• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
JUNGU KUU: Hatari ya Mlima kutengwa na rais

JUNGU KUU: Hatari ya Mlima kutengwa na rais

NA WANDERI KAMAU

ENEO la Mlima Kenya liko hatarini kutengwa kisiasa baada ya uchaguzi mkuu wa Jumanne, kwa kukosa kuwa na chama kimoja cha kisiasa.

Wadadisi wa kisiasa wanasema kuwa eneo hilo liko hatarini kujipata kwenye “baridi” ya kisiasa, bila kuzingatia mwaniaji urais atakayeshinda baina ya Naibu Rais William Ruto na Bw Raila Odinga, anayewania kwa tikiti ya muungano wa Azimio-One Kenya.

Wadadisi wanasema kuwa kukosekana kwa chama kimoja cha kisiasa katika eneo hilo, kumelifanya kama “yatima” kisiasa, hali inayolifanya kukosa usemi wa pamoja.

“Viongozi wa kisiasa wa Mlima Kenya wanafaa kufahamu kuwa Bw Odinga na Dkt Ruto ni washindani wa kisiasa wanaofahamiana kwa undani. Wawili hao washawahi kuhudumu katika chama cha ODM katika jukwaa la ‘Pentagon’ mnamo 2007, Bw Odinga alipokuwa akiwania urais. Hivyo, si nadra wawili hao kuungana tena kisiasa baada ya Agosti 9,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana na wadadisi, huenda msukumo wa “handisheki” ya pili kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto ikawa usaliti wa kisiasa waliofanyiwa na viongozi wa ukanda huo.

Wanasema kuwa licha ya Rais Uhuru Kenyatta kumuunga mkono Bw Odinga, hilo halijaponya ‘kovu’ la kisiasa alilo nalo, kwani amesalitiwa mara mbili.

Mara ya kwanza, ni wakati alipomuunga mkono marehemu Mwai Kibaki mnamo 2002 kuwania urais kwa tikiti ya muungano wa Narc.

Wakati huo, Bw Odinga ndiye aliongoza kampeni za Rais Kibaki kupitia kauli ya “Kibaki Tosha”, marehemu huyo alipojeruhiwa ajalini.

Bw Odinga aliungana na Bw Kibaki pamoja na wenzake kama marehemu William ole Ntimama, Prof George Saitoti, Kalonzo Musyoka, David Musila kati ya wengine, waliokuwa katika chama cha Liberal Democratic Party (LDP).

Kwa upande wake, Bw Kibaki alikuwa amebuni muungano wa National Alliance of Kenya (NAK) pamoja na Gavana Charity Ngilu (Kitui) na marehemu Wamalwa Kijana, aliyekuwa akiongoza chama cha Ford-Kenya.

Kulingana na wadadisi, Mzee Kibaki na washirika wake “walimsaliti” Bw Odinga licha ya kuongoza kampeni za kuvumisha azma yake ya urais alipokuwa amelazwa hospitalini jijini London, Uingereza, kufuatia ajali aliyopata karibu na mji wa Machakos wakati wa kampeni zake.

“Kulingana na Mkataba wa Maelewano (MoU) uliokuwepo kati ya Bw Kibaki na Bw Odinga, wawili hao wangeibadilisha Katiba na kubuni nafasi ya Waziri Mkuu, ambayo angepewa Bw Odinga. Hata hivyo, Bw Kibaki alimgeuka. Hiyo ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya ghasia zilizotokea mnamo 2007,” asema Dkt Geoffrey Sang’, ambaye ni mwanahistoria na mchanganuzi wa siasa.

Anasema hiyo ndiyo iliyokuwa mara ya pili kwa familia ya Bw Odinga ‘kusalitiwa’, baada ya Mzee Jomo Kenyatta kumsaliti babaye Bw Odinga, Jaramogi Oginga Odinga miaka ya 60.

Kwa upande wake, Dkt Ruto amesalitiwa na Rais Kenyatta licha ya kumuunga mkono mara tatu; mwaka 2002 alipowania urais kwa tikiti ya Kanu, mwaka 2013 na 2017.

Zaidi ya hayo, wanasema eneo hilo pia “limemsaliti” kisiasa kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kwani Mzee Kibaki alikuwa ameahidi kumuunga mkono mnamo 2013, kwa kuongoza harakati za kuyarai mataifa tofauti duniani kujiondoa kama wanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Hili lilitokana na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu yaliyowakabili Rais Kenyatta na Dkt Ruto katika mahakama hiyo.

Katika hali hiyo, wadadisi wanasema ikiwa wawili hao wataungana, basi itawalazimu viongozi wa ukanda huo kufutilia mbali tofauti zao za kisiasa na kuungana tena ili kuhakikisha hawatatengwa kisiasa tena, kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa marehemu Daniel arap Moi.

“Ili kuepuka hali kama hiyo, lazima viongozi kama Bi Martha Karua na mgombea-mwenza wa Dkt Ruto, Rigathi Gachagua, kufutilia mbali tofauti zao za kisiasa ili kuhakikisha kuwa eneo hilo halijatengwa kisiasa ikiwa Bw Odinga na Dkt Ruto watabuni ‘handisheki’ ya ‘RaiRuto’,” akasema Dkt Sang’.

Anaeleza kuwa licha ya uwepo wa Rais Kenyatta katika Baraza Kuu la Muungano wa Azimio, hilo huenda likakosa kuzuia eneo hilo kutengwa kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Wanasiasa wamemaliza yao, uamuzi sasa ni wako

UJAUZITO NA UZAZI: Kutokwa damu ukiwa mjamzito

T L