa ushahidi John Mugendi Njeru alimweleza jaji kuwa mnamo siku hiyo Benson alimpigia simu na kumweleza walikuwa wanafunga buchari yao.

“Benson alinipigia simu mwendo wa saa moja unusu. Tuliungana nao tukaenda kilabu kwa jina Mamur ambapo nilibugia jagi moja ya pombe (keg). Benson na Emmanuel hawakulewa,” alisema Mugendi. Mugendi alisema mama ya ndugu hao aliwapigia simu na kuwataka waende nyumbani.

Mahakama ilifahamishwa wakitoka kilabuni walikuta polisi wakishika doria. “Benson alituamuru tukimbie tusishikwe na polisi kwa vile masaa ya kafiu yalikuwayamefika,” Mugendi alikumbuka Katika harakati za kutoroka Emmanuel aliteleza na kuanguka kwa vile kulikuwa kuna manyunyu.

“Wacha kuokota kiatu tukimbikie,”Benson alimweleza nduguye. Mugendi alisema alikimbia akajificha kwenye shimo lakini alikuwa anaona kinachoendelea. “Benson alirudi mahali nduguye alikuwa ameanguka walipofukuzwa na afisa wa polisi aliyekuwa ameshika rungu,” Mugendi alisema.

Mugendi alisema afisa huyo aliyekuwa ameshikarungu alimchapa Benson bengani kisha akamsukuma na kumwigza ndani ya gari. “Nilisikia Emmanuel amegongwa akatoa sauti “puuuu”,” alisema Mugendi. Akihojiwa na wakili Danstan Omari anayewatetea maafisa hao wa polisi, Mugendi alisema hakushuhudia polisi hao wakiwaua ndugu hao na wala hakurudi kuwaona ndugu hao tena.

Mugendi alisema ndani ya gari hilo la polisi aliwaona watu wawili waliokuwa wameshikwa kwa kukaidi sheria za kafyu za kutokuwa nje baada ya saa nne usiku. Kafyu ilikuwa imetangazwa na Rais Uhuru Kenyatta kupunguza kuenea kwa ugonjwa wa Corona.

Siku iliyofuatwa, Mugendi alisema alifahamishwa na watu wa boda boda (piki piki) kwamba Emmanuel na Benson waliuawa.

You can share this post!

Muuzaji bangi na chang’aa aona cha mtema kuni

Jinsi kampuni inavyowafaa wakulima 8,000 wa pilipili Pwani

T L