• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Hospitali mpya zimehudumia wagonjwa 16,000 jijini – Ripoti

Hospitali mpya zimehudumia wagonjwa 16,000 jijini – Ripoti

Na COLLINS OMULO

WAGONJWA 16,200 wamehudumiwa katika hospitali nne mpya zilizofunguliwa na Idara ya Huduma katika jiji la Nairobi na kupunguzia wakazi wa mitaa ya mabanda mzigo wa matibabu.

Hospitali hizo zilizofunguliwa mwezi mmoja uliopita zimepunguzia presha Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, (KNH) na Mama Lucy Hospital.

Hospitali hizo nne – Muthua-Uthiru, Ushirika-Dandora, Kiamaiko na Kayole-Soweto- zilifunguliwa na Rais Uhuru Kenyatta mwishoni mwa Februari.

Hospitali hizo zilizo na vitanda 16 ni sehemu ya hospitali 24 za viwango vya Level 2 na Level 3 zinazojengwa katika mitaa ya mabanda jijini Nairobi kwa gharama ya Sh 2 bilioni.

Kulingana na takwimu za kitengo cha afya cha NMS, tangu hospitali nne zilipofunguliwa, jumula ya wagonjwa 16,208 wametibiwa humo.

Hospitali ya Uthiru ilihudumia wagonjwa 5,974, Kayole-Soweto wagonjwa 3,774, Ushirika hospital wagonjwa 3,541 na Kiamaiko wagonjwa 2,919.

Kufikia Machi 1 2021, wanawake 41 walijifungua katika hospitali hizo 17 wakiwa Uthiru, 11 katika hospitali ya Kayole-Soweto, wanane katika hospitali ya Kiamaiko na watano katika hospitali ya Ushirika.

Wagonjwa 737 walitafuta huduma za kliniki za akina mama wajawazito na baada ya kujifungua wengi wao katika hospitali za Uthiru na Kayole-Soweto.

Wengine 750 wametafuta huduma za mpango wa uzazi katika hospitali hizo , 1,380 huduma za chanjo na 718 huduma za maabara na 1,771 huduma zinazohusiana za lishe bora.

Hata hivyo, wengi walikuwa ni walio na umri wa zaidi ya miaka mitano takwimu zikionyesha walikuwa 6,963. Wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka mitano walikuwa 3,796.

You can share this post!

Jinsi sheria inavyoweza kuliweka taifa katika giza kipindi...

LISHE: Jinsi ya kuandaa chips masala